test

Monday, July 25, 2016

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya Kumi na Tisa

Mtunzi: Enea Faidy
 
.....DORICE alipozitazama zile nguo zilikuwa ni nguo nzuri sana za kuvutia. Kulikuwa na gauni moja refu linaloacha wazi mikono lenye rangi ya dhahabu inayong'aa sana. Kulikuwa na viatu virefu vinavyoelekeana na rangi ya gauni kidogo, ushungi wenye rangi ya gauni, mkufu wa dhahabu pamoja na hereni.

Dorice alivishangaa vitu vile kwa mshangao wakati huo Mansoor alikuwa akiachia tabasamu mwanana pembeni yake.

"Vaa Dorice!" Ilisikika sauti ya Mansoor ndipo Dorice alipopata nafasi ya kumtazama tena Mansoor. Akapigwa na bumbuwazi baada ya kuona mansoor amevalia nguo tofauti na alizokuwa amevaa mwanzo, alionekana kama mwanaume wa kihindi pale anapofunga ndoa kwa mavazi yake. Dorice alimshangaa sana Mansoor, woga kiasi ukamvaa moyoni mwake kisha akaanza kuzivaa nguo zile alizopewa na Mansoor.

Pindi anapozivaa nguo zile Mansoor alikuwa tayari ameshatoweka eneo lile.Dorice alipovaa nguo zile, alibadilika sana. Alionekana mrembo mno kwa jinsi alivyopendeza. Ukimtazama kwa haraka utadhani msichana kutoka India kumbe ni mnyaturu wa Singida. 


Alijitazama kupitia kioo kilichokuwa mbele yake, akajikiri kwamba kweli Mungu hakumkosea katika uumbaji ila alitumia ufundi wa hali ya juu katika kukamilisha sura na umbile lake.

Bada ya kumaliza kuvaa, Mansoor alitokea tena palepale alipokuwa amesimama mwanzo. Alimshtua sana Dorice lakini tayari alikuwa ameshaanza kumzoea Mansoor hivyo hakuogopa sana.

"Umependeza sana Malkia wangu.. Kwa jinsi ulivyositamani hata uende Duniani.. Nahisi wivu sana.." Alisema mansoor huku akimtazama mrembo yule kama waridi likiwa bustanini wakati wa jua la asubuhi.

"Uliniahidi nini?" Aliuliza Dorice kwa hamaki."Usijali... Nitakupeleka duniani kama nilivokuahidi ila nimekuambia tu hisia zangu... Kama unanipenda kweli ni heri ubaki na mimi huku huku kwetu!" Alisema Mansoor kwa sauti ya upole sana. Dorice hakijibu kitu. Wakaondoka pale na kwenda moja kwa moja kwa malkia.

Malkia alifurahi sana kuona kijana wake ameambatana na mtu ampendae. Radi tatu mfululizo zilipigwa ili kudhihirisha furaha aliyokuwa nayo malkia. Mansoor alitabasam akiwa amemshika mkono mkewe mtarajiwa.

"Harusi ya mwanangu Mansoor... Iwe ya furaha sana kwani amepata kile alichokuwa anahitaji.." Alisena malkia kwa sauti kali. Dorice alimtazama Mansoor kwa woga.

"Usiogope malkia wangu.. Na kuanzia Leo nitakuita Aisha..!"
"Aisha! Kwanini?" Alihamaki Dorice.
"Ukiwa mke wangu huwezi kuitwa Dorice.." Alisema Mansoor.

Wakati Dorice akiendelea kushangaa ghafla upepo mkali ukapigwa, halafu kwa muda huohuo walijikuta wapo eneo lingine lililojaa watu wengi ambao Dorice hakuwaelewa elewa kwa jinsi walivyokuwa.
********
Majira ya SAA moja jioni Mr. Alloyce alikuwa amewasili nyumbani kwake. Kichwa kilijaa mawazo tele ambayo hakujua yataisha vipi kwani matatizo aliyokuwa nayo yalikuwa ni mazito kuzidi kilo mia za Mawe. Njia nzima aliwaza na kuwazua lakini bado alijiona yupo kwenye msitu mkubwa wa matatizo ambao hakujua atapenya vipi ili kuepukana nao.
Kila Mara sura ya mkewe mpenzi ilimjia kichwani mwake hakuamini kama kweli amempoteza katika mazingira ambayo ilikuwa vigumu kuyaelewa. Alimfikiria mwanawe Eddy ambaye mpaka Dakika ile hakujua angeanzia wapi kumtafuta ilhali hajui alikoelekea!. Kichwa kilimgonga sana kwa mawazo.

Alifika getini kwake na kumkuta mlinzi wake ambaye alimfungulia. Bila hata ya salamu Mr.Alloyce alipita getini pale na kuelekea ndani lakini alishtushwa sana kuona taa zinawaka ndani pia alisikia sauti kubwa ya muziki. Mr.Alloyce alisitisha mwendo wake kidogo. Akamgeukia mlinzi.

"We Seba nani yupo ndani?"
"Atakuwa Eddy Huyo.."
"Eddy! Eddy gani?" Mr. Alloyce alishtuka sana.
"Kwani kuna Eddy wangapi hapa Mzee..!" Alijibu Mlinzi Seba kwa masihara kwani alikuwa ni MTU wa masihara sana.
"Sipo kwenye utani ujue Seba.. Nani yupo ndani?.." Aliuliza kwa hasira mr. Alloyce kwani alihisi Seba anamtania.
"Eddy Mzee.." Alijibu mlinzi.
Mr.Alloyce alihisi kama nguvu zikimpungua mwilini mwake kwani alikuwa haamini yanayotokea kwenye maisha yake. Alijkuta anapatwa na woga ghafla.

"We Seba hebu twende wote ndani..!" Seba hakusita aliamua kumsindikiza bosi wake. Lakini moyoni mwake alikuwa na maswali mengi kwa nini bosi iweje arudi peke yake tena kwa mguu bila gari?. Alijiuliza ila hakuthubutu kunyanyua mdomo wake kuuliza chochote kwani alishaona hali ya bosi wake siku ile haikuwa nzuri.

Walifika mlangoni na kukuta mlango ukiwa wazi ilhali waliondoka na funguo. Suala like lilizidi kumchanganya Mr.Alloyce.

"Hebu niitie Huyo Eddy kwanza!" Alisema Mr.Alloyce kwani alikuwa anaogopa kuingia ndani ila hakujionesha kwa Seba kuwa alikuwa na hofu.

"Eddy!" Aliita Seba.
"Naaam!" Sauti kutoka ndani ilisikika.
"Muite aje nje.. Haiwezekani afungue mziki kama disco humu.." Alisema Mr Alloyce kwa kujivungisha tu kwani bado alikuwa haamini kama Kweli Eddy yupo nyumbani.

"Njoo huku we bwana mdogo.." Alisema Seba. Punde tu, Eddy alitoka nje na kumkuta baba yake. Mr.Alloyce alishtuka sana akahisi yupo ndotoni lakini ilokuwa sio ndoto Bali kweli. Machozi ya furaha yalimtoka, kwani hakutaraji kama angemkuta mwanaye akiwa yuko hai.

"Daddy! Karibu ndani!" Alisema Eddy kwa uchangamfu sana.
"Asante! Seba waweza kwenda..!" Alisema Mr.Alloyce huku wakiingia ndani na mwanae. Mr.Alloyce alishindwa kuizuia furaha yake, alijikuta anamkumbatia mwanaye kwa nguvu huku chozi likimdondoka.
"Eddy mwanangu umefika SAA ngapi?"
"Nilikuja toka mchana..!"
"Kwanini ulitutoroka?"
"Niliwatoroka wapi?" Aliuliza Eddy kwa mshangao, swali hilo lilimshangaza sana Mr.Alloyce. Ila hakutaka kuendekeza zaidi mada ile akijua kuwa inaweza sababisha mambo mengine.
"Umekula nini?" Aliamua kubadilisha mada Mr.Alloyce.
"Nilipika ugali na samaki zilizokuwemo kwenye jokofu."
"Ulikula ee..?"
"Ndio"

Mr.Alloyce alishangaa sana kusikia vile kwani hakutegemea kama Eddy angekula chakula kwani siku zote alikuwa akikataa chakula akidai ni kichafu. "Leo amekula?" Alijiuliza Mr.Alloyce ama kweli Mungu ametenda.

Mr. Alloyce pia alimshangaa sana mwanaye kwa uchangamfu aliokuwa nao siku ile, alikuwa na furaha ambayo Hakuwahi kumwona akiwa nayo tangu apate matatizo yake. Mr.Alloyce alifurahi ingawa alijiuliza sana imekuwaje?. Baada ya wote kuketi kwenye viti kwa ukimya mzito, ndipo Eddy alipoamua kuvunja ukimya kwa kumtupia swali baba yake. Swali lililoibua simanzi moyoni mwa Mr.Alloyce.

"Mama yuko wapi?"
Swali hilo liliibua machozi kwa Mr. Alloyce, alishindwa amwambie nini mwanaye.
"Daddy mbona unalia kulikoni?" Aliuliza Eddy kwa mshangao.

"Eddy... Mama yako amefariki... Sielewi ntafanyaje... Sielewi ntawaambia nini ndugu zake mpaka wanielewee.. Sielewi..!"
"Amefariki? Kivipi?" Eddy alishtuka sana.
"Amefariki baada ya wewe kutoroka..!"
"Kwani Mimi nimewatoroka wapi?"
"Eddy umesahau au..? "
*********
Mwalimu Amina na Matron walibaki wakishangaana tu kwani walipoingia bwenini alikokuwa amelala Doreen. Hawakumkuta mtu yeyote ila walikaribishwa na harufu kali ya haja kubwa. 

Walipotazama chini kulikuwa na hali mbaya sana kwani kinyesi kilikuwa kimetandazwa chini kwa mafungu kama matano. Walikunja sura zao kwa kinyaa hawakutaka hata kuingia bwenini mle.
"Doreen!" Aliita Madam Amina kwa sauti lakini hakujibiwa. Alienda hadi chooni kumwangalia lakini hakuwepo.Madam Amina aliamua kwenda madarasani kumtafuta lakini ilikuwa kazi Bure kwani huko pia hakuwepo.

"Dunia ina mambo..!" Alisema Madam Amina. Matron alibaki anashangaa tu huku anatikisa kichwa kwa masikitiko.
"Ila tusije tukauliwa na sisi...!" Alisema Matron.
"Hakuna kitu kama hicho..!"
" mbona unajiamini sana? Una nini mwenzetu?"
"Mungu tu ndo nilienae ananifanya nijiamini sana..!"
"Mh Haya.. Nimeamini kweli huyu mtoto ni mchawi haswa.. Kweli amejisaidia bwenini namna ile?.. Sasa sijui ameenda wapi.."Alisema matron.
"Bora tu aondoke ili shule ibaki na Amani tu..!" Alisema Madam Amina.
Kiukweli aliwashangaza sana. Ila bado hawakujua binti yule ameenda wapi.
 
*********
Mwalimu Jason alikuwa ameshikilia kisu kile chenye makali ili atimize sharti alilopewa kwenye karatasi lile la ajabu. Machozu yalimchuruzika sana, alilia kwa uchungu ulioje.

"Judith... Nakupenda... Ila sina budi kufanya hili...!" Alisema mwalimu Jason huku akitamani kusitisha jambo analotaka kufanya lakini alishindwa kutokana na nguvu za Giza zilizokuwa zikimshinikisha kufanya vile. Alimuonea huruma sana Judith, msichana ambaye alimpenda kwa dhati na kuahidi kufunga naye ndoa. Alimtazama Judith kwa simanzi, judith alikuwa akilia sana huku haja ndogo ikimshuka taratibu miguuni mwake. Alitetemeka kwa hofu sana akijuta kwanini alienda kumtembelea Jason.

"Nataka titi lako.."
"Jason kweli we umekuwa katili namna hiyo.. Kwanin lakini Jason.. Nimekosa nini .." Alilalamika Judith machozi yakimchuruzika mashavuni mwake alikuwa mwekundu kama pilipili iliyoiva.

"Kwa sababu hiyo.. Bora nife Mimi Judith.. Maana nina mawili tu ya kuchagua. ." Jason aliposema hivyo tu akakiinua kisu na kukishusha kwa kasi mpaka kifuani kwake. Kikazama taratibu huku Judith akimshuhudia jinsi Jason anavyojiua..Akataka kupiga kelele lakini akajiziba mdomo kwa hofu na mshangao...
 Itaendelea.......
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU