CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kulisaidia Jeshi la
Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hivi
karibuni Jeshi la Polisi lilitoa zuio la mikutano ya siasa ya wazi na
ya ndani nchini kote, hata hivyo CCM imepanga kufanya Mkutano Mkuu
tarehe 23 Julai mwaka huu mjini Dodoma.
Kwenye
mkutano huo, Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM atakabidhi mamlaka
hayo kwa Dk. John Magufuli ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa chama hicho.
Baraza
la Vijana wa Chadema (Bavicha) limepanga kuzuia mkutano huo kwa madai
ya kulisaidia Jeshi la Polisi kusimamia agizo lake kwa vyama vya siasa
nchini.
Wakizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam viongozi wa Bavicha
walisema, hatua hiyo ni katika kuhakikisha wanalisaidia jeshi kutekeleza
amri iliyotolewa na Rais Magufuli ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa
hadi mwaka 2020.
“Tumeandaa
vijana takribani 2000 kutoka mikoa yote nchini watakaokwenda Dodoma
kusaidiana na Jeshi la Polisi kutawanya mkutano usio halali wa CCM. Kwa
sababau Jeshi la Polisi limezuia mikutano yote ya siasa kwa sasa.
“Pia
ni katika kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwamba, hakuna mikutano
ya vyama vya siasa mpaka mwaka 2020. Huu ndio msiamamo wa baraza.
“Mikutano
yetu sisi kama Chadema tunazuiwa lakini CCM wanafanya. Mahafari ya
chama cha mapinduzi yanafanyika. Ni jana CHASO (Jumuiya ya Wanafunzi wa
Vyuo Vikuu Chadema) Morogoro tumezuiwa lakini UVCCM (Umoja wa Vijana wa
CCM) Mkoa wa Morogogo wamefanya na picha zipo. Hii sio haki, kama mbwai
na iwe mbwai,” alisema Patrick ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo.
George Tito, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya alisema “… ni kwamba, huko mikoani vijana wameshajipanga. Wana ari kubwa ya kwenda Dodoma.
“Tumeamua
kufikia hatua hii kwa sababu tumekuwa tunaona hakuna haki katika nchi
hii. Kuna mahafali yanafanyika vyuo vikuu, wenzetu CCM wanaruhusiwa sisi
Chadema tunakatazwa.Vijana wa Chadema wamekuwa wakikamatwa bila sababu
za msingi,” alisema Tito.