test
Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

Monday, May 28, 2018

Rais Na Mwenyekiti Wa CCM Dr Magufuli Aongonza Mkutano Wa Halmashauri Kuu Ya Taifa (NEC) Ya CCM Jijini Dar Es Salaam Leo

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli  akiwa meza kuu katika Ukumbi wa mikutano wa Kikwete katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ukumbi wa Kikwete leo Jumatatu Mei 28, 2018  

Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahman Kinana wakati akisoma muhtasari wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Katika ukumbi wa Kikwete jijini Dar es salaam leo Jumatatu Mei 28, 2018
Wajumbe wakishangilia baada ya  Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli kuwaita  Ndg. Mizengo Pinda na Ndg. Makongoro Nyerere waingie ukumbini baada ya kukubaliwa kuwa wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi wa Kikwete jijini Dar es salaam leo Jumatatu Mei 28, 2018

Vilio Vyatawala Bungeni....Bunge Laahirishwa Hadi Kesho

Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson leo asubuhi ameahirisha Bunge mpaka kesho saa tatu asubuhi kupisha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Buyungu Mwl. Kasuku Bilago aliyefariki siku ya Jumamosi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
 Vilio na simanzi vilitawala katika ukumbi wa Bunge kutokana na kifo hicho cha Mbunge huyo wa Chadema aliyefariki dunia Jumamosi Mei 26. 

“Waheshimiwa wabunge, Spika wa Bunge mheshimiwa Job Ndugai  anasikitika kuwatangazia kifo cha mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kilichotokea juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa mujibu wa kanuni zetu, leo shughuli za Bunge hazita endelea na badala yake tutakuwa na maombolezo,” amesema Naibu Spika.

Wakati Naibu Spika Ackson akitoa taarifa za msiba na kuahirisha Bunge, wabunge Julius Kalanga (Monduli), Suzan Kiwanga (Mlimba), Halima Mdee (Kawe) na Dk Semesi Sware (Viti Maalum ) wote wa Chadema walikuwa wakilia.

Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) alishindwa kabisa kujizuia na wabunge walilazimika kumpa usaidizi.

Naibu Spika Dkt. Tulia amesema kuwa Wabunge watakao kwenda kuwakilisha kwenye mazishi hayo wataondoka Dodoma siku ya Jumanne asubuhi na kurejea Dodoma Jumatano mara baada ya mazishi hayo kumalizika.

Pamoja na hayo, Naibu Spika ameendelea kwa kusema "siku ya kesho tutakuwa na kikao cha Bunge kama kawaida isipokuwa tutahairisha Bunge saa sita mchana ili kutoa fursa kwa shughuli za heshima za mwisho kwa mwili wa marehumu Bilago na baada ya hapo tutaendelea na maombelezo hadi siku ya Jumatano".

ACT Wazalendo Wahoji Matumizi Fedha Za Korosho

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kupeleka haraka asilimia 65 ya fedha za mauzo ya nje ya korosho ghafi kwa Bodi ya Korosho ili zitumike kama zilivyokusudiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema kutokupeleka fedha hizo kutasababisha gharama za uzalishaji kwa wakulima kuongezeka kutokana na ununuaji wa pembejeo kutegemea kwa asilimia 100 katika fedha hizo.

Alisema jambo hilo lilitokea mwaka jana kupanda kwa dawa aina ya salfa (Sulphur) katika maeneo mengi kutoka Sh 16,000 hadi kufika Sh 70,000.

“Kwa mujibu wa sheria ya korosho namba 18 ya mwaka 2009 kifungu 17(A), inaitaka Serikali kuingiza fedha hizo Bodi ya Korosho lakini fedha hizo hazijapelekwa kwa miaka miwili sasa,” alisema Shaibu.

Alisema hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Korosho iliyotolewa na kamati ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo kwa misimu miwili ya mauzo ya korosho, bodi haijapokea fedha hizo na hivyo kuleta athari mbalimbali katika kilimo hicho.

Aliongeza kuwa taarifa hiyo inadai kuwa Bodi ya Korosho haijapokea Sh bilioni 211 ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 wanadai Sh bilioni 91 na 2017/18 wanadai Sh bilioni 110.

“Kutopeleka fedha hizi kutaathiri Kituo cha Utafiti cha Naliendele kinachozalisha mbegu bora za korosho na dawa za kudhibiti magonjwa ambacho kinategemea fedha hizo kwa asilimia 90 kujiendesha kitashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi,” alisema Shaibu.

Aliongeza kuwa athari nyingine ni kuvurugika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu ya usimamizi wa mfuko huo kutegemea fedha hizo kwa asilimia 100.

“Mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima na maofisa ugani yamesimama kwa sasa kutokana na kukosekana kwa fedha hizo,” alisema Shaibu.

Alisema wanamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kulitolea ufafanuzi suala hili ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Shaibu, alisema umefikia hatua ya majimbo na kitaifa utafanyika Agosti 25 hadi 27, mwaka huu jijini Mbeya.

Alisema chama hicho kinapinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga, aliyoitoa hivi karibuni bungeni kuwa suala la uanachama wa Sahara Magharibi lina utata wa kisheria katika Umoja wa Afrika na katika duru za kimataifa.

“Tunapinga kauli hii kwa kuwa Tanzania tumekuwa mstari wa mbele kuwasaidia kupata uhuru wa Sahara Magharibi chini ya chama cha ukombozi cha Polisalio,” alisema Shaibu.

Akizungumza hivi karibuni, Waziri Mahiga, alisema Polisalio ni chama cha ukombozi kilichopewa hadhi ya Serikali na uanachama wa Umoja wa Afrika tangu 1982, lakini suala hilo limeanza kuleta utata kisheria.

Sunday, May 27, 2018

Lema alipongeza Bunge, akomaa na Stahiki za Tundu Lissu

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefunguka kuwa bado wanaendelea kutafakari suala la Mbunge wa Sigida Mashariki Tundu Lissu kuhangaika na kutafuta misaada ya matibabu kwa watu mbalimbali duniani, kwani Bunge bado linatafakari kuhusu stahiki zake, haki na gharama za matibabu.

Mhe. Lema amezungumzia hayo ikiwa ni siku moja tangu kutokea kwa kifo cha Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago aliyefariki wakati akipatiawa matibabu katika hospitali ya Taifa, Muhimbili.

Lema amesema "Mwili wa Marehemu Mhe. Bilago umepata heshima, haki na stahiki ya Kibunge, tumefanya kikao tena Kati ya Bunge, Chama na Familia, wema wa Bunge kwa mwili wa marehemu umekuwa ni wa kifani".

Ameongeza "Wakati tunalishukuru Bunge kwa wema huu, bado tunaendelea kulitafakari la rafiki yetu Lissu aliyeko Ubeligiji".

Lissu ambaye anatibiwa nchini Ubelgiji alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 9, 2017 maeneo ya Area D akiwa anatokea katika majukumu yake ya kikazi bungeni Dodoma.

Sababu za Lissu kutotibiwa na Bunge ziliwekwa wazi na Spika wa Bunge, Job Ndugai  siku moja baada ya tukio hilo ambapo alisema kuwa utaratibu wa matibabu kwa mbunge ulikuwa umeshafuatwa lakini familia pamoja na chama  waliamua kumpeleka Nairobi, na siyo kama wao walishindwa kumpeleka nchini India.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefunguka kuwa bado wanaendelea kutafakari suala la Mbunge wa Sigida Mashariki Tundu Lissu kuhangaika na kutafuta misaada ya matibabu kwa watu mbalimbali duniani, kwani Bunge bado linatafakari kuhusu stahiki zake, haki na gharama za matibabu. Mhe. Lema amezungumzia hayo ikiwa ni siku moja tangu kutokea kwa kifo cha Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago aliyefariki wakati akipatiawa matibabu katika hospitali ya Taifa, Muhimbili. Lema amesema "Mwili wa Marehemu Mhe. Bilago umepata heshima, haki na stahiki ya Kibunge, tumefanya kikao tena Kati ya Bunge, Chama na Familia, wema wa Bunge kwa mwili wa marehemu umekuwa ni wa kifani". Ameongeza "Wakati tunalishukuru Bunge kwa wema huu, bado tunaendelea kulitafakari la rafiki yetu Lissu aliyeko Ubeligiji". Lissu ambaye anatibiwa nchini Ubelgiji alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 9, 2017 maeneo ya Area D akiwa anatokea katika majukumu yake ya kikazi bungeni Dodoma. Sababu za Lissu kutotibiwa na Bunge ziliwekwa wazi na Spika wa Bunge, Job Ndugai siku moja baada ya tukio hilo ambapo alisema kuwa utaratibu wa matibabu kwa mbunge ulikuwa umeshafuatwa lakini familia pamoja na chama waliamua kumpeleka Nairobi, na siyo kama wao walishindwa kumpeleka nchini India.

PICHA: Rais Magufuli Alivyokutana na Kufanya Mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Kinana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Mei, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahman Kinana, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli alipokea salamu kutoka kwa viongozi wa chama na Serikali wa Afrika Kusini na Zimbabwe ambako hivi karibuni Ndg. Kinana aliongoza ujumbe wa viongozi wa CCM kutembelea nchi hizo na kukutana na viongozi wakuu wa vyama tawala vya ANC na ZANU-PF vinavyoongoza Serikali.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli na Ndg. Kinana wamezungumzia maandalizi ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) vitakavyofanyika  tarehe 28-29, Mei, 2018 Jijini Dar es Salaam.

Thursday, May 24, 2018

Sugu Ampongeza Mwandosya kwa Kumtembelea Gerezani

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu (Chadema), ameliambia Bunge kuwa wakati akiwa gerezani, alipokea salamu kutoka kwa viongozi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akimpongeza Prof. Mark Mwandosya kwa kuwa mwana CCM pekee aliyekwenda kumsalimia gerezani.

Akichangia bungeni jijini Dodoma jana mjadala wa makadirio ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka ujao wa fedha, Sugu aliwapongeza viongozi na wabunge wa CCM kwa kumtumia salamu gerezani huku akidai wengi wao waliogopa kwenda kumjulia hali.

Hata hivyo, Sugu alisema CCM waliwakilishwa vizuri na waziri wa zamani Prof. Mwandosya ambaye ndiye pekee wa chama tawala hicho aliyefika gerezani kumjulia hali.

Mbunge huyo ambaye jana alikuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo, pia alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa wananchi wa Mbeya ambao alidai waliungana naye kutumikia kifungo hicho.

"Nawashukuru watu wote waliopaza zauti zao kulaani kifungo dhidi yangu," alisema Sugu katika maneno yake ya utangulizi kabla ya kujikita katika hoja iliyokuwa bungeni.

Mbunge huyo mwanzoni mwa mwaka huu alihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani baada ya kukutwa na hatia kisha kuachiwa wiki mbili zilizopita kwa msamaha wa Rais.

Katika mchango wake jana, Sugu alisema matukio ya uhalifu na vifungo dhidi ya wanasiasa kama yeye yanayotokea nchini yanawafanya baadhi ya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini.

Alisema pamoja na kwamba Tanzania inaweza kuwa na jitihada za kuwashawishi wawekezaji kutoka nje kuwekeza nchini, mkakati huo huenda usifanikiwe kwa kuwa wawekezaji wanapenda kuwekeza katika nchi zenye usalama kuliko nchi zenye vurugu na mauaji.

Sugu pia alimshauri Rais aanze kusafiri kwenda nje ya nchi akisisitiza kuwa safari za nje zina faida kama ilivyokuwa enzi za uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyekuwa akisafiri mara kwa mara.

“Pamoja na hayo, serikali haiwatendei haki Watanzania wanaoacha kazi nje na kuja kufanya kazi nchini kwa sababu inataka iwalipe mishahara midogo kama ilivyotokea kwa bosi mmoja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)," Sugu alisema.

Musukuma amkana Bashe Sakata la Kutekwa na Usalama wa Taifa

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma Kasheku, amefungukia madai yaliyowahi kutolewa na Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe, kwamba walitekwa na watu wa usalama wa Taifa ni ya uongo na kwamba kilichotokea walikamatwa na askari na mbinu zilizotumika ni zile wanazofundishwa bungeni.

Musukuma ametoa kauli hiyo jana  wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa na  EATV , ambapo alifafanua kwamba walikuwa wakidhaniwa kufanya uhalifu.

Musukuma alisema kwamba "Mara ya kwanza kulala polisi nimelala nikiwa mwana- CCM, mara ya kwanza Dodoma, mara ya pili ni Geita, na nilikubali kwa sababu wala hatukutekwa, nilikuwa na kina Bashe, nilimsikia rafiki yangu Hussein Bashe alisema tumetekwa, hatukutekwa".

"Tulikamatwa tukapelekwa polisi, tukapekuliwa, tulipoonekana hatuna hatia tukaachiwa , hatukutekwa. Sikumjibu Hussein Bashe aliposema tumetekwa kwa sababu sikuwepo, nasema hapa hatukutekwa," Musukuma.

Aprili 11, 2017 Mbunge wa Nzega Mjini(CCM) Hussein Bashe aliwataka wabunge kuacha unafiki kuhusu Usalama kuwateka watu na kwamba yeye ni mmoja wa watu waliokamatwa wakati wa mkutano Mkuu wa CCM.

"Mimi nimekamatwa na kuteswa na Usalama wa Taifa. Nimenyanyaswa sana nchi hii. Ikibidi mnifukuze CCM - " alisema Bashe wakati Waziri wa Tamisemi,(kabla hajaenguliwa katika nafasi hiyo) George Simbachawene kumtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuthibitisha kuwa matukio ya ukamataji yanafanywa na usalama wa Taifa.

Wednesday, May 23, 2018

Msukuma: Kuna Baadhi ya Wizara Zinatia Kichefuchefu na Kila Nikiwaona Mawaziri Wake Natamani Kukimbia

Mbunge wa Geita Vijijini Mh. Joseph Musukuma amesema baadhi ya Wizara ni kichefuchefu na kuna Waziri hata akifumba macho akifumbua akamuona anakimbia kutokana na anavyofanya kazi zake katika Wizara anayoongoza ndio maana baadhi wamepata taabu kupitisha Bajeti zao Bungeni.

Akiongea jana Mei 23, kwenye kipindi cha Kikaangoni cha EATV , Musukuma aliwataja baadhi ya Mawaziri wanaozitendea haki Wizara zao kuwa ni Waziri William Lukuvi wa Ardhi na Ummy Mwalimu wa Afya.

''Unajua sio kila Wizara unachangia tu zingine zimekamilika hata Mawaziri wake waliposimama kusoma Bajeti zao ili zipitishwe hakuna aliyepinga, lakini kuna Waziri hata ukinifumba macho nikifumbua tu nikamuona nakimbia'', amesema.

Musukuma alisema baadhi ya Mawaziri wamekuwa wakifanya kazi kwa mihemuko ndio maana wao kama wabunge wanajitahidi kuwashauri wanapokuwa wameenda tofauti.

Aidha ameeleza kuwa kitendo cha Wabunge kushauri vitu kadhaa Bungeni hawamaanishi lazima wasipitishe bajei ila wanachofanya ni kushauri kisha kupitisha ili serikali ikafanyie kazi ushauri wao.

Msukuma: Wanaolisema Vibaya Jeshi la Polisi Wanakosea....Siku Likiacha Kazi Watu Watabakana bila Kutongozana

Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Musukuma, amesema kwamba watu wanaomsema Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kuhusu watu wasiojulikana na wanao likashifu jeshi la polisi na kulituhumu kwa mambo yasiyofaa wanalikosea jeshi hilo, kwani bila wao tusingekuwa salama.

Musukuma ameyasema hayo jana alipokuwa akiongea na East Africa Television, na kusema kwamba iwapo jeshi la polisi likiacha kazi kufanya kazi hata kwa siku moja hakutakuwa na amani, kwani watu watafikia hatua ya kubakana bila kutongozana.

“Ilitengenezwa tu chuki kuwa watu wasiojulikana wanatumwa na Makonda, sijui na nani!! Mara polisi, hii dhana si nzuri, haya matukio yametokea sehemu nyingi, Kibiti huko, sijui wapi huko, ila mnalichafua tu jeshi la polisi , Siku jeshi la Polisi likisema liache kufanya kazi, hali itakuwa mbaya, hatutatongozana tutabakana.”, alisema Musukuma.

Sambamba na hilo Musukuma amesema watu wanaofanya hivyo hawako sahihi, kwani badala yake wanapaswa kulishukuru jeshi hilo kwa jukumu la kuwalinda wao na mali zao.

Waziri Mkuu: Tanzania Inahitaji Wawekezaji ili Kupata fursa ya mitaji na teknolojia za kisasa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inahitaji wawekezaji na kupitia kwenye uwekezaji, inapata fursa ya mitaji na teknolojia za kisasa.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Mei 23, 2018) wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Alfayo Kidata ambaye alifika kumuaga kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amemtaka Balozi Kidata atumie fursa ya uwepo wake nchini Canada kuangalia namna ya kuisadia nchi kuimarisha sekta za kilimo, madini na utalii.

“Tukiimarisha sekta hizi, uchumi ndani ya nchi unakua lakini pia tunategemea kutumia nchi rafiki kukuza uchumi wetu wa ndani kwa maana ya kukuza mitaji na kupata teknolojia za kisasa,” amesema.

“Ukienda huko mkakati wako mkubwa uwe ni kuzingatia mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano lakini zaidi mkakati wetu wa kukuza uchumi wa viwanda,” amesisitiza.

Amemtaka Balozi huyo akasimamie pia suala la upatikanaji wa masoko kwa ajili ya mazao yanayozalishwa nchini ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Hapa nyumbani tuna mazao matano ambayo tumeazimia kuyafufua lakini masoko ya ndani hayatoshi, kwa hiyo kazi yako mojawapo ukiwa huko ni kututafutia masoko,” amesema.

Waziri Mkuu amemweleza Balozi Kidata azingatie pia suala zima la kuongeza idadi ya watalii. “Tunataka ukasaidie kutangaza nchi yetu ili watalii waje kuona vivutio vyetu. Tunataka kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni mbili ya sasa hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2020,” amesema.

Alimtaka Balozi huyo akafuatiilie pia fursa za masomo kwa ajili ya Watanzania wanaotaka kusoma Canada na Cuba. 

“Nilipoongea na Makamu wa Rais wa Cuba, aliahidi kuongeza idadi ya Watanzania wanaotaka kusomea udaktari. Kwa hiyo, ukifika itabidi ufuatilie ahadi hiyo,” ameongeza.

Waziri Mkuu pia alimsisitizia Balozi Kidata akifika huko awatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio Canada na awahamasishe wafanye kazi ili waweze kuwekeza nyumbani.

Kwa upande wake, akizungumza baada ya kuagana na Waziri Mkuu, Balozi Kidata alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa na Waziri Mkuu.

Alisema anatambua kwamba Canada ina idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na atafanya juhudi zaidi za kuitangaza Tanzania ili waje kuona vivutio vilivyopo nchini. Pia atafuatilia fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa Kitanzania.

“Kwenye suala la uchumi wa viwanda, tunahitaji kuwa na uzalishaji wa mazao ya kutosha. Kwa hiyo tunahitaji kuwana kilimo cha uhakika na cha muda wote kuliko. Tunahitaji kupata utaalamu na mitaji kwa ajili ya mashamba ya umwagiliaji,” alisema.

Alisema kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji, kutasaidia kuwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi zitazakotumika kwenye viwanda.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Lukuvi, Mengi Wakutana Kujadili Fursa za Uwekezaji

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekutana na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dkt. Reginald Mengi ili kuzungumza na kutambua fursa zinazopatikana za uwekezaji katika sekta ya Ardhi nchini.

Dkt. Mengi amekutana jana na Mhe. Lukuvi ofisini kwake kanda ya Dar es salaam ambapo walijadili mambo mbalimbali ambayo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeyafanya katika sekta ya ardhi  na kutoa fursa  kwa wawekezaji wa ndani kuwekeza kwa urahisi.

Halima Mdee ataka wenye vyeti feki kuonewa huruma

Mbunge wa Kawe (Chadema),  Halima Mdee ameitaka Serikali kuwa na huruma na watumishi wake iliowaondoa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti feki.

Mdee ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Mei 23, 2018 wakati akiuliza swali la nyongeza, kubainisha kuwa  kuna watumishi waliotumia vyeti vya watu wengine kujiendeleza kielimu na wamefanya kazi kwa uadilifu mkubwa.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Angellah Kairuki ambaye wakati wa uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma ukianza alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) amesema hakuna malipo wala huruma yoyote itakayotolewa kwa wafanyakazi hao.

" Mdee mdogo wangu na dada yangu wewe ni mwanasheria lazima ujue kuwa hakuna kitu kama hicho kwa hiyo Serikali haiwezi kuwalipa au kuwapa msamaha," amesema Kairuki.

Amesema kwa kuzingatia maelezo hayo, mjadala huo utakuwa umefungwa kwani waliostahili kurudi kazini walisharudishwa.

Waziri Makamba Awatoa Hofu Watanzania mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge

Baada ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge katika Pori la Akiba la Hifadhi ya Selous kutikisa Bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka Watanzania kutulia na kubainisha kuwa tathmini ya mradi huo inafanyika.

Makamba ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 23, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio Clouds.

Jana bungeni mjini Dodoma mradi huo ulikuwa gumzo wakati wabunge wakijadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2018/19, ambapo baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi akiwemo Nape Nnauye (Mtama) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), walitaka tathmini ifanyike kabla ya kuanza kwa mradi huo.

Wamehoji kitendo cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutangaza tenda ya kukata miti katika pori hilo, tenda inayohusisha ukataji miti zaidi ya mita za ujazo 3,495 na kwamba idadi ya miti inayokatwa ni sawa na ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam huku ikijulikana  wazi kuwa tathmini bado haijakamilika.

Katika maelezo yake ya leo, Makamba amesema  tathmini inafanyika ili kujua athari  na namna ya kukabiliana nazo, “lazima sheria ifuatwe ikiwamo kufanya tathmini ya athari ya mazingira, ndicho kinachofanyika hivi sasa kuhusu mradi huo.”

“Tanesco walikuja NEMC (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira)  kusajili mradi wa Stigle’s Gorge ili kufanya tathmini ya mazingira. Baada ya kuandikisha Tanesco walimchagua mshauri ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ni kazi ya kisayansi.”

Makamba amesema tayari shirika hilo limeshapeleka ripoti katika ofisi yake baada ya kufanya tathmini hiyo na kinachofuata ni NEMC  kutuma timu kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu yaliyoandikwa katika mradi na yanayoonekana kama ni kweli.

Amesema baada ya hapo kamati ya ufundi ya ushauri itazungumza  na wadau wote katika eneo la mradi na kuthibitisha taarifa zilizopo kuhusu mradi husika.

Bajeti Maliasili na Utalii yapita, mradi wa Stigle’s Gorge watikisa

Sakata la mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge ambao utekelezaji wake unafanyika katika pori la akiba la Hifadhi ya Selous, liliibuka tena bungeni jana jioni Mei 22, 2018 na kuzua mvutano  huku Spika Job Ndugai akieleza kutoridhishwa na majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Suala hilo lilitikisa Bunge jana mchana baada ya wabunge kadhaa kuhoji utekelezaji wa mradi huo, kueleza athari za kimazingira zinazoweka kujitokeza.

Selous ni miongoni mwa mapori yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (Unesco) kama sehemu ya urithi wa dunia, lakini uamuzi wa Serikali kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 ikitumia zaidi ya Dola 2bilioni (zaidi ya Sh4.5trilioni) unaelezwa kuwa huenda ukaliondoa pori hilo kwenye orodha hiyo.

Bunge lilipokaa kama kamati jana jioni kupitisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2018/19 ya Sh115bilioni, mbunge wa Ulanga (CCM), Godluck Mlinga alianza kwa kuhoji kama Serikali itakuwa na mkakati mzuri wa kuwasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Hoja ya Mlinga iliungwa mkono na Ndugai aliyeitaka Wizara ya Nishati kuwa makini na kutengeneza utaratibu wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali yanayoanzishwa miradi ya umeme.

Ndugai amesema katika maeneo mengi Wizara hiyo imekuwa na utaratibu wa kukata miti mingi katika utekelezaji wa miradi lakini inakosa usimamizi wa upandaji miti mingine.

“Mheshimiwa Mlinga  naamini kuwa wamekuelewa lakini na ninyi Nishati lazima muwe na mipango mizuri ya kupanda miti katika miradi yenu. Haiwezekani unakata miti lukuki lakini hakuna mpango wa kuipanda hiyo haikubariki kabisa,” amesema Ndugai.

Ndugai ambaye pia aliungwa mkono na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kwa pamoja walipingana na majibu ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuhusu upandaji wa miti katika eneo hilo.

Wakati wawili hao wakitaka kusikia majibu ya Serikali kuhusu utunzaji wa mazingira katika eneo hilo, ikiwa ni sambamba na kupanda miti baada ya kuikata iliyopo, Dk Kalemani hakuwa akitoa majibu ya kina kuhusu hoja yao hiyo.

Katika majibu yake Dk Kalemani alisema miradi inayoanzishwa itakuwa na mipango mizuri hata ya uhifadhi wa mazingira, huku akijikita zaidi kueleza mpango wa kuongeza nguvu ya uzalishaji umeme nchini.

“Yaani Waziri hujatuelewa kabisa tunachotaka sisi ni hii  miti mingi mnayokata halafu mnakusanya na hampandi mingine, hivi hamjui habari ya uhifadhi kweli basi nimemaliza, nimemaliza waziri usisimame tena,” alisema Ndugai baada ya waziri huyo kuomba kujibu tena huku wabunge wakipinga.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola alisema mradi huo hauna madhara kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, akijitokeza mtu akaupinga atafungwa  bila huruma.

Tibaijuka: Kwa Hili Serikali ni Lazima Iwajibike.....Utawala wa Sheria Uheshimiwe

Mbunge wa Muleba Kusini(CCM), Profesa Anna Tibaijuka ameitaka serikali ya awamu ya tano iwajibike kuwanunulia ng'ombe wafugaji walioshinda kesi zao Mahakamani kama sheria inavyosema nasio vinginevyo.

Prof. Tibaijuka ametoa kauli hiyo jana  Mei 22, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 34 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasiri na Utalii ya mwaka 2018/19 ambayo ni shilingi 115.8 bilioni baada ya kuwepo tatizo la muda mrefu kwa wafugaji kuporwa mifugo yao na watu wa maliasili pindi wanapokuwa wamevamia hifadhi kwa lengo la kulisha mifugo yao.

"Serikali hii ya awamu ya tano naishukuru sana walitoa miezi 10 kwa Mawaziri humu ndani Bungeni kutafuta ardhi za wafugaji lakini hiyo kazi haikufanyika kilichotokea watu walikuja kuondolewa kwenye hifadhi kama operesheni na kwa kweli yalikuwa mateso makubwa sana. Mhe. Spika ni utawala wa sheria kama mtu ameshinda mahakamani na anatakiwa arudishiwe mifugo yake ni lazima afanyiwe hivyo na kama haipo lazima inunuliwe, serikali hapo inatakiwa kuwajibika", alisema Tibaijuka.

Pamoja na hayo, Prof. Tibaijuka aliendelea kwa kusema "kuwajibika hakuwezi kuwa sehemu ya wananchi pekee yake bali na serikali yenyewe lazima iwajibike pale ambapo kosa limefanywa na watendaji wake".

Kwa upande mwingine, Profesa Anna Tibaijuka amesema hawezi kuiunga hoja iliyokuwa mezani mpaka pale suala lake litakapopatiwa majibu yenye kuridhisha.

Sugu alitetea Jeshi la Magereza Bungeni

Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi 'Sugu' amelitetea Jeshi la Magereza mbele ya  Bunge  kuwa jeshi hilo lina matatizo makubwa ya kiusafiri jambo ambalo linapelekea wafungwa kupelekwa Mahakamani kwa miguu kitendo ambacho kina hatarisha usalama wa mfungwa na askari kiujumla.

Kauli hiyo ya Sugu imetolewa jana  Mei 22, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 34 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

"Pamoja na matatizo waliyokuwa nayo Jeshi la Polisi katika masuala ya vyombo vya usafiri lakini niwahakikishie Jeshi la Magereza lina hali mbaya sana, hawana magari sio tu magari mabovu hawana magari kabisa, kiasi kwamba wanafikia hatua ya kuwapeleka wafungwa ambao wanakesi Mahamani kwa miguu huku wakiwa wamewafunga pingu. Hii ni mbaya sana kwa usalama wa askari magereza pamoja na wale watuhumiwa ambao wamefungwa pingu", alisema Sugu.

Pamoja na hayo, Sugu aliendelea kwa kusema "mtu anatuhumiwa ujambazi halafu anapitishwa mtaani kwa miguu wananchi wanamuona, wanaweza wakamvamia na kumshambulia pamoja na kuhatarisha maisha ya mfungwa".

Kutokana na ushauri huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba akampongeza Mhe. Sugu kwa kusema "nimpongeze Mhe. Sugu kwa kuuliza swali kwa experience, na niseme kwamba yeye ni mshauri mzuri. Tutalizingatia hilo ili tuweke mgao kwenye upande wa Jeshi la Magereza ili kuepuka na tahadhari aliyosema".

Sababu Zilizofanya 'Makontena ya RC Paul Makonda' Yakose Masamaha wa Kodi

Kitendo cha nyaraka za makontena 20 yenye samani yaliyo katika hatari ya kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato (TRA) mwezi ujao kuwa na jina la mtu binafsi Paul Makonda,ni moja ya sababu zilizomkwamisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusamehewa ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kama alivyoomba, imefahamika.

Kwa mujibu wa barua ya Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango kwa 'RC' Makonda ya Machi 24, mwaka huu kwa mujibu wa sheria, shehena hiyo ya samani haistahili kupata msamaha wa ushuru wa forodha au bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa sababu kadhaa ikiwamo kuonekana kuwa mali ya mtu binafsi.

Makonda aliiandikia wizara barua Januari 3, mwaka huu akiomba msamaha wa kodi kwenye samani za shule za Mkoa wa Dar es Salaam zenye thamani ya "takribani" Sh. bilioni 1.4 ambazo alidai ni msaada kutoka kwa wananchi wapenda maendeleo waishio Marekani.

Ombi hilo hata hivyo limekataliwa na Waziri Mpango kwa kuzingatia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014.

Barua ya Dk. Mpango inasema kwa mujibu wa Sheria ya VAT, msamaha kwa taasisi za Serikali ni kwa shughuli zisizo za kibiashara, "kwa masharti kwamba usiwepo uwezekano wa shughuli kama hiyo kutolewa na taasisi isiyo ya kiserikali".

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Wizara ya Fedha, samani kama hizo zinaweza kutolewa na taasisi isiyo ya kiserikali au mtu binafsi hivyo kuwa nje ya eneo la msamaha.

Aidha, Makonda amekataliwa msamaha wa kodi kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa siyo asasi ya kiraia au taasisi ya kidini, barua hiyo inasema na kufafanua:

"Magazeti ya Serikali namba 205 na 206 ya mwaka 2016 yanatoa misamaha ya ushuru wa forodha na wa bidhaa kwa asasi za kiraia na taasisi za dini kwa vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya kuendeleza, kuanzisha au kukarabati miradi inayolenga elimu, usambazaji maji, huduma za afya na miundombinu."

Viti, meza na mbao za darasani vinavyodaiwa kuwamo katika mzigo wa Makonda vinaonekana kuangukia nje ya jedwali hilo.

Mbali na majibu kwa Makonda, nakala ya barua ya Waziri Dk. Mpango imepelekwa pia Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Tamisemi, Wizara ya Fedha na TRA.

Alipoulizwa jana kwa njia ya simu kama Makonda alipokea barua hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwipaja hakuweza kuthibitisha.

Lakini alionyesha kushangazwa kwake kusikia "barua iliyonakiliwa kwa Waziri Mkuu ipo mitandaoni?"

Mwanzoni mwa wiki iliyopita TRA ilitangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Makonda ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 zitakazomalizika katikati ya mwezi ujao.

Katika tangazo hilo, Kamishna wa Idara ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa, alitoa siku 30 kwa wamiliki wa mali mbalimbali zilizopo katika ghala la TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya muda huo zitapigwa mnada kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa forodha.
Credit: Nipashe

Tuesday, May 22, 2018

Ripoti ya Ufisadi Mali za CCM Yatua kwa Rais Magufuli

Tume ya kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoundwa na Rais John Magufuli, imebaini madudu ukiwamo utapeli na usimamizi mbaya wa mali hizo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais Magufuli kukagua mali za chama hicho, imefanya kazi hiyo kwa miezi mitano ambapo imekusanya taarifa, kuhakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk. Bashiru Ally, amesema tume yake pia ilibaini usimamizi mbovu wa mali za chama.

Akielezea namna tume hiyo ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo mengine, tume iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.

Katika ripoti hiyo, Dk. Bashiru ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

“Uhakiki huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” amesema.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.

“Nilipokuwa nateua tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.

Wabunge Wa CUF Wamfagilia Rais Magufuli ....Wasifu Kasi Yake Na Waziri Mkuu Ya Uletaji Maendeleo

WABUNGE watatu kutoka Chama cha Wananchi (CUF) mikoa ya Lindi na Mtwara wamepongeza kasi ya utendaji kazi ya Rais John Pombe Magufuli katika kutatua kero za wananchi wa mikoa hiyo.

Wabunge hao Bw. Selemani Said Bungara (Kilwa Kusini), Bw. Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) na Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) walitoa pongezi hizo jana, (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati walipopewa nafasi ya kusalimia wananchi kwenye mikutano ya hadhara ambayo Waziri Mkuu alihutubia.

Akiwa wilayani Lindi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuzindua kituo cha kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa katika kijiji cha Mahumbika, aliwapa fursa wabunge wote alioambatana nao katika ziara hiyo maalum kwa ajili ya uzinduzi wa miundombinu ya nishati kwa mikoa ya Kusini.

Akizungumza na wananchi na viongozi wa taasisi mbalimbali mkoani humo waliohudhuria uzinduzi huo, Mbunge wa Kilwa Kusini, Bw. Bungara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Lindi alisema analishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuisimamia vizuri Serikali ya CCM.

“Faida ya demokrasia ya vyama vingi ni kwamba CCM bila CUF, CCM hakuna na CUF bila CCM, kama ambavyo hakuna Simba bila Yanga wala hakuna Yanga bila Simba. Tuwe kitu kimoja tu, Kusini kwanza, vyama baadaye!” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa juhudi zake za kuwaunganisha wabunge wa mikoa ya Kusini bila kuwabagua au kujali itikadi zao.

Naye Mbunge wa Liwale, Bw. Kuchauka alisema: “Niwapongeze wewe Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais Magufuli kwa yale ambayo mnayasimamia na mnaamini kwamba yataleta ukombozi kwa wananchi wa Tanzania. Lazima nikiri kwamba wakati mnazindua sera ya uchumi wa viwanda, nilikuwa siamini katika hiyo sera yenu kwa sababu niliona ni moja ya mbinu zenu za kututenga sisi watu wa mikoa ya Kusini.”

“Niliona hivyo kwa sababu nilijiuliza unawezaje kuwa na uchumi wa viwanda wakati huna nishati ya uhakika ya umeme? Sasa nimeona mwanga kwamba mikoa ya Kusini nayo inaweza kushiriki kwenye uchumi wa viwanda,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema hivi sasa hakuna asiyeona mambo yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano kwani dunia yote imekuwa kama kijiji na lolote linalofanywa na Mhe. Rais au Waziri Mkuu hakuna asiyejua. “Lolote analolifanya Mheshimiwa Rais au wewe Waziri Mkuu Watanzania wote watalijua, hakuna asiyeliona. Hivi sasa hakuna haja ya kubishana nani kafanya nini, jambo kubwa ni kuungana na tuangalie Tanzania yetu. Vyama vyote baadaye, Kusini kwanza,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Bw. Maftaha alisema mwaka 2006 baada ya kuhitimu kidato cha sita, alipangiwa afanye mafunzo ya ualimu kwa vitendo katika shule ya sekondari Mingoyo, eneo la Mnazi Mmoja lakini alitafuta nyumba ya kuishi yenye umeme hakupata.

“Wakati ule nyumba zenye umeme zilikuwa hazizidi hata 10, na kulikuwa na simba na wadudu wa kila aina. Leo nafarijika kuona kwa kasi ya ajabu, ninyi viongozi tuliowapa dhamana, mnatumia rasilmali za nchi hii, mnasambaza umeme kwa wananchi wa mikoa ya Kusini, na pale Mnazi Mmoja leo hii, umeme siyo tatizo tena.”

Wabunge wengine waliofuatana na Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bibi Hawa Ghasia; Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bi. Hamida Mohammed Abdallah (Viti Maalum). Mbunge wa Nachingwea, Bw. Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nanyamba, Bw. Abdallah Dadi Chikota.

Waziri Mkuu alizuru pia mkoa wa Mtwara na kukagua ujenzi wa bandari, ukarabati wa mabomba ya kupokelea mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta, kuzindua upanuzi wa kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa bandari.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU