test
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts

Monday, May 28, 2018

Mwanafunzi Chuo cha SAUT Ajinyonga Baada ya Timu Yake ya Liverpol Kufungwa

Mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo kikuu cha ‘St. Augustine’ kampasi ya Mbeya Moses Mashaka amejinyonga mara baadaya timu yake ya Liverpol kushindwa kutwaa ubingwa wa klabu bingwa barani ulaya.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Jijini Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi Mussa Taib amesema Moses (24) amejinyonga mara baadaya ‘kubet’ na timu yake kushindwa kutwaa ubingwa.

“Mwanafunzi wa chuo kikuu cha sauti mwaka wa pili anachukua shahada ya ualimu amefariki baada ya ‘kubet’ pesa ambazo hazijulikani ni kiasi gani na baadaya Liverpol kushindwa ndipo akachukua uamuzi huo”,amesema kamanda Taibu.

Aidha Kamanda Taibu amewataka wanafunzi kuacha kutumia fedha za wazazi kwa mambo yasiyohusiana na masuala mazima ya elimu, kwani matokeo yake ni hasara kwa wazazi.

Sunday, May 27, 2018

Mtanzania Aibuka Kidedea Mashindano Ya Kuhifadhi Quran Afrika.....Waziri Mkuu amtaka Sheikh Kishki akaonane na Waziri wa Ardhi atoe maamuzi ya kiwanja

KIJANA wa Kitanzania, Shujaa Suleiman Shujaa ameibuka kidedea na kitita cha sh. milioni 15 katika mashindano ya 19 ya Afrika ya kuhifadhi Quran kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.

Shujaa mwenye miaka 23 ambaye ni mkazi wa Morogoro, amejishindia pia laptop, kiwanja chenye hati eneo la Kigamboni kilichotolewa na kampuni ya Property International ya jijini Dar es Salaam pamoja na dola za Marekani 500 kutoka kwa Bw. Ahmed Seif “Magari” aliyetoa dola 500 kwa washindi wote watano.

Akizungumza na maelfu ya waumini na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana  mchana (Jumapili, Mei 27, 2018), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuilinda amani iliyopo nchini kwani ikipotea hakuna atakayeweza kufanya ibada.

“Mtakubaliana nami kuwa amani ya nchi yetu, ndiyo inatufanya tutembee vifua mbele dhidi ya wenzetu, ni neema kubwa ambayo kila muumini anapaswa kuilinda kwani ikipotea hata mkusanyiko wetu huu wa leo si rahisi kufanyika mahali kama hapa,” alisema.

“Leo hii tuko hapa uwanjani kwa sababu tuna amani, kama Serikali isingekuwa inashirikisha Watanzania wote kulinda amani, basi tusingeweza kukutanika hapa. Kuna nchi 18 ziko hapa, na watu wake wamekuja hapa uwanjani kwa kuwa wana uhakika na amani tuliyonayo sisi Watanzania,” alisema.

Alisema katika nchi ambazo amani imetoweka, watu wanalazimika kufanya shughuli za ibada majumbani au kwa kujificha. 
“Wenzetu hao, hawapati fursa adhimu kama hii ya kujumuika pamoja na majirani, ndugu, jamaa na marafiki kusikiliza na kufurahia kisomo cha Quran au kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,” aliongeza.

Aliwataka Watanzania waendelee kubeza na kupuuza kauli za walio wachache ambao kwao kuzungumzia amani ni kujipendekeza kwa Serikali. “Watu hao wamesahau kwamba tofauti katika Uislamu hazikuanza leo, lakini tofauti hizo hazikuwa sababu ya wema waliotangulia kuacha kuheshimiana na kushirikiana,” alisisitiza.

Mshindi wa pili kwenye kundi hilo la juzuu 30 ni Ahmed Noor wa Sudan ambaye ameshinda sh. 12,564,750 pamoja na laptop akifuatiwa na Muzamil Awadh Mohamed wa Sudan alijishindia sh. milion 7.5 pamoja na laptop zilizotolewa na kampuni ya Camara Education.

Mshindi wa nne ni Abdulally A. Mohammed wa Kenya aliyepata zawadi ya sh. 5,711,000 na wa tano ni Ibrahim Maazur kutoka Niger, aliyepata sh. 3,426,000. Washindi hao wote watano walipewa zawadi ya kwenda hijja na Waziri wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ally Sheikh.

Washiriki wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji Djibouti, Kenya, Ethiopia, Congo DRC, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

Washiriki wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu (washindi watatu), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na Juzuu 20 (washindi watatu).

Viongozi wengine waliohudhuria mashindano hayo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kutoka Saudi Arabia, Comoro, Oman, Uturuki, Kenya, Msumbiji na Nigeria, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Sheikh Nurdin Mohammed Ahmad (maarufu kama Sheikh Kishki) akaonane na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi ili atoe maamuzi ya kiwanja chao kilichopo eneo la Matumbi ambacho mwaka jana aliagiza kifuatiliwe taratibu zake na kisha wapatiwe.

“Kuhusiana na suala la kiwanja mlichosema, mamlaka ya awali ni Manispaa ya Temeke na ilishakamilisha taratibu zote za kisheria, ikapeleka kwa Afisa Ardhi wa Mkoa kuona kama limepita kwenye vikao vyote ndipo wanaenda wizarani kupata kibali. Hakuna sababu ya wizara kuikatalia manispaa huku eneo lenyewe likiwa kwenye ramani kuu ya manispaa yenyewe, nenda mumuone Waziri mwenye dhamana, awape ardhi,” alisema.

Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kupewa taarifa akiwa jukwaani kwamba taasisi ya Al-Hikma iliwasiliana na Manispaa ya Temeke, hadi mkoani wakapewa barua zinaonyesha eneo liko sawa lakini walipofika wizarani wamekwamishwa na Afisa mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Mama Mpetula.

Juni 11, mwaka jana katika mashindanio ya 18, taasisi ya Al-Hikma waliomba wapatiwe kiwanja na.118 kwenye kitalu E kilichoshikamana na kiwanja na. 117 chenye shule yao ya Al-Hikma Girls iliyoko Temeke ili waweze kujenga zahanati.

Thursday, May 24, 2018

Mwanamke Amuua Mumewe kwa Kisu...Ni Baada ya Kugoma Kumpikia Chakula Kisha Ugomvi Ukaibuka

Sophia  Salehe, mkazi wa Kata ya Namiongo, Newala mkoani Mtwara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kumuua mume wake kwa kumchoma kwa kisu.

Mauaji hayo yalitokana na ugomvi baina ya mtuhumiwa ambaye inadaiwa kuwa alikataa wito wa mumewe kupika chakula baada ya kutokushiba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya, amesema tukio hilo lilitokea juzi mkoani humo.

Kwa mujibu wa Mkondya, mwanamume huyo alikufa papo hapo baada ya kuchomwa kisu na mke wake.

Alisema siku ya tukio majira ya saa 1:30 usiku, mwanamke huyo alimwandalia mume wake chakula na kumpatia.

“Kile chakula kilikuwa kidogo, mume wake, Ahmed Salim, alimtaka arudi jikoni kwa ajili ya kupika tena chakula kwa kuwa hakikumtosha. Hapo ndipo palitokea ugomvi wakalumbana na wakaendelea kugombana na mkewe akachukua kisu na kumchoma kifuani,” alisema Kamanda Mkondya.

Kamanda Mkondya alisema Salim alifariki dunia papo hapo baada ya kutokwa na damu nyingi kwenye jeraha.

Aidha, alisema katika tukio hilo wanamshikilia na mwanaume mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Alisema wanamshikilia kijana huyo kwa kuwa katika tukio hilo alikuwapo, hivyo watakapopata maelezo yatakayojiridhisha kutohusika ataachiwa.

“Bado huyu kijana tunamhoji ni kwa nini hakutoa msaada wa kuamua ugomvi huo. Hapa tunataka kujua na yeye amehusika au la na kwa huyu mwanamke taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema.

Aidha, Kamanda alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi.

Wednesday, May 23, 2018

Kiwanda Cha Nyama Chapigwa Faini Ya Milion 5 Dodoma Kwa Kushindwa Kukidhi Vigezo Vya Usafi Wa Mazingira


Labels
Kiwanda cha nyama cha Tanzania (TMC) kimepigwa faini ya Milion 5 baada ya kukiuka kanuni za uhifadhi wa mazingira na kuchelewa kutekeleza agizo walilopewa kuhakikisha wanafanyiakazi maagizo waliyopewa juu ya kufanyiakazi kanuni za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufanya tathmini mazingira kabla ya kuanza kazi.

Akizungumza wakati akikagua machinjio hayo na kiwanda hicho cha nyama Naibu waziri wa nchi Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola  Ameelezea kutoridhishwa na hali ya mazingira kiwandani hapo.

Akitoa tamko hilo ,Naibu waziri Lugola alisema kuwa kulingana na sheria za usimamizi na usafi wa mazingira ni sharti kiwanda hicho kitozwe faini ili iwe fundisho kwa viwanda vingine kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mazingira kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji.

Pamoja na mambo mengine  Lugola alikiagiza kiwanda hicho kuelekeza taka ngumu kwenye dampo la jiji lililopo Chidaya -Ntyuka ili kuepuka madampo yasiyo rasmi yanayozagaa katikati ya jiji na kukuta mizoga ya nyama ikiwa imezagaa maeneo mbali mbali.

Awali akisoma taarifa kwa naibu waziri Lugola,Mtendaji  Mkuu wa kiwanda hicho Aron Luziga alizungumzia changamoto zilizopo  kiwandani hapo kuwa ni pamoja na mfumo wa maji taka usio rasmi kutokana na gharama kubwa ya ujenzi pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika hali inayokwamisha shughuli za uzalishaji .

Alisema,hali ya kukatika katika kwa umeme kiwandani hapo inakwamisha shughuli za uzalishaji hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya umeme ili kukidhi mahitaji .

"Lengo la kiwanda hiki ni kuwa kinara katika uzalishaji wa nyama na kusafirisha nchi nyingi zaidi duniani hii ikiwa ni pamoja na uchakataji wenye kiwango kuendana na soko La kimataifa," alisema Luziga.

Wakati huo huo  Naibu waziri  Kangi Lugola  ameliagiza Baraza la usimamizi wa mazingira la Taifa (NEMC) kushirikiana na uongozi wa jiji la Dodoma kukagua kwa undani mifumo ya maji taka ya kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Sunshine kilichopo katika kijiji cha Zuzu.

Hatua hiyo imekuja kutokana na kushindwa kuibaini mifumo ya majitaka kiwandani hapo kutokana na kuwa kiwanda kimesitisha uzalishaji kutokana uhaba wa malighafi kiwandani hapo.

Kutokana na hayo Naibu waziri Lugola emeutaka uongozi wa kiwanda hicho kuingia mkataba na wakulima ili waweze kupata malighafi ambazo zitawezesha kiwanda hicho  kuwa na uzalishaji wakati wote.

"Ni kweli tunahitaji Tanzania ya viwanda,lakini viwanda hivyo  vije kwa kuzingatia sheria za mazingira ili kuyahifadhi na kwa manufaa ya vizazi vijavyo," alisema.

Hata hivyo alisema viwanda vinapaswa kuchochea wananchi kuondokana na umaskini hivyo ni wajibu kushirikiana na wananchi bega kwa bega kupata solo la uhakika.

Mashine Ya CT-Scan Muhimbili Yaharibika

Hospitali  ya Taifa Muhimbili (MNH), imekiri kuharibika kwa moja ya mashine zake za CT-Scan hali inayolazimu wagonjwa kupimwa kwa kutumia mashine moja ambayo ni mpya.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alithibitisha kuharibika kwa mashine hiyo jana.

“Ni kweli mashine yetu moja ya CT Scan, ile ambayo ilikuwa inatumika kwa muda mrefu hapa hospitalini imeharibika si chini ya miezi mitatu sasa,” alisema.

Eligaesha alisema hivi sasa madaktari wanalazimika kuwafanyia uchunguzi wagonjwa katika mashine mpya iliyonunuliwa na Serikali miaka miwili iliyopita.

“Hii mpya haina tatizo lolote, MOI (Taasisi ya Mifupa Muhimbili), wanatarajia kufunga CT-Scan mpya, tutakuwa tunashirikiana nao kuwachunguza wagonjwa,” alisema.

Alipoulizwa iwapo pamoja na ushirikiano huo, Muhimbili itanunua mashine mpya nyingine ya CT-Scan, alisema hawana mpango huo kwa sasa.

“Mashine hizi ni gharama kubwa mno, ni kati ya Sh. bilioni mbili hadi tatu hivi, kwa kuwa MOI watafunga, tutaendelea kushirikiana nao pamoja na yetu kusaidia wagonjwa,” alisema.

Zanzibar Yaagiza Walimu 300 Wa Sayansi kutoka Nigeria

Serikali ya Zanzibar imeagiza zaidi ya waalimu 300 wa masomo ya Sayansi kutoka nchini Nigeria ambao tayari wameanza kuwasili visiwani humo.

Kwa mujibu wa serikali ya Zanzibar, waalimu hao wanaoingia kwa awamu, na wanatarajiwa kuziba pengo la uhitaji wa zaidi ya waalimu 300 wa masomo hayo.

Naibu waziri wa Elimu Zanzibar Mmanga Mjengo amesema ujio huo utasaidia kuamsha pia morali ya waalimu wengine wa masomo ya sayansi visiwani humo.

Ameongeza pia wameamua kwenda Nchini Nigeria kwa sababu kuna wingi wa waalimu na wenye ubora na haikuwa rahisi kuchukua kutoka nchi za karibu kwa sababu na wao pia wana tatizo la uhaba wa waalimu.

''Mchakato wa upatikanaji wa waalimu hawa hufanywa kwa kutegemea uwezo wao katika ufundishaji na pia ubora wa kazi zao.'' alisema waziri Mjengo.

Serikali ya Zanzibar imesisitiza kuwa sio mara ya kwanza kwa ujio kama huu kwani katika miaka ya nyuma waalimu hawa wamekua wakija kwa kujitolea.

Ujio wa waalimu hawa ambao watakuwepo kwa kipindi cha miaka miwili unatajwa kupunguza uhitaji wa zaidi ya waalimu 300 visiwani humo.

Rais wa TLS, Fatma Karume akutana na kufanya majadiliano na IGP Sirro

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amemtembelea mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ofisini kwake akieleza wamejadiliana mambo manne yanayohusu masuala ya sheria na haki.

Wakati Fatma akieleza hayo jana, msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema: “Alikuja kujitambulisha kuwa yeye ni rais wa TLS. Ilikuwa ziara ya kawaida na binafsi, hapa tunapokea wageni wa kila aina.” 
Fatma ameyataja mambo waliyojadiliana kwakina na IGP Sirro kuwa ni wanasheria kutobughudhiwa wanapokuwa kwenye vituo vya polisi, hali ya usafi na usalama wa mahabusu wawapo rumande, haki ya maandamano na uhuru wa polisi kufanya uamuzi bila kushinikizwa na wanasiasa.

Fatma ambaye ni wakili wa kujitegemea alichaguliwa kuongoza TLS Aprili 14, akichukua mikoba ya Tundu Lissu aliyemaliza muda wake wa uongozi.

Alisema wanasheria wamekuwa hawatendewi haki wanapokuwa katika vituo vya polisi kutetea wateja wao.

Fatma alisema ni haki ya kila raia kuwa na mwanasheria anapopata tatizo la kisheria na ni haki ya wanasheria kutimiza majukumu yao bila kuingiliwa.

Pia, alisema walijadiliana kuhusu usafi wa mahabusu na kutojaza watuhumiwa kwenye vyumba vidogo.

Alisema alizungumzia haki ya wananchi kuandamana na umuhimu wa kufanya hivyo.

Kuhusu uhuru wa polisi kufanya kazi bila kuingiliwa alisema: “Natambua kuwa sheria ya mfumo mzima wa Jeshi la Polisi haijakaa sawa, ingekuwa amri yangu ingebadilishwa ili kuwe na usawa katika utendaji na wao wafanye kazi zao bila kuingiliwa na wanasiasa.”

“Nchi zilizoendelea wakuu wa polisi wanateuliwa na kamati, lakini sheria za nchini wanateuliwa na Rais, jambo ambalo linawawia vigumu kufanya kazi kwa kujitegemea,” alisema Fatma.

Alisema anatambua hilo lipo nje ya uwezo wa Polisi, hivyo kitu pekee wanachopaswa kufanya ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Fatma alisema IGP Sirro aliwaomba kuelimisha wananchi kuhusu sheria, kutambua haki zao na wajibu wao katika kuzitekeleza.

“Nimelichukua hili, tutatafuta majukwaa kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii kuhusu sheria, namna ya kuzitekeleza na wajibu wao,” alisema Fatma.

Maofisa Watatu Kituo cha Uwekezaji cha nchini ( TIC ) Wafariki kwa Ajali

Maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji cha nchini  (Tanzania Investment Center (TIC) wamefariki dunia katika  ajali ya gari usiku wa kuamkia jana Mei 22, 2018 maeneo ya Chalinze wakiwa njiani kuelekea jijini Dodoma.

Waliofariki ni Saidi Amiri Moshi (Kaimu Mkurugenzi wa Research zamani Corporate Affairs), Zacharia Kingu (Kaimu Mkurugenzi wa Corporate Affairs zamani Investment Promotion) na Martin Masalu (Meneja Research).

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jonathan Shana amesema ajali hiyo imehusisha gari ya serikali STK 5923 aina ya Toyota land cruiser lililongana na Scania T620 AQV ambaye dereva wake alihama kwenye njia yake na kusababisha ajali hiyo.

Waliopata majeraha ni wawili Godfrey Kilolo (Meneja wa Sheria) na dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina moja tu la Priscus.

Kamanda wa Polisi aliyewaonya wanaume kukohoa azungumzia kuhamishwa kwake ghafla baada ya kauli hiyo

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi Visiwani Zanzibar, Hassan Nassir Ali, amefunguka juu ya uhamisho wake aliopewa siku chache baada ya kuwaonya wanaume juu ya tabia zao zisizofaa kwenye jamii.

Kamanda Hassan amesema kwamba uhamisho wake ni wa kawaida na wala haujatokana na kauli alizotoa, ambazo zilizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

Akiendelea kutolea ufafanuzi suala hilo Kamanda Hassan amesema kwamba kauli hiyo aliitoa na alikuwa anamaanisha, lakini haijaleta mtafaruku wowote kwenye jamii kama ambavyo inasemekana, na hata walipoijadili kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar ilikuwa ni utani.

“IGP amesema mwenyewe amefanya uhamisho na uteuzi huu ili kuimarisha safu yake kiutendaji, mimi ningekuwa nimesema nimewakwaza watu sio kweli, hata wale waliosema katika Baraza la Uwakilishi ilikuwa ni kwa utani, ni uhamisho wa kawaida kabisa, wala sio chuki”, amesema Kamanda Hassan.

Kamanda Hassan ameendelea kwa kuwataka wananchi wa Kaskazini Pemba ambako amehamishiwa kufuata sheria bila shuruti kwani kazi iko pale pale.

“Nitaendelea kufanya kazi yangu vizuri nitaendelea kusimamia sheria vizuri, kazi iko pale pale bado mimi ni Kamanda wa polisi nitasimamia sheria za nchi, wala sio jambo langu hili wala mie sio mzee wa vikohozi, mimi nimetoa mifano, hivyo kazi iko pale pale”, amesema Kamanda Hassan.

Kamanda huyo ambaye metokea visiwani Zanzibar wiki iliyopita aliibua mzozo kwenye mitandao baada ya kuwaonya wanaume wenye tabia ya kukohoa pindi waonapo wanawake wenye maumbile makubwa, akisema hilo ni kosa kisheria ambalo linatambulika kama shambulio la aibu.

Monday, May 21, 2018

Watakaohujumu Miundombinu Tanesco Kukiona

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuilinda na kuitunza miundombinu ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), huku akiagiza mamlaka husika kuwashughulikia watakaojihusisha na uharibifu wa miundombinu hiyo.

Majaliwa ameyasema hayo jana Mei 21, alipokuwa akizindua uunganishaji wa gridi ya taifa kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara iliyofanyika katika Kituo cha kupozea umeme cha Maumbika mkoani hapa.

“Wapo baadhi ya watu wasio na nia njema na serikali wanaharibu miundombinu kwa kung’oa vyuma na kuuza kama vyuma chakavu, hawa ni wahujumu uchumi.

“Naagiza mamlaka zinazohusika kufanya ukaguzi kila eneo linalouza au kununua chuma chakavu kubaini kama kuna miundombinu ya Tanesco na endapo mtaikuta wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria,” alisema Majaliwa.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Majaliwa amesema kuwa mkakati uliopo sasa ni kuboresha miundombinu ya zamani na kujenga miradi mipya ya umeme ili kuzalisha umeme wa kutosha ili kuwafikia wananchi wengi.

Friday, May 18, 2018

Sethi Agoma Kuvuliwa Madaraka IPTL

Siku chache baada ya kuondolewa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, mfanyabiashara Herbinder Sethi ameeleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo, huku akisema hautambui uongozi mpya uliowekwa madarakani.

Uamuzi wa kumwondoa Sethi katika bodi ya wakurugenzi ambayo pia ilimvua uenyekiti wa IPTL, ulifikiwa baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi kwa miezi sita mfululizo bila ruhusa, tangu Juni 19, 2017 alipokamatwa na kushtakiwa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimsomea Sethi mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 22.198 milioni za Marekani (Sh309.5 bilioni).

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa wakili wake, Hajra Mungula iliyotolewa jana kupitia mitandao ya jamii ilisema Sethi hatambui mabadiliko ya uongozi uliowekwa na kwamba yeye ni mmiliki halali wa IPTL ambayo kimsingi inamilikiwa na kampuni anayoimiliki ya Pan African Power Solutions (PAP).

“Pamoja na kuagiza wanasheria wake kuchukua hatua za haraka za kisheria, Mwenyekiti Sethi pia hana taarifa zozote juu ya mabadiliko hivyo anapenda kuutaarifu umma wazipuuze taarifa hizo kwa kuwa hazitokani na mamlaka halali ya kisheria ya kampuni hiyo,” ilisema taarifa ya Mungula

Mungula alisema mabadiliko hayo yamekwenda kinyume na notisi ya katazo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali la Februari 12, 2018 lenye kumbukumbu Na. AGS234 lililozuia aina yoyote ya uhamishaji wa mali na umiliki wa mali za IPTL.

“Kimsingi mabadiliko hayo batili yanaathiri na kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali.

“Pamoja na kwamba Mwenyekiti bado yuko mahabusu akituhumiwa kwa mashtaka kadhaa ya jinai, hiyo haiondoi ukweli kuwa IPTL ni kampuni binafsi yenye wamiliki halali wenye hisa halali, hivyo haiwezekani kwa mtu asiyehusika na asiye mwanahisa kutangaza mabadiliko ya uongozi bila kufuata taratibu zilizopo kisheria,” alisema Mungula.

Alisisitiza kwamba licha ya Sethi kuwa na mashtaka ya jinai yanayomkabili, lakini Watanzania wajue bado kampuni hiyo iko chini ya usimamizi salama wa PAP na kwamba madeni yote, madai ya mali na stahiki zote zinazohusiana na kampuni hiyo zipo katika mikono salama.

IGP Sirro afanya mabadiliko Polisi

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI) Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.

Kabla ya uteuzi huo, Makabila alikuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu ya Polisi Dar es Salaam.


Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Mei 17, 2018 na msemaji wa polisi, Barnabas Mwakalukwa imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo aliyekuwa DCI Zanzibar, Ramadhan Ng’anzi ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Charles Mkumbo aliyehamishiwa makao makuu ya upelelezi, Dar es Salaam.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali anakwenda kuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa makao makuu ya upelelezi Dar es Salaam.

“Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja, Makarani Khamisi amehamishiwa makao makuu ya upelelezi Zanzibar na nafasi yake kuchukuliwa na kamishna msaidizi wa polisi, Suleiman Hassan aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kaskazini Unguja,” anasema Mwakalukwa katika taarifa hiyo.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq anakuwa ofisa mnadhimu makao makuu ya polisi Zanzibar na nafasi yake inachukuliwa na kamishna msaidizi, Haji Abdallah Haji aliyekuwa ofisa mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.

Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.


Chanzo- Mwananchi

TPSF Yataja Sababu za Wafanyabiashara Kufunga Biashara Zao

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye amesema kinachochangia kufa na kufungwa  kwa biashara nchini kunatokana na  mazingira magumu ya biashara pamoja na sera kandamizi zilizopo.

Amesema utafiti uliofanywa na TPSF umebaini kuwa biashara 4,640 zimefungwa nchini kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na vikwazo mbalimbali, huku akibainisha kuwa mfuko huo kwa sasa upo  tayari kusaidia maeneo mbalimbali ya ujasiliamali pamoja na kutoa elimu.

Simbeye ametoa kauli hiyo jana Mei 17, 2018 katika kongamano la kambi ya ujasiriamali iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Alisema  Tanzania inatakiwa kupiga hatua zaidi katika suala ujasiriamali kwa sababu  ni sekta pekee inayozalisha ajira kwa wingi nchini, hivyo ni vyema ikatumika kitaaluma katika kuwaandaa wanafunzi kufùndishwa kwa vitendo  wanapokuwa vyuoni.

“Sekta binafsi ni mwajiri pekee wa kudumu katika maisha ya mtu ama watu hivyo vijana wetu wanatakiwa kuwa wathubutu na kuondokana na uwoga kwani ni tatizo kubwa kwa vijana wetu,”amlisema Simbeye.

Thursday, May 17, 2018

Watumishi Wa Afya Nchini Wanatakiwa Kuchunguza Watoto Saratani Ya Macho Kila Wanapohudhuria Kliniki

WATUMISHI wa Afya wa ngazi ya Jamii,Zahanati , Vituo vya afya vya na Hospitali za Kliniki za Mama na Mtoto za Wilaya zinatakiwa kuchunguza Uakisi wa mwanga kwenye mboni za watoto kila wanapoenda kucheki ukuaji wa watoto hao ili kupunguza uwepo wa saratani ya macho kwa watoto.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mohammed Bakari Kambi wakati akitoa tamko la saratani ya macho kwa watoto kwa niaba ya Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es salaam.

“Iwapo mtoa huduma za afya unahisi kuwa mtoto ana tatizo kwenye jicho usimrudishe nyumbani hadi uhakikishe mtoto huyo ameonwa na mtaalamu wa macho ili kugundua kama ana tatizo kwenye macho yake” alisema Prof. Kambi.

Aidha Prof. Kambi amesema kuwa katika kuboresha huduma hizo Wizara imeandaa mwongozo ambao utasaidia kuinua uelewa wa wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua watoto wenye tatizo hilo na kuwapa rufaa mapema.

Kwa Mujibu wa Prof. Kambi amesema kuwa takwimu za hapa nchini zinaonesha kuwa watoto137 wenye saratani hii walionwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa mwaka 2017 na watoto 80 hadi 100 hupewa rufaa na kufika kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wengine hutibiwa KCMC Moshi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi  wa mpango wa Macho wizara ya Afya Dkt. Benadertha Shilio amesema kuwa anawashukuru wadau wote wa macho ambao wamekuwa bega kwa began a Serikali ya Tanzania katika kufanikisha kuboresha huduma za Macho kwa watoto.

“Tunawashukuru Rotary Club ya Dar es salaam Oysterbay wakishirikiana na Rotary Club ya Chelsea nchini Uingereza ambao wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kutibu Saratani ya macho vinavyogharimu kiasi cha Dola za Kimarekani 65,000 na Kampuni ya Pricewaterhouse ya Tanzania ambayo imetoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 25 ambavyo vimesambazwa Muhimbili na Mloganzila” alisema Dkt. Shilio.

Maadhimisho ya Wiki ya sarani ya Macho kwa watoto kwa mawaka 2018 imebeba kauli mbiu isemayo “MBONI NYEUPE KWENYE JICHO LA MTOTO INAWEZA KUWA SARATANI YA MACHO”.

Halmashauri Zatakiwa Kutumia Fedha za Mgawo wa Ada ya Wanyamapori Kutoa Ulinzi kwa Wananchi

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali  imezitaka Halmashauri za Wilaya Nchini zinazopata mgawo wa mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.

Hayo yameelezwa jana Bungeni, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Leah Jeremiah Komanya juu ya lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake.

“Takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu  vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali,” alisema Mhe. Hasunga.

Aidha amesema, Wizara imekuwa ikitoa mgawo wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya wilaya husika.

Hata hivyo amesema, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukalisha mfumo wa kielektroniki  ujulikanao kama “MNRT Portal” ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo .

Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 01 Julai, 2018 ambapo nakala ngumu za taarifa zitakuwa zikitumwa kwenda wilaya husika.

Wakati huo huo Mhe. Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Salum Msabaha juu ya mkakati wa Serikali katika kuboresha vivutio vya utalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi na kukuza pato la Taifa, amesema Wizara imeandaa mkakati wa kuvitambua na kuvitangaza vivutio vyote nchini ukiwemo mji wa Bagamoyo.

Amesema mpango unalenga kushirikisha mashirika yaliyo chini ya Wizara yaani Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAMWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Ameendelea kusema,  vituo vya malikale vilivyopo Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo yatakayoendelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika hayo. Aidha, vivutio vyote vya utalii nchini vitaendelea kutangazwa kupitia Taasisi zinazohusika ikiwemo Bodi ya utalii Tanzania (TTB).

Ametaja kazi zitakazotekelezwa na mashirika hayo kuwa ni kuweka huduma muhimu kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususani majengo na barabara ili kuwezesha kufikika kwa urahisi na kuwa na muonekano unaovutia , kujenga vituo vya kumbukumbu na taarifa pale ambapo vinahitajika, kuboresha vioneshwa na kuvitangaza , kuhamasisha wawekezaji wa hoteli, michezo na vivutio vingine vya watalii.

Hata hivyo, Wizara ya MaliAsili na Utalii itaendelea kusimamia majukumu yote ya uhifadhi, utafiti na kuandaa taarifazitakazosaidia kuboresha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kwa kutoa elimu kwa Umma juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale na maliasili za nchi yetu.

Watanzania Watakiwa Kutumia Takwimu Zinazotokana na Sensa Mbalimbali Kujiletea Maendeleo

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Luhaga Mpina amewataka Watanzania  kutumia takwimu za sensa mbalimbali  zinazotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kuongeza tija na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Mhe. Mpina ametoa wito huo jana Jijini Dodoma, alipokuwa akizindua matokeo ya utafiti wa Kilimo wa mwaka 2016/2017 ukiwa ni utafiti wa pili kufanyika nchini ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2014/2015.

“Tunapenda kufanya sensa lakini mwisho wa siku hakuna anayetumia sensa hiyo. Huwezi kufanya mapinduzi ya kiuchumi bila ya kutumia matokeo mbalimbali ya tafiti,” alisema Mhe. Mpina.

Aliendelea kusema, matokeo ya tafiti hizo yametumika katika kupima mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.10 wakati mwaka 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.1. Aidha mchango wa shughuli za kilimo kwa mwaka 2014 ulikuwa asilimia 28.8 wakati mwaka 2017 ulikuwa asilimia 30.1.

Vile vile amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa zao la mahindi mwaka 2016/2017 uzalishaji wake ulikuwa tani 5,766,984 na kwa takwimu za utawala za mwaka 2017/2018uzalishaji ni tani 6,681,000. Katika mwaka 2017 ongezeko la thamani ya shughuli za kilimo cha mazao iliongezeka na kufikia shilingi trilioni 5.3 kutoka shilingi trilioni 5.1 mwaka 2016.

Mhe. Mpina amesema, kwa upande wa Tanzania Baramkoa wa Mbeya umeendelea kuongoza katika uzalishaji wa zao la mahindi kwa tani 578,280 (10%) wakati Mkoa wa Morogoro umeongoza.

Aidha kwa upande wa mifugo, Tanzania Bara inaidadi ya ng’ombe 30,496,687, mbuzi 18,947,657, kondoo 5,565,468 na kuku wa asili 38,595,106 ambapo mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe ni pamoja na Tabora (8.7%), Mwanza (7.9%) na Manyara (7.2%). 
Tanzania Zanzibar ina idadi ya ng’ombe wapatao 175,314, mbuzi 107,993, kondoo 517 na kuku wa asili 1,754,786 na mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe kwa Tanzania Zanzibar ni Kaskazini Pemba (30.3%) ikifuatiwa na Kusini Pemba (19.9%).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amewaomba watumiaji wa takwimu hizo kuzitumia kwa manufaa ya kufuatilia na kutathimini mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na si vinginevyo.

Hata hivyo amesema, Tanzania bado ni nchi ya pili katika Bara la Afrika kwa kuwa na mifugo mingi hivyo ni dhahiri kuwa uwezo wa viwanda vya nyama hapa nchini  na kuuza nyama na bidhaa zake zinazozalishwa kwa lengo la kujipatia fedha za kigeni.

Mwakyembe, Afukua Utajiri wa Marehemu Kanumba

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe

SIFA anazomwagiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe mitaani, zinatosha kusema kuwa waziri huyo ni noma katika uchapakazi wake.

Dawati la Ijumaa ambalo kila siku halipoi kusaka habari ziliokwenda shule limebaini kuwa Dk Mwakyembe amekuwa kiongozi anayetajwa na wananchi wengi hasa wasanii kuwa anamudu kuingoza wizara iliyo chini yake.

Ukaribu wake na wasanii wa muziki wa ladha tofauti, ufuatiliaji wa masuala ya michezo ukiwemo mpira wa miguu, ngumi, riadha na usimamiaji wa haki za wasanii kwa jumla ni miongoni mwa mambo yanayompandisha chati waziri huyo.

 HABARI ILIYOBAMBA

Hivi karibuni, Dk Mwakyembe, akiwa bungeni jijini Dodoma, aliliamsha dude kwa kuahidi kufuatilia kwa kina mikataba yote isiyokuwa na tija kwa wasanii ambayo hatimaye huyaacha maisha yao kwenye ufukara.

Ahadi ya ufuatiliaji huo wa mikataba feki ilichochewa na waziri huyo kuguswa na hali ya ugonjwa na changamoto za kimatibabu zinazomkabili mwigizaji mkongwe nchini, Amri Athuman ‘Mzee Mjuto’ ambaye kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu.



“Leo hii Mzee Majuto anaumwa, anaomba pesa, ninachanga pesa kutoka mfukoni kwangu, lakini leo hii nusu ya mabango ya biashara, matangazo ya biashara kwenye TV ni Majuto, ninaomba sasa nitumie nafasi hii kusema nimeunda kamati ya wanasheria, tunaanza na kesi ya Majuto. Mashirika yote, kampuni zote zilizoingia mkataba na Majuto, tutapitia hiyo mikataba, kama ameonewa lazima ilipwe familia yake…tumechoka.



“Tukishamaliza na Majuto tunarudi na kwa Kanumba (marehemu Steven Kanumba) na msanii yeyote ambaye anaona ameingia mkataba wa kipumbavu, aje tuone. Mheshimiwa mwenyekiti inaudhi, lakini ndiyo hivyo.

“Leo hii Mzee Majuto yuko hospitalini, amekosa shilingi laki tano, nimtumie mimi wakati waziri pesa yenyewe ndiyo hiyo mnaelewa, eeh…maisha siyo…”

 IJUMAA NA DK MWAKYEMBE KATIKA MAZUNGUMZO

Baada ya tamko hilo la waziri huyo anayetaka kuuvunja mfupa uliowashinda mawaziri wenzake wengi wa kuwafanya wasanii wa Kibongo nao kula bata kupitia kazi zao za sanaa, gazeti hili lilizungumza katika mahojiano maalum na kutaka kujua amefikia wapi katika kushughulikia mikataba au naye amepoa?



Fasta bila kuchelewa, waziri huyo alipokea simu yake ya mkononi iliyopigwa na Mwandishi Wetu saa 7: 24 mchana wa Mei 9, mwaka huu na hapo ndipo alipofungua kabrasha la taarifa kamili juu ya kauli yake hiyo.

MSIKIE DK MWAKYEMBE

“Zoezi limeshaanza, kwa sababu suala la mikataba linahitaji umakini, weledi na kusimamia haki, nimeshaunda timu ya wanasheria watano ambao wanapitia hiyo mikataba.

“Lakini kwa sababu suala lenyewe ninahitaji liende haraka, ninakusudia kuongeza wanasheria wengine wanne ili wafikie tisa, lakini kwa sasa hao watano wameshaanza kuchambua baadhi ya mikataba inayolalamikiwa na wasanii wetu.

“Ninachoweza kukuambia ndugu yangu ni kwamba, katika hiyo mikataba tuliyopokea, tayari kuna mingine imeshachambuliwa na atumefikia hadi hatua za kuwakutanisha walalamikaji na wanaolalamikiwa, kwa hiyo zoezi linakwenda vizuri,” alisema Dk Mwakyembe wakati akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Mwandishi Wetu.

 ATOA WITO KWA WASANII

Aidha, Waziri Mwakyembe, mbali na kueleza kuwa atajitokeza hadharani hivi karibuni kuwaambia wananchi kile atakachovuna katika kazi yake hiyo aliyoianza amewataka wadau wa sanaa wenye mikataba yenye shaka wajitokeze ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.

Wito huo ulitolewa na waziri huyo baada ya gazeti hili kutaka kujua wizara yake iko ‘siriaz’ na mikataba ya Kanumba na Majuto peke yake au na wasanii wengine wanaweza kujiunga katika msafara huo aliouanzisha wa kuuangamizi unyonyaji.

MITAANI KWA WASANII KUKOJE?

Baada ya waziri kuliamsha dude, gazeti hili lilipita katika ulimwengu wa sanaa na kuwaangalia wasanii wenyewe wameipokeaje hatua hiyo ya waziri ambapo ilibainika kuwepo kwa vicheko na nderemo.

Mama mzazi wa msanii maarufu aliyega dunia miaka sita iliyopita, Steven Kanumba aitwaye Flora Mtegoa ni miongoni mwa watu waliofurahia hatua hiyo ya waziri.



“Mwanangu amefariki dunia, ameacha mikataba mingi kwenye makampuni, lakini hakuna nilichopata, kuna siku nilikwenda kwenye kampuni (anaitaja lakini tunahifadhi jina) kuulizia, nilipofika waliniambia Kanumba alishakufa na mikataba yake ilishakufa pia.

“Yaani sijui nikuambie nini, nimefurahi kusikia waziri anatafuta haki za mwanangu, najua kwa sasa yuko bungeni, akitoka huko nitakwenda kumuona,” alisema mama Kanumba.



Mbali na mama Kanumba, mwingine ambaye Ijumaa lilinasa habari za kulalamikia mkataba feki ni Wastara Juma ambaye mara kadhaa amekuwa akijitokeza na kudai kudhulumiwa kiasi cha shilingi milioni 80 na Kampuni ya KZG ya China.

Wastara anadai kuwa, KZG ilimpa mkataba wa kuwa balozi wa bidhaa za simu ya mkononi kwa makubaliano ya kiasi hicho cha fedha, lakini baadaye kampuni hiyo ilitimka nchini na kurejea China huku ikimwacha Wastara akilia.

 WANASHERIA WAFUKUA UTAJIRI WA KANUMBA, MAJUTO

Habari za chini ya kapeti zilizonaswa na gazeti hili zilidai kuwa, timu hiyo ya wanasheria walioteuliwa na Waziri Mwakyembe wameshaanza kufukua mikataba yote ya Kanumba na Majuto na endapo hali ikiwa upande wa wasanii hao, huenda utajiri ukawatembelea licha ya Kanumba kutokuwepo duniani na Majuto kuwa hospitalini huko India.

Kwa miaka kadhaa, kumekuwepo na kesi mbalimbali za wasanii wa Bongo kudhulumiwa haki zao, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuanza kupatiwa tiba na huenda likawatajirisha wasanii wengi.

 TUPEKUE KIDOGO HABARI HII

Pamoja na nia njema ya waziri ya kuwasaidia wasanii kupata haki katika mikataba feki, Timu ya Ijumaa inaungana na Waziri Mwakyembe na kumshauri kuwa jambo hilo linahitaji umakini mkubwa kulishughulikia kutokana na aina, maisha na uelewa wa wasanii wengi hapa nchini.

Kutokana na uzoefu na kuishi karibu na wasanii wa Bongo, gazeti hili limebaini kuwa maisha ya ‘njaanjaa za kujiendekeza’ yamekuwa yakisababisha baadhi ya wasanii kuingia mikataba feki ili kujipatia fedha hata kiduchu za kufanyia matanuzi mjini angalau kwa siku moja.

Kwa msingi huo, gazeti hili linawataka wasanii wa Bongo kutambua hadhi yao, kujielimisha kuhusu mikataba, kuacha tabia za kuingia mikataba kwa lengo la kukidhi shida ya siku moja.

Wednesday, May 16, 2018

TRA Yakamata Malori Yenye Bidhaa za Magendo

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata malori mawili yenye bidhaa mbalimbali eneo la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kupitia njia ya magendo yakitokea nchini Kenya zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20.

Akizungumza jana jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere alisema kuwa, malori hayo yenye namba T 985 AJP na T 840 ABF yalikamatwa usiku wa tarehe 10 Mei, 2018 na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo wamevunja sheria kwa kuwa hawakulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.

Kichere alifafanua kuwa, wafanyabiashara wenye bidhaa hizi zilizokamatwa, wamevunja kifungu cha sheria namba 82 na 200 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 na Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004.

"Kwa ujumla bidhaa hizi zote zina thamani ya shilingi 20,037,330.15 ambayo kodi ya bidhaa hizi ni shillingi 28,524,758.11 na adhabu au faini ya bidhaa hizi ni shilingi 10,768,665.08. Hivyo jumla ya mapato
yanayotakiwa kulipwa Serikalini ni shilingi 39,293,423.19," Kichere.

Ameongeza kuwa "Hivyo kwa Sheria hizo, wafanyabiashara hawa wanatakiwa kulipa kodi pamoja na faini ya shilingi milioni 39 na magari yao kutaifishwa".

Amezitaja bidhaa zilizokamatwa kuwa ni pamoja na mifuko 362 ya sukari yenye uzito wa kilo 50 kila mmoja, maboksi 40 ya mafuta ya kula yanayoitwa Karibu, maboksi matatu ya mafuta ya kula yanayoitwa Daria, magaloni 100 ya mafuta ya kula yanayoitwa Nyata na maboksi matatu ya viungo vya mboga

Kufuatia tukio hilo, Kamishna Mkuu Kichere amewakumbusha wafanyabiashara wote kuzingatia taratibu za uingizaji bidhaa nchini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na kuongeza kuwa, TRA haitavumilia ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara kwa kutozingatia sheria na taratibu hizo.

Kibatala Aiomba Mahakama Ifute Mashtaka Kesi ya Mbowe na Wenzake

Upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, umeomba Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali mashtaka dhidi ya washtakiwa kwa kuwa yanamapungufu, kisheria.

Maombi hayo yamewasilishwa jana Mei 16, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilabard Mashauri na Wakili Peter Kibatala, ambaye aliwasilisha mapingamizi nane ya kisheria ‘yanayoshambulia’ uhalali wa hati ya mashtaka na mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Katika Mapingamizi hayo, Kibatala alidai, kibali cha DPP kina mapungufu ya kisheria kwa sababu haioneshi imetolewa kwa mashtaka yapi na pia hati ya mashtaka imewataja majina washtakiwa wote bila ya kufafanua na pia imetaja tu kifungu cha sheria ambacho washtakiwa wameshtakiwa nacho huku akidai pia kwamba, hakuna kibali kilichowasilishwa mahakamani hapo kwa maana hiyo mashtaka dhidi ya washtakiwa yamepelekwa mahakamani hapo bila ridhaa ya DPP.

Aidha, Kibatala alitoa ombi mbadala na kuomba, iwapo mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao basi iyafutilie mbali mashtaka ambayo yanamapungufu kisheria, likiwamo shtaka la nne, latano, la sita na la saba.

Alidai, maelezo ya mashtaka hayo yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea ipasavyo, pia mashtaka hayo kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya (DPP) ambayo haipo kutokana na mapungufu hayo, inaonesha hakuna ridhaa yake.

“Kwa kuwa mashtaka hayo tajwa kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya DPP, lakini kuwa haipo tunaomba yafutiliwe mbali. Hati ya mashtaka inamapungufu kwa sababu shtaka la pili na la tatu hayana maelezo ya kutosheleza ya kuwapa washtakiwa msingi na uwezo wa kuweza kujitetea kikamilifu katika kesi hiyo ya jinai.

“Katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali hati haijataja watu waliotishiwa na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo haijulikani ni washtakiwa ama ni watu wengine. Mashtaka yanayowakabili washtakiwa yamejichanganya na hayaonyeshi walipelekeaje kifo cha Akwilina na hao majeruhi walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini,” alisema Kibatala.

Amedai maelezo katika hati ya mashtaka yamerundikana kiasi kwamba ni vigumu mtu kujitetea na kwamba unapomshtaki mtu kwa kisababisha kifo ni lazima utoe Maelezo ya kutosha kuonesha unamaanisha kitu Fulani ili mtu aweze kujitetea.

Alidai mapungufu mengine yaliyomo kwenye hati hiyo ni kuwa hayaoneshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya washtakiwa haki ya kujitetea. Kibatala alidai kuwa hati ya mashtaka inamapungufu kwa sababu vifungu vilivyotajwa katika shtaka la Tatu, tano na saba siyo sahihi.

Alidai kuwa katika shtaka la kumi, kumi na moja na kumi na mbili yanamapungufu kisheria kwa sababu hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya makosa ni wakina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa Kinondoni ama wapiga kura bila kujali itikadi zao.

Akijibu mapingamizi hayo, Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiomba mahakama kuyatupilia mbali mapingamizi yote hayo ya upande kwa kuwa hayana mashiko kisheria.

Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi, Kadushi alidai kuwa hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo na nini ama hakipaswi kuwepo.
 
Akiahirisha kesi hiyo, hakimu Mashauri alisema atatoa uamuzi kuhusu pingamizi hizo Juni 11, mwaka huu.

Mbali na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, washtakiwa wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU