RAIS
John Magufuli ameonesha nia ya kuhamia Dodoma kwa kuanza kushughulikia
masuala muhimu, ikiwamo ya kuzindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja
wa Ndege wa Dodoma na kuhamishia maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mkoani
Dodoma.
Akizungumza
juzi wakati wa mkutano wa kitaifa wa amani ulioandaliwa na Jumuiya ya
Ahamadiyya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema katika
kuonesha dhamira ya kuhamia Dodoma ambao ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya
Tanzania miaka ya 1970, Rais alielekeza fedha zilizobaki kwenye bajeti
iliyopita zitumike kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ambao pia
ujenzi wake utazinduliwa na Rais mwenyewe Julai 22, mwaka huu.
Aidha,
Rugimbana alisema Rais Magufuli pia ameagiza maadhimisho ya Siku ya
Mashujaa mwaka huu yahamie Dodoma ambapo kwa miaka mingi sasa yamekuwa
ikifanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa, Mnazi Mmoja Dar es Salaam.
“Ndio
natoka kwenye kikao cha kuzungumzia maadhimisho hayo kufanyika Dodoma
hilo linadhihirisha wazi dhamira ya Rais kuhamia Dodoma,” alisema
Rugimbana na kuongeza kuwa Rais Magufuli atashiriki Mkutano Mkuu Maalumu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utakaoanza Julai 23, mwaka huu.
Akizungumzia
suala la amani, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali itawachukulia hatua
kali viongozi wa taasisi mbalimbali ambao wamekuwa na tabia za kutumia
nafasi zao kuhubiri uchochezi na hivyo kutishia amani na utulivu wa
nchi.
Alisema
viongozi ambao wamekuwa na tabia za kutumia taasisi zao kama sehemu ya
kuhubiri masuala ya uovu, ikiwemo kushawishi vitendo vya uvunjifu wa
amani, serikali haitawafumbia macho.
Aliwataka
viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba za
taasisi zao na siyo kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi na tamaa.
Alisema pia serikali inaunga mkono jitihada za taasisi za dini katika
kuhubiri amani na utulivu wa nchi ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi
mbalimbali.
“Kama
serikali, tunaunga makono jitihada zenu mbalimbali ikiwemo kupinga
vitendo vya maovu pamoja na ufisadi ambao umekuwa ukilitafuna taifa
letu,” alisema.
Naye
Mwakilishi wa Jumuiya hiyo ya Ahmadiyya, Abdulrahman Ahmed akitoa mada
kuhusu amani, alisema Waislamu wanatakiwa kuzingatia miiko ambayo
imewekwa na dini hiyo katika kusaidia kudumisha amani na utulivu.
Wakati
huo huo, mapema wiki hii Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa alisema serikali inakarabati na kuongeza ukubwa
wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili upokee ndege kubwa za mizigo, abiria na
viongozi wa kitaifa na kimataifa, ikiwa ni maandalizi ya kuufanya mkoa
kuwa makao makuu ya nchi kivitendo.
Ujenzi
huo unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 11.5 ambazo ni fedha za
ndani na utakamilika kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa mashirika ya
ndege kuanza huduma mkoani Dodoma, ikiwemo ndege kubwa zitakazonunuliwa
na serikali mwaka huu.
Profesa
Mbarawa akizungumza baada ya kukagua uwanja huo alisema uamuzi huo
unafikiwa kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kutaka kuufanya Dodoma
makao makuu ya nchi kivitendo, jambo linalotarajiwa kuongezeka shughuli
mbalimbali zikiwemo za kiutawala, uchumi, biashara na diplomasia
sambamba idadi ya wageni.
Kwa
upande wake, Meneja Mradi wa Upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbila Mdemu alisema mpaka sasa mita
900 zimekamilika kwa kuweka tabaka la kwanza lami katika eneo la kuruka
na kutua ndege na kazi ya kuchimba na kusawazisha eneo la kurefusha njia
imekamilika.
Alisema
wanatarajia kukamilisha kazi hiyo kwa muda mfupi. Upanuzi wa uwanja huo
unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa Km 2.5 na
mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.