test

Monday, August 1, 2016

Waziri Mkuu Aitaka Wizara Kuweka Mikakati Ya Kuendeleza Uvuvi Katika Kina Kirefu Cha Bahari


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha wananchi kuvua katika maji ya kina kirefu cha bahari kwa kutumia meli kubwa na za kisasa ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imekuwa ikichukuliwa na wavuvi wenye vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.

Aidha, amezitaka halmashauri zote nchini ziweke mikakati na mipango ya kuifanya mito na maziwa mbalimbali nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli za wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema bado nchi haijaweza kutumia rasilimali hiyo kikamilifu.

Amesema halmashauri zinatakiwa zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha miradi ya kufuga samaki katika maeneo yao na wewezeshwe kupata teknolojia ya ufugaji huo.

Akizungumzia vikundi vya wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa alishauri waelimishwe kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana bora za kisasa za uvuvi ili shughuli zao ziwe na tija.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema wakulima wanatakiwa  kuzingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa na wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.

Akizungumzia kuhusu suala la usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali alipata fursa ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.

Amesema amefurahi kuona wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo wana ari kubwa ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza uchumi wa viwanda.

“Naamini kuwa pamoja na lengo la kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi wataongeza ari ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,” alisema.

Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kushirikisha taasisi za umma na binafsi, mashirika na vikundi vya ujasiriamali katika maeneo yao.

Akizungumzia namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.

Awali Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda na maeneo ya vipando vya mazao mbali mbali yaliyoko katika viwanja hivyo ambapo alisema ameridhishwa na juhudi zilizofanyika katika maandalizi ya maonesho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa uwanja huo.

“Napenda kutoa pongezi za dhati kwa kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za kufanyia maonesho. Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu, Mashirika yetu ya Umma na binafsi; na watu binafsi ambao wamejenga na wanaendelea kujenga majengo mazuri na ya kudumu,” alisema.

Pia alizindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na kusema kuwa uboreshaji wa viwanja hivyo unaonesha jinsi wadau wote katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika wanavyotambua umuhimu wa maonesho hayo kama njia ya kuongeza maarifa na kumuenzi mkulima, mfugaji na mvuvi kwa kutambua mchango wao katika uchumi wa Taifa.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo: vijana shiriki kikamilifu   (“HAPA KAZI TU”) 
        
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 01, 2016.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU