test
Showing posts with label KIMATAIFA. Show all posts
Showing posts with label KIMATAIFA. Show all posts

Monday, May 28, 2018

Korea Kaskazini Yasisitiza Ipo Tayari Kwa Mazungumzo na Marekani

Ni nia ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un kuwa mkutano kati yake na Rais wa Marekani Donald Trump uendelee, imeeleza taarifa ya vyombo vya habari vya Korea Kaskazini.

Hii ni kutokana na mkutano wa kushtukiza wa siku ya Jumamosi kati ya Kim na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in.

Rais Trump alisitisha mkutano uliopangwa kufanyika tarehe 12 mwezi Juni kuzungumzia mpango wa nuklia wa Korea Kaskazini, lakini alisema Jumamosi kuwa mambo yanaendelea vizuri sana

Wakati huo huo ujumbe wa Marekani uliripotiwa kwenda Korea Kaskazini siku ya Jumapili.

Balozi wa zamani wa Marekani nchini Korea Kusini, Sung Kim, atafanya mazungumzo na naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini kuhusu maandalizi ya mkutano, vyombo vya habari vya Marekani na Korea Kusini vimeeleza.

Mkutano huo ni matunda ya jitihada za kidiplomasia ambazo zilianza mwaka huu kujaribu kuondoa hali ya msuguano uliohofiwa kugeuka kuwa makabiliano ya kijeshi kati ya Korea Kaskazini, Korea Kusini, na Marekani.
Credit:BBC

Saturday, May 26, 2018

Mo Salah atacheza World Cup? Daktari wa timu atoa neno hili.

Mtanange wa yule Bingwa wa Ulaya umekamilika. Real Madrid wameshinda taji lao la tatu mfululizo kwa ushindi wa mabao matatu kwa moja. Golikipa wa Liverpool Karius akisababisha uzembe ulioigharimu timu hao baada ya kurusha mpira kimakosa na ukagomga Benzema aliyegfunga bao la kwanza kabla ya Mane kusawazisha. unga magoli mawili. Bale alitokea benchi na kufunga mabao mawili.

Niliwahi kusema kinyago cha Gazzaniga (Kombe la Dunia) kiliwanyima mastaa wengi usingizi. Majeraha ilikuwa changamoto kubwa sana kwa wachezaji wa pande zote.
kilichotokea leo ni kitu ambacho wengi tulitarajia kutapoteza ladha ya mchezo huu.

Mo Salah ambaye alikuwa mchezaji tegemezi wa Liverpool hivi leo atolewa kwenye mchezo mapema kabisa baada ya kuumia bega. Ilikuwa ni kashkash kati yake yeye na Sergio Ramos. Ramos alikwenda kumkaba Salah na ilionekana wakishikana mkono. Picha na video zinaonesha kuwa alimvuta mkono na kumsababisha Salah kuondoka vibaya na kulalia bega lake.

Je wachambuzi wakubwa wanasemaje?
Rio Ferdinand
Ramos amekaba vyema. Alifanya kitu ambacho mlinzi yeyote angefanya. Sidhani kama alidhamiria.
Frank Lampard
mnapokuwa mmesogeleana sana mara nyingi ni rahisi sana kushikana mikono. ile ni bahati mbaya sana.

Rio na Lampard hawa ni waingereza na wana haki ya kutoa Maoni yao. Jana nilimsikia David Beckham aliweka pembeni sana suala la Uzalendo. Na aliweka mapenzi yake dhahiri kuwa Real inafaa iifunge Liverpool. Rio nae ni hasimu mkubwa wa Liverpool. Bila shaka ukiangalia ile video utagundua hakuna ajali. kuna tofauti kubwa ya kushikana na kumvuta mtu kwa makusudi ukidhamiria.

John Simpson anasema hivi
Nimeangalia maoni ya wachambuzi wakubwa, wanasema lile tukio ni ajali. Sawa. Lakini ukimwangalia Ramos wakati Salah anatolewa nje utagundua alidhamiria.

kuna baadhi ya video zinamuonesha Ramos akitabasamu na Mwamuzi wa pembeni.
David Maddock anasema
Inauma sana. Ramos amefanya kitendo cha kikatili haswa. Hajaharibu tu ndoto za Salah za Uefa pia huenda ameharibu ndoto wa Wamisiri wote.

Mo Salah taarifa zinasema mishipa ya bega imeachana. Na majibu kamili yatatolewa wakirudi jijini Liverpool. Hii inaleta wasiwasi mkubwa kama atahitaji kufanyiwa upasuaji. na itamlazimu kukosa michuano ya kombe la dunia.

hata hivyo taarifa za hivi punde zinasema kuwa ukurasa wa timu ya taifa ya Misri umeweka taarifa kuwa Mo Salah atacheza michuano ya kombe la dunia

Thursday, May 24, 2018

Wanawake 40 Kunyongwa Iraq

Serikali inatarajia kuwanyonga wachumba 40 wa wanamgambo wa Dola ya Kiislamu (IS) kulipiza kisasi kwa wapiganaji hao wa jihadi kuikalia kwa miaka mitatu ardhi ya Iraq wakati wa mapigano yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa kikatili.

Wanawake hao ambao ni wa kigeni walikiri mahakamani kwamba na wao ni waathirika wa IS, walipewa dakika 10 kila mmoja kutetea uhai wao kabla ya majaji kufikia uamuzi wapewe adhabu kali.

Wanawake hao walishutumiwa na mahakama ya Iraq na raia wa kawaida kwa kuwapa msaada waume zao wapiganaji waliosababisha maafa katika eneo walilokuwa wanakalia kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.

Mwanamke mmoja mwenye uraia wa Ufaransa aitwaye Djamila Boutoutao, 29, alidai kuwa alidhani alikuwa anaolewa na mwanamuziki wa miondoko ya rap.

“Ni baada ya kuwasili Uturuki kwa ajili ya ‘mapumziko’ ya wiki moja ndipo nilipogundua ya kuwa mume wangu ni mpiganaji wa kijihadi,” alisema Djamila.

“Mimi ni mwathirika. Mume wangu alinipiga na kunifungia kwenye pango na watoto wangu nilipokataa kumfuata (hadi Iraq).’

Djamila ni mmoja wa raia wa Ufaransa wapatao 1,900 na wasafiri wa kigeni wanaokadiriwa kuwa 40,000 waliosafiri hadi Syria na Iraq kujiunga na miliki ya khalifa.

Katika hukumu yake ya hivi karibuni, ambako aliomba asitenganishwe na binti yake, Djamila aliwaambia waandishi wa habari wa gazeti la The Guardian: “Nachanganyikiwa hapa. Nakabiliwa na adhabu ya kifo au kifungo cha jela maisha. Hakuna anayeniambia chochote, si balozi wetu wala watu ndani ya gereza.”

“Jamani nawasihi msiwaache waondoke na binti yangu. Niko tayari kuwapa fedha endapo mtawasiliana na wazazi wangu. Tafadhali niokoeni.”

Takriban wanawake 40 ndio wamehukumiwa kifo na watu wengine 300 wenye mafungamano na IS wameshauawa.

Wednesday, May 23, 2018

Facebook Yaendelea Kuomba Msamaha

Mkurugenzi wa Facebook Mark Zuckerberg ameomba msamaha kwenye Bunge la Ulaya kutokana na madhara yaliyosababishwa na kuvuja kwa data za watumiaji wa mtandao huo na pia kwa kushindwa kupambana na habari za uongo/ feki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg aliomba msamaha kwa watumiaji wa Ulaya wa mitandao ya kijamii na kuahidi kupambana na habari feki za uongo  na vile vile ameahidi kwamba data za watumiaji hao zitalindwa vyema.

Zuckerberg alifika mbele ya viongozi wa makundi ya kisiasa wa Bunge la Ulaya baada ya Facebook kukubali kwamba ilitoa taarifa binafsi za watumiaji wapatao milioni 87 kwa kampuni ya Cambridge Analytica ya nchini Uingereza, zikiwemo zile za watumiaji karibu milioni 2.7 kutoka kwenye nchi za Umoja wa Ulaya. Facebook ilikubali kwamba ilitoa taarifa hizo binafsi kwa njia isiyo sawa.

Hata hivyo Zuckerberg aliyakwepa baadhi ya maswali magumu aliyoulizwa na wabunge hao, na kisha kuomba msamaha kutokana na sera za Facebook zilizorahisisha kuenea kwa habari feki wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2016 na pia katika matokeo ya kura ya maoni juu ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Ulaya hata hivyo wamelalamika kwamba Zuckerberg hakutoa majibu halisi juu ya matumizi mabaya ya data za mamilioni ya watumiaji wa mtandao huo. 
Jan Philipp Albrecht, mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia ulinzi wa data za Umoja huo (GDPR) amesema ipo haja ya kuwepo ulinzi mkubwa.

Mjumbe huyo maalum anayeshughulikia masuala ya ulinzi wa data katika Umoja wa Ulaya amesema pia uangalizi unahitajika zaidi kwenye shughuli za mtandao huo wa Facebook, kwa mfano katika kuitenganisha Facebook na WhatsApp au Facebook Messenger ambapo hatua kama hiyo sasa itakuwa ni chaguo la mtu binafsi . Bwana Albrecht amesema hilo ni moja kati ya maswali ambapo Mark Zuckerberg hakutoa majibu ya kina.

Zuckerberg ameomba msamaha kwa niaba ya kampuni yake kwa kushindwa kuzuia kutumiwa vibaya baadhi ya mifumo yake ya internet huku wengi wa wabunge waliokuwepo katika mahojiano hayo wakisema bilionea huyo wa Facebook alishindwa kutoa majibu yaliyoweza kuwatoa wasiwasi walio nao.

Mfumo wa kujibu maswali ulimruhusu Zuckerberg kujibu maswali hayo mwishoni, na hivyo kuwaacha wabunge wakiwa wamekata tamaa kutokana kushindwa kupata majibu ya moja kwa moja kwa maswali yao.

Rais wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani alimwambia Zuckerberg kwamba kufika kwake kumetoa ishara muhimu ya heshima  yake kwa Bunge hilo pamoja na wananchi wa Ulaya.

Iran yaendelea kupinga masharti ya Marekani

Iran imeendelea kupinga masharti kutoka Marekani ya kufanyia mabadiliko sera yake ya kigeni na mpango wake wa nyuklia huku mshirika wake Syria, ikitupilia mbali wito wa Marekani kuviondoa vikosi vya Iran nchini humo.

Ufaransa, mmoja ya mataifa yenye nguvu barani Ulaya, iliosikitishwa na hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa nyuklia uliyotiwa saini mwaka 2015, imesema hatua ya Marekani ya kuiongezea vikwazo zaidi Iran, itawaimarisha zaidi wanasiasa wenye msimamo mkali nchini Iran.

Jumatatu wiki hii waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo aliitishia iran kuwa itakabiliwa na vikwazo zaidi katika historia iwapo haitaachana na ushawishi wake wa kikanda, akiishutumu nchi hiyo kuunga mkono makundi ya silaha katika mataifa kama vile Syria Lebanon na Yemen.

Pompeo aliyasema haya wiki mbili baada ya rais Trump kujiondoa katika mpango wa kimataifa wa nyuklia wa Iran, uliopelekea taifa hilo kuondolewa vikwazo kufuatia hatua yake ya kukubali kusitisha uendelezaji wa mpango huo. 
Mataifa yenye nguvu barani Ulaya yanauona mkataba huo kama nafasi nzuri ya kuizuwia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Pompeo amerejelea shutuma za zamani dhidi ya nchi yake ila safari hii shutuma hizo zimetolewa kwa ukali zaidi.

Naye afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran Meja jenerali Mohammad Bagheri, amesema Iran haitaisujudia Marekani katika shinikizo lake la kudhibiti shughuli zake za kijeshi. 
Mjini Paris, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba huo wa nyuklia na kuiwekea Iran vikwazo itazidisha misimamo mikali na kuhatarisha eneo hilo.

Le Drian amesema Ufaransa itaendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba huo hata kama inakubaliana na Marekani kwamba shughuli za nyuklia za Iran pamoja na makombora  zinapaswa kudhibitiwa.

Huku hayo yakiarifiwa Syria imetupilia mbali wito wa Marekani wa kuviondoa vikosi vya Iran nchini humo. Katika vita vya Syria vilivyodumu miaka 7, Iran imekuwa ikitoa msaada muhimu kwa  jeshi la serikali ya Bashar al Assad.

Kim Jong-un azidi kumvuruga Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump ametilia shaka kuhusu kufanyika kwa mkutano na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un mwezi june mwaka huu huko Singapore.

Ameyasema hayo mara baada ya Korea Kaskazini kutishia kujiondoa katika mkutano huo endapo Marekani itaendelea kusimamia msimamo wake wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Aidha, Rais Trump hakuweka wazi ni masharti gani ambayo yamewekwa kwa ajili ya mkutano huo,na alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya masharti aliyoiwekea Korea Kaskazini amesema kuwa suala la kuachana na silaha za nyuklia ni lazima litekekelezwe na Korea Kaskazini.

Mkutano kati ya rais Trump na Kim Jon-un uanatarajiwa kufanyikwa June 12 nchini Singapore ukitanguliwa na mkutano wa marais wa Korea hizo mbili uliofanyika mwezi April.

Hata hivyo, ameongeza kuwa mwelekeo wa Kim Jong-un umebadilika baada ya ziara yake ya pili mwezi huu nchini China.

Thursday, May 17, 2018

Trump Amgeuka Mshauri Wake Kuhusu Kuifanya Korea Kaskazini Kama Libya

Rais wa Marekani, Donald Trump amepinga kauli ya mshauri wake mkuu wa masuala ya ulinzi, John Bolton aliyedai kuwa mfumo wa kuondoa silaha za kinyuklia nchini Korea Kaskazini utafanana na uliotumika Libya.

Tump amesisitiza kuwa makubaliano kati ya Marekani na Korea Kaskazini yanayotarajiwa kuanza katika mkutano kati ya viongozi wa nchi hizo mbili, uliopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu hayana mlengo wowote wa mfanano na aliyoyasema Bolton.

“Mfumo uliotumika Libya sio mfumo ambao tunaulenga tunapofikiria suala la Korea Kaskazini,” alisema Trump.

Rais Trump alifafanua kuwa anachofikiria ni kuhakikisha Korea Kaskazini inafuata mfumo wa Korea Kusini katika kuleta maendeleo baada ya kuondolewa vikwazo. Aliwasifu watu wa Korea Kaskazini kuwa ni watu wazuri na wachapakazi, hivyo anaamini baada ya makubaliano hayo yatakayoondoa vikwazo pia nchi hiyo itakuwa tajiri zaidi.

Korea Kaskazini ilitishia kuachana na mpango wa kiongozi wake, Kim Jong-un kufanya mazungumzo na rais Trump nchini Singapore baada ya kukasirishwa na kauli za Bolton pamoja na mazoezi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini ambayo waliyataja kuwa ni mazoezi ya kujiandaa kufanya uvamizi.

Mwaka 2003, Libya chini ya uongozi wa Muammar Gaddafi ilitangaza kuachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi za kinyuklia, hatua iliyoishtua dunia. Uamuzi huo ulisababisha kuondolewa vikwazo pamoja na kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Marekani pamoja na washirika wake.

Hata hivyo, mwaka 2011, Libya ilivamiwa na waasi walioungwa mkono na Marekani chini ya mwamvuli wa NATO na mwisho wakamuua Gaddafi.

Historia hiyo imemshtua Kim Jong-un ambaye alitangaza kuteketeza vinu na eneo la majaribio la silaha za maangamizi za kinyuklia za nchi hiyo.

Hata hivyo, kuna mkanganyiko wa matakwa ya Marekani na inachofanya Korea Kaskazini, ambayo imesema kuwa katika makubaliano yake na Korea Kusini, walikubaliana kuharibu na kuachana na mpango wa silaha za nyuklia katika eneo lote la Rasi ya Korea, kwa pande mbili.

Nkurunziza Kutawala Burundi Mpaka 2034

Nchi ya Burundi leo inapiga kura ya maoni kufanya marekebisho ya katiba ambayo yanaweza kumuweka Rais wa sasa Pierre Nkurunziza madarakani mpaka mwaka 2034


Kwa mujibu wa BBC Kura hiyo itapigwa ya ndiyo au hapana ili kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani kutoka miaka mitano mpaka saba katika awamu moja.

Katiba ya sasa imeweka ukomo kwa Rais aliyepo madarakani kuhudumu kwa kipindi cha awamu mbili, kwa mujibu wa mabadiriko yatakayofanywa yatampa uhuru Rais Nkurunziza kugombea tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akiwa kama mgombea mpya na hivyo huenda akatawala mpaka mwaka 2034.

Chama tawala CNDD-FDD kinachoongozwa na Nkurunziza ndicho kinaendesha kampeni ya kuunga mkono upigwaji wa kura ya ndiyo huku kiongozi wa upinzani Agaton Rwasa chini ya mwamvuli wa muunganiko wa vyama vya upinzani ujulikanao kama Amizero y’Abarundi wakihamasisha kura ya hapana.

Monday, May 14, 2018

Raia wa Senegal ateuliwa Kuwa Makamu wa Rais Benki ya Dunia

Makhtar Diop, raia wa Senegal ameteuliwa kuwa makamu wa rais wa Benki ya Dunia (WB) atakayekuwa anasimamia miundombinu.

Diop alitangazwa kushika nafasi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo kumfanya kuwa miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa taasisi hiyo muhimu duniani.

Taarifa iliyotolewa na benki hiyo inasema Diop anayaanza majukumu hayo mapya baada ya kuwa Makamu wa Rais anayesimamia Afrika katika miaka sita iliyopita akifanikisha kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya Dola 70 bilioni za Marekani.

Ndani ya miaka hiyo sita, Diop alisimamia miundombinu ya usafiri na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), nishati na madini, fedha na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP).

‘Katika majukumu yake mapya, Diop atasimamia ufadhili wa miundombinu ya fedha katika ufanikishaji wa maendeleo endelevu hivyo kupunguza tofauti iliyopo kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Uteuzi wa Diop anayetajwa kuwa miongoni mwa Waafrika 100 wenye ushawishi zaidi duniani utaanza Julai Mosi.

Alipokuwa akiisimamia Afrika, inaelezwa alisimamia upatikanaji wa fedha za kufanikisha miradi ya aina tofauti akihamasisha zaidi ubunifu na uvumbuzi wa kisayansi.

Alihakikisha Afrika inapata umeme wa uhakika na nafuu huku ikiunganishwa kwa barabara zinazopitika wakati wote.

Ndani ya benki hiyo, Diop ameshahudumu kama mkurugenzi wa fedha, sekta binafsi na miundombinu Amerika Kusini na Visiwa vya Caribbean.

Kati ya mwaka 2009 na 2012 alikuwa mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Brazil ambako alisimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Alishawahi kuwa Mkurugenzi Mkazi katika nchi za Kenya, Eritrea na Somalia.

Saturday, May 12, 2018

Waziri Mkuu Azuiwa Kusafiri

Waziri Mkuu wa zamani Najib Razak na mkewe Rosmah Mansor wamezuiwa kuondoka nchini, Idara ya Uhamiaji imesema Jumamosi.

Taarifa ya Idara ya Uhamiaji ilitolewa muda mfupi baada ya kiongozi huyo wa zamani mwenye kashfa ya ufisadi kuandika katika Facebook kwamba yeye na familia yake wanatarajiwa kwenda ughaibuni kwa mapumziko kuanzia Jumamosi na watarejea wiki ijayo.

Katika akaunti ya Twitter Najib amesema ataheshimu amri ya kuzuiwa iliyotolewa na serikali kumtaka asiondoke nchini.

"Nimetaarifiwa kwamba Idara ya Uhamiaji imenizuia mimi na familia yangu kusafiri nje ya nchi. Naheshimu amri na nitabaki nchini na familia yangu,” ameandika Najib.

Waziri mkuu huyo aliyeondolewa kupitia sanduku la kura sasa anachunguzwa na Serikali juu ya tuhuma za ufisadi wa fedha za uwekezaji ambazo maofisa wanadaiwa kuiba zaidi ya dola za Marekani 4.5bilioni.

Inadaiwa kiasi kingine cha fedha kiliishia kwenye akaunti binafsi ya Najib katika benki.

Najib amekanusha kufanya kosa lolote na anasema fedha hizo zilitolewa na familia ya kifalme ya Saudi Arabia na kwamba alikwisharejesha.

Friday, May 11, 2018

Shirika Linalotetea Watu Wanaotaka Kufa Limetangaza Kifo cha Mwanasansi David Goodal Aliyejiua kwa Sumu

Shirika Linalotetea Watu Wanaotaka Kufa Limetangaza Kifo cha Mwanasansi David Goodal Aliyejiua kwa Sumu
Mwanasayansi David Goodall mwenye miaka 104, aliyesafiri kutoka Australia hadi Uswizi ili kujitoa uhai amefariki May 10, 2018 usiku katika kliniki moja nchini Uswizi, shirika linalotetea haki za watu wanaotaka kufa limetangaza.

Mwanaikolojia huyo ambaye pia alikuwa mtaalamu wa mimea hakuwa anaugua lakini alisema kuwa aliamua kujitoa uhai kutokana na kudhoofika kwa ‘ubora wa maisha yake’.

Uswizi, ni nchi pekee iliyo na vituo vinavyotoa huduma hiyo kwa raia wa mataifa mengine, huduma ambayo inaruhusu watu kujitoa uhai.

Thursday, May 10, 2018

Kenya inatarajia kurusha Satelaiti yake leo

Kenya inajiandaa kutimiza ndoto kubwa ya kisayansi leo Ijumaa. Chombo cha Satelaiti kilichoundwa nchini humo kitarushwa katika anga za juu hii leo kutoka nchini Japan.
Wanasayansi wa anga za juu kutoka Kenya waliokiunda chombo hicho tayari wako katika makao ya Uchunguzi wa Sayansi ya Anga za juu nchini Japan, (JAXA) ambapo chombo hicho kitarushwa kutoka huko.

Nchini Kenya kwenyewe raia wataweza kufuatilia shughuli hiyo moja kwa moja kwenye mtandao wa You Tube, na sherehe maalumu ya kushuhudia imeandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi.

Satelaiti hiyo ndogo ni ya thamani ya dola milioni moja - gharama inayoonekana kuwa ndogo kifedha kwa kiwango cha sayansi ya anga za juu.

Imebandikwa kamera mbili pamoja na vyombo vya kunasa na kupeperusha sauti.

Wahadhiri wa vyuo vikuu wanasema satelaiti hiyo inaweza kutoa huduma tofuati ikiwemo kukusanya taarifa zitakazosaidia katika kilimo na usalama, kutabiri hali ya hewa na hata kukabiliana na majanga.

Kenya kwa sasa inakabiliwa na janga la mafuriko ambalo limesababisha maafa makubwa.

Takriban watu mia mbili wamepoteza maisha yao, huku wengine zaidi ya laki mbili wamepoteza makaazi yao.

Huenda ufanisi katika uzinduzi wa satelaiti hii utaisaidia serikali pakubwa katika kujitayarisha kupambana na majanga ya aina hiyo.

Uzinduzi wa satelaiti hiyo leo unatokana na ushirikiano kati ya Idara ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, afisi ya masuala ya anga za juu ya Umoja wa Mataifa, na Shirika la utafiti wa anga za juu la Japan.

Kenya itaanza kushughulika kuunda satelaiti kubwa na bora zaidi iwapo uzinduzi wa leo utafanikiwa.

Marekani Yalaani Mashambulizi ya Irani Dhidi ya Israel

Marekani  imelaani mashambulizi ya roketi yaliyofanywa na Iran katika eneo linalokaliwa na Israeli –Golan Heights na kuwa halikubaliki na ni hatari kwa maendeleo ya eneo lote la Mashariki ya Kati.

Katika tamko lililotolewa Alhamisi, Ikulu ya Marekani  imesema kuwa walinzi wa jeshi la Mapinduzi la Kiislam la Iran (IRGC) “litawajibika kikamilifu kwa matokeo yoyote ya vitendo vyao vya ovyo” na kuonya kuwa jeshi hilo na “wanamgambo wanaopigana kwa niaba yao” wasiendelee kufanya “vitendo vya uchokozi zaidi.”

Israel imesema Alhamisi ndege zake za kivita zilipiga dazeni ya vituo vya kijeshi vya Iran ndani ya Syria usiku wa Jumatano ikiwa ni hatua ya kujibu mashambulizi hayo.

Jeshi la Israeli limesema kuwa shambulizi hilo la anga lililenga vituo vya kijasusi, maghala ya silaha na vituo vya kupanga vita, na kuwa ndege hizo za kivita pia ziliangamiza mifumo ya ulinzi wa anga ya Syria.

Pia Israel imeonya kuwa “haitoruhusu vitisho vya Iran kujikita katika ardhi ya Syria” na wamesema serikali ya Syria itawajibishwa “kwa kila kitu kinachotokea katika ardhi yake.”

Wednesday, May 9, 2018

Uingereza, Ufaransa, Ujerumani Zasikitishwa Na Maamuzi ya Trump Kujiondoa Mkataba wa Nyuklia wa Iran

Hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani, ya kutangaza kwamba nchi hiyo inajiondoa kwenye mkataba wa kimataifa wa mpango wa kuizuia Iran kutengeneza silaha za nuklia, JCPOA, imepokelewa kwa hisia kinzani na wabunge wa Marekani na viongozi mbalimbali ulimwenguni kote.

Wabunge wengi wa chama cha Demokratik wameikosoa huku Warepublikan wakiisifu kama hatua ifaayo.

Speaker wa bunge, Paul Ryan, ambaye ni Mrepublikan, aliutaja mkataba huo kuwa ulikuwa na hitilafu kubwa.

Lakini kiongozi wa wachache kwenye bunge hilo, Nancy Pelosi alimshutumu Trump na kusema kwamba katika uamuzi wake, rais huyo hakutilia maanani ukweli kwamba mkataba huo ulikuwa unafanya kazi kama ulivyokusudiwa.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kupitia ujumbe wa Twitter aklisema kuwa nchi yake, Ujerumani na Uingereza "zimesikitishwa mno na hatua hiyo ya Trump."

Mapema Jumanne, Macron alisema kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono mikakati ambayo itaimarisha usalama katika eneo hilo.

Katika hotuba iliyosubiriwa na wengi, RaisTrump alitangaza Jumanne kwamba ameamua kuiondoa Marekani kutoka mkataba wa kimataifa juu ya mpango wa kuizuia Iran kutengeneza silaha za nuklia, JCPOA.

Akizungumzia kutoka Ikulu, Trump alisema ataiwekea tena Iran vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyondolewa wakati wa kufikiwa mkataba huo na mataifa mengine matano yenye nguvu duniani pamoja na Iran mwaka 2015.

Washirika wa Ulaya hasa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, wamekuwa wakijaribu kumshawishi kiongozi huyo kutochukua hatua hiyo ambayo wanasema ndio njia pekee ya kusimamia na kufuatilia harakati za nuklia za Iran.

Kabla ya hatua hiyo ya Trump, Iran ilikuwa imeeleza kwamba haingekubali kujadiliana tena juu ya mkataba mwengine na Marekani, na kwamba kwa kujiiondoa, Marekani ingekuwa inakiuka mkataba uliopo na kwamba itaendelea na mipango yake.

Wizara ya fedha ya Marekani ilitoa taarifa Jumanne kuwataka Wamarekani wote walioanza uhusiano na Iran chini na makubaliano hayo, kuanza kusitisha kazi zao.

Israel Yasema Itamuua Rais Assad wa Syria

Mmoja  wa mawaziri walio katika Kamati ya Usalama ya Baraza la Mawaziri Israel amesema wanaweza kuupindua utawala wa Rais, Bashar al Assad na kumuua iwapo Iran itatumia ardhi ya Syria kuishambulia Israel.

Waziri huyo wa Nishati, Yuval Steinitz amenukuliwa na mtandao wa habari wa Israel, Ynet akisema Israel haijajiingiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria hadi sasa.

Lakini alionya iwapo Rais Assad ataendelea kuiruhusu Iran kuendesha shughuli zake katika ardhi ya nchi hiyo Israel itammaliza na kuundoa madarakani utawala wake.

Kadhalika Waziri huyo ameendelea kueleza ikiwa Rais Assad atairuhusu Iran kuigeuza Syria kambi ya kijeshi dhidi ya Israel anapaswa kufahamu huo utakuwa mwisho wake.

Israel na Iran zimekuwa zikishambuliana katika vita maneno kuhusu Syria tangu Februari mwaka huu 

Aprili 9 mwaka huu shambulio la anga liliua askari sita wa kikosi cha makomando cha Revolutionary Guards cha Iran kambini nchini Syria.

Tehran iliilaumu Israel na kuapa kulipa kisasi, kauli iliyojibiwa na Israeli kuwa itafanya mashambuilizi makubwa dhidi ya miliki za Iran nchini Syria.

Pia Waziri Steinitz alionekana kugusia kuwa kauli yake haiakisi sera ya Serikali ya Israeli, akisema: ‘Sizungumzii kuwapo mkakati wowote kumhusu.”

Hakukuwa na mwitikio wa haraka kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu wala Wizara ya Ulinzi Israel kuhusu kauli hiyo nzito.

Iran, wanamgambo wa Lebanon, Hezbollah na Urusi zimekuwa zikiimarisha usaidizi wao kwa Damascus dhidi ya uasi wa miaka saba nchini Syria.

Lakini Israel inahofia uwapo wa maadui wake Iran na Hezbollah utatengeneza jeshi nchini humo litakalotishia usalama wake.

Rais Trump ajitoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran

Rais Donald Trump ametangaza kujitoa katika mkataba wa kimataifa wa Nyuklia wa Iran. Ameuita mpango huo kuwa umeoza na ni kero kwa raia wote wa Marekani.

Amesema mpango huo hauwezi kuleta amani hata kama Iran ikikubaliana na kila kitu kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huo uliosainiwa mwaka 2015 chini ya utawala wa aliyekuwa rais taifa hilo Barack Obama.

Rais wa Iran amekosoa hatua ya Marekani kujitoa na kudai kuwa haiheshimu makubaliano yake. 
Akienda kinyume na mataifa ya Ulaya yaliyofikia makubaliano hayo,Trump amesema kuwa watarejesha vikwazo vya kiuchumi vilivyoondolewa dhidi ya Iran kupitia makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Israel na Saudi Arabia kwa pamoja wamepongeza hatua hiyo.Vikwazo vipya vinatarajiwa kuanza dhidi ya Iran ndani miezi mitatu ijayo.

Trump awali alilalamikia mkataba huo kwamba ulikuwa unaiwekea Iran vikwazo kwa muda tu na kwamba ilishindwa kusitisha mpango wake wa makombora

Friday, March 2, 2018

Wanafunzi 400 wavamia Nyumba ya Mwalimu na Kufanya Vurugu....Shule Yafungwa Wiki 2

Serikali imeifunga Shule ya Sekondari ya Lyamungo iliyoko Hai mkoani Kilimanjaro, baada ya wanafunzi wake kuzusha vurugu kubwa huku wakivamia na kuivunja ofisi ya Makamu Mkuu wa shule hiyo.

Tuesday, July 26, 2016

Koffi Olomide akamatwa DR Congo

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekamatwa akiwa nyumbani kwake mjini Kinshasa.

Mwanamuziki huyo amekamatwa kwa agizo la ofisi ya mwendesha mashtaka.

Olomide alitimuliwa kutoka nchini Kenya baada ya video kuonekana akimpiga teke mnenguaji wa kike katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mapema asubuhi baada yake kuwasili.

Alipangiwa kutumbuiza mashabiki wake Bomas of Kenya siku ya Jumamosi lakini tamasha hiyo ikaahirishwa.

Alikamatwa Ijumaa usiku na maafisa wa polisi wa Kenya na siku iliyofuata asubuhi akaingizwa kwenye ndege na kurejeshwa Kinshasa.

Katika hatua nyingine, waandalizi wa tamasha ambalo Olomide alipangiwa kutumbuiza nchini Zambia pia walitangaza kufuta hafla hiyo kutokana na yaliyotokea Nairobi.

Mwanamuziki huyo, akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumapili, aliomba radhi mashabiki wake na hasa “wanawake na watoto”.

“Najutia sana yaliyotokea… kilikuwa ni kipindi kifupi cha wenda wazimu,” aliambia kituo cha televisheni cha taifa cha RTNC.

Baadaye, aliomba msamaha kutoka kwa raia wote wa DRC ambao huenda alihisi kwamba tabia yake iliwavunjia heshima.

Waziri wa masuala ya vijana na jinsia Kenya, Sicily Kariuki katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya video iliyoonyesha tukio hilo kusambaa, alipendekeza Olomide azuiwe daima kutembelea Kenya.

Friday, July 15, 2016

Picha ya Rais Zuma wa Afrika Kusini akimbusu msichana huyu yawa gumzo

Picha ya msichana akimbusu Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma imezua utata nchini humo.

Picha hizo zilisambaa Jumatano hii baada ya msichana huyo kuziweka kwenye mitandao ya kijamii. “We will check the matter,” alisema msemaji wa serikali Bongani Ngqulunga alipoulizwa kuhusu picha hizo.

Msichana huyo mwenye miaka 19 anaitwa Lindokuhle Dlamini. Kwenye picha hizo aliandika: He is not just a blesser, we are inlove and I am grateful for all that he has done for me, much love. Xo xo.”

Blesser inamaanisha ni mtu mzima anayehonga wasichana na kuwa na uhusiano nao. Akaunti yake ya Facebook imefutwa.

Hata hivyo mtoto wa kiume wa rais huyo, Edward amedai kuwa msichana huyo ni dada yake na kwamba akaunti iliyopost picha hizo ni feki. Baadhi ya magazeti likiwemo Citizen‚ yamesema yaliambiwa na wasomaji wake kuwa ni kweli binti huyo ni mtoto wa Zuma.

Hata hivyo Makamu wa Rais wa Economic Freedom Fighters Floyd Shivambu alikosoa kwa kutweet: Okay cool? What kind of Grand Fathers and Fathers kiss their Grand Daughters & Daughters like this? Perverts??”

Serikali bado haijatoa majibu kama ilivyoahidi.

Thursday, July 14, 2016

Mbunge wa Afrika Mashari Auawa Kikatili Burundi

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi, ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Bujumbura.

Mossi aliyewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika serikali ya nchi hiyo, aliuawa jana katika barabara ya Gihosha eneo la Nyankoni.

Taarifa zilizothibitishwa na Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurikiye zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 4:00 asubuhi. Nkurikiye alisema mbunge huyo alipigwa risasi kifuani kwenye moyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako baadaye alipoteza maisha.

EALA ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambacho wanachama wake ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, ukiwa ni umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa kibiashara huku ukikusudia kuwa na sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.

Mkazi wa eneo alikouawa Mbunge huyo, Achel Majabuka alisema kuwa alisikia mlio wa risasi na baadaye kuona watu wawili wakiondoka katika gari baada ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Bunge la Afrika Mashariki katika taarifa yake iliyotolewa Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa risasi katika eneo la Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.

Alimkariri msemaji huyo wa Polisi akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu na nyumbani kwake, huku Mbunge mwingine wa Burundi katika EALA, Emerence Bucumi akithibitisha kifo hicho.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega alilaani mauaji hayo na kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi aliyekuwa amejikita kusimamia na kutetea utengamano wa ukanda huo.

Spika huyo ambaye yuko Uganda kwa ziara ya kikazi, ameishauri Serikali ya Burundi kuwatia nguvuni mara moja wauaji wa Mossi ambaye pia aliwahi kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

“Ninatoa salamu za rambirambi kwa serikali, familia, marafiki na wananchi wa Burundi. Ninawaomba wawe watulivu katika wakati huu mgumu na ninaamini mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka kuhakikisha waliohusika na tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,” alisema Spika Kidega.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alikielezea kifo cha mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa kwa serikali yake. Naye Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada na kuwa jumuiya imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.

Mwaka jana, Mossi alitembelea wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na kulia, ameuawa wakati mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yakiwa yanaendelea kufanyika jijini Arusha.

Alikuwa na Shahada ya Uandishi wa Habari na aliwahi kufanya kazi katika BBC na alikuwa Waziri wa Burundi wa Masuala ya Afrika Mashariki hadi Juni 2012 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.

Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano, Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005 hadi 2007.

Burundi, taifa katika Afrika Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.

Mgogoro huo wenye kuendana na umwagaji damu, umesababisha watu 1,500 kuuawa, huku ukiwahusisha wafuasi wa Rais Nkurunziza na wale wanaopinga ushindi wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa mara ya tatu, wakidai kuwa ulikiuka Katiba ya nchi hiyo.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU