test

Tuesday, July 26, 2016

Hatua iliyochukuliwa na serikali kuhusu madereva 18 waliogoma Bukoba

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesitisha leseni za madereva 18 kutokana na mgomo walioufanya kupinga wenzao kupelekwa mahakamani.

Wamiliki wa mabasi 12 ambayo madereva hao walikuwa wanaendesha kwenda sehemu mbalimbali nchini, wamepewa siku saba kujieleza ni kwa nini wasifutiwe leseni za kutolea huduma hizo pamoja na kutakiwa kusitisha ajira kwa madereva hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema Julai 23 mwaka huu mkoani Kagera, madereva wa mabasi hayo walifanya mgomo kupinga kitendo cha madereva wenzao kupelekwa mahakamani, kukosa dhamana na kulala rumande kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo kuendesha kwa mwendo kasi.

Kamanda Mpinga alisema dereva yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya zaidi ya kilometa 90 kwa saa atafikishwa mahakamani na sio kutozwa faini kama awali ili kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza safari zake kwenye Manispaa ya Bukoba, walisitisha huduma kwa kushinikiza Mahakama iwaachie wenzao waliokamatwa kwa makosa ya mwendo kasi.

‘’Serikali haitavumilia kuona madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani na sheria za kazi na ajira. Jeshi la Polisi ndio tunawapa madereva mafunzo, tunasajili vituo vya mafunzo na kuwapa leseni. Hivyo tunasitisha leseni zao kwa mujibu wa sheria kwa kukiuka kanuni za leseni,’’ alisema Mpinga na kuongeza kuwa askari watakaoachia madereva na kampuni za mabasi kutembea kwa zaidi ya kilometa 90 kwa saa watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe, aliyataja mabasi pamoja na madereva waliositishiwa leseni kuwa ni Hussein Tegatega na Miraji Kondo wa Kampuni ya RS Express wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 425 DDT aina ya Zongtong linalotoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.

Said Omary na Amos Danney wa basi la Kimotico lenye namba za usajili T 966 CDY aina ya Nissan linalotoka Bukoba kwenda Arusha na madereva wanne wa mabasi ya Princess Muro yenye namba za usajili T 166 DCA na T 923 DCT yanayosafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.

Madereva hao ni Ally Mshuza, Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.

Madereva wengine ni Musa Tindwa na Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 968 CPC linalofanya safari zake Bukoba kwenda Dar es Salaam na Paul Ngussa wa basi lenye namba za usajili T 810 BDW aina ya Scania linalotoka Bukoba kwenda Musoma, mali ya Kampuni ya Bunda Express.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU