Kada aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ally Muswanya ameachia wadhifa huo hata kabla ya kuapishwa.
Wakati
uteuzi wa makada watatu wa kwanza ulisahihishwa na Ikulu, Maswanya
hajaibuka kwenye hafla ya kiapo na tayari mtu mwingine amekwenda kuziba
nafasi yake.
Maswanya,
ambaye alikuwa aapishwe juzi na mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa,
hakuapishwa na badala yake aliapishwa John Palingo ambaye katika uteuzi
uliotangazwa na Ikulu alikuwa aongoze Wilaya ya Kongwa.
Taarifa
za Maswanya kuachia nafasi hiyo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya
kijamii juzi usiku zikieleza kuwa amejiuzulu nafasi hiyo, lakini
haikuelezwa sababu za kuchukua uamuzi huo wa kukataa kumwakilisha Rais
wilayani.
Hata
hivyo, Maswanya, ambaye ni meneja wa kampuni ya huduma za simu ya Tigo,
Kanda ya Ziwa, hakutaka kuzungumzia kwa kina sakata hilo.
“Kama ambavyo inajulikana, mimi ni meneja wa Kanda wa Tigo,” alisema Maswanya alipozungumza na Mwandishi
“Hayo
ndiyo yako kwenye mamlaka yangu kuzungumzia. Kama ni suala la Tigo,
karibu tuzungumze yote kuhusu mipango na mikakati yetu.”
Maswanya
alisema kwa sasa, nguvu akili na uwezo wake wote anaelekeza katika
kutimiza wajibu kwenye nafasi hiyo yake Kanda ya Ziwa.
Hata baada ya kuulizwa kama ndiye aliyekataa uteuzi, Maswanya alisisitiza “Hayo yatazungumziwa na mamlaka husika ambazo naamini kwa nafasi yako unazijua.”
Alipoulizwa
kama Maswanya alihudhuria hafla ya kula kiapo ya wakuu wa wilaya
katikati ya wiki, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Rais,
Gerson Msigwa alisema hafahamu kama alikuwapo au la kwa kuwa wengi ni
wakuu wapya hivyo haikuwa rahisi kwake kujua nani hakuwapo.
Sarakasi
ya meneja huyo kutochukua madaraka aliyopewa na Rais inafanya idadi ya
watu walioteuliwa na kushindwa kuanza kazi kutokana na sababu tofauti
kufikia wanne.
Kabla
ya wakuu wateule kula kiapo cha maadili Ikulu jijini Dar es Salaam,
Rais Magufuli alieleza kuwa uteuzi wa wakuu hao ulifanywa kwa makini na
kwamba anafahamu kwa majina watu wote aliowateua, akisema alizingatia
umri, elimu na uzoefu.
Tukio
la kwanza lilikuwa la uteuzi wa Fikiri Said kuwa mkuu wa Wilaya ya
Ikungi, lakini akabadilishwa kwa maelezo kuwa jina lake liliwekwa
kimakosa. Badala yake aliyekuwa katibu wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Miraji
Mtaturu akateuliwa kuchukua nafasi hiyo.
Pia
aliyeteuliwa kuongoza Wilaya ya Rombo, Fatma Toufiq alibadilishwa kwa
maelezo kuwa tayari alishakuwa na wadhifa mwingine wa ubunge wa viti
maalum na nafasi yake akapewa Agness Hokororo.
Rais
John Magufuli alisema wakati akielezea suala hilo kuwa hakutaka mtu
ashike nafasi mbili kwa wakati mmoja na kwamba hiyo ndiyo tafsiri ya
falsafa ya “Hapa Kazi Tu”.
Tukio
lililokuwa la aina yake katika uteuzi huo ni la kubatilisha uteuzi wa
Emile Ntakamulenga aliyetangazwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Serengeti.
Hakukuwa
na taarifa za awali za kubatilisha uteuzi huo na Ntakamulenga alienda
Ikulu kama makada wengine, akaruhusiwa kujisajili na kuingia kwenye
viwanja vya makazi hayo makuu ya nchi.
Lakini
wakati akisubiri kula kiapo cha maadili, Jaji Salome Kaganda akatoa
maelezo kuwa kulifanyika makosa katika kutangaza jina lake na kwamba
aliyekusudiwa alikuwa Nurdin Babu ambaye naye alikuwa ameitwa Ikulu siku
hiyo.
Kutokana
na makosa hayo, Jaji Kaganda alisema: “Naomba utupishe” na ndipo
Ntakamulenga akanyanyuka na kuanza kuondoka kutoka viunga vya Ikulu
akiacha maswali.
Akizungumzia
kutoapishwa kwa Maswanya kuwa mkuu wa Wilaya ya Mbozi na badala yake
kumwapisha Palingo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa alisema
alipokea ujumbe mfupi kwa njia ya simu kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi
akijulishwa kwamba mtu aliyekuwa amepangiwa wilaya hiyo, John Ernest
Palingo amebadilishwa kituo cha kazi, hivyo ataongoza Mbozi.
Galawa
alisema alipokea maelekezo ya ujumbe huo kutoka kwa Katibu Mkuu
Kiongozi kwamba ampokee na kumuapisha ili aanze kazi mara moja, lakini
akaongeza kuwa hana taarifa za mtu aliyeteuliwa awali kuwa bosi wa
Mbozi.
“Nilichofanya ni kutekeleza maagizo ya mkuu wangu,” alisema Galawa.
“Pia
mimi nilichokuwa nahitaji ni kukamilishiwa ma-DC wangu kwa wilaya zote,
hivyo jana (juzi) asubuhi nilifanya mawasiliano na DC aliyeelekezwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, tukamtumia tiketi ya ndege na jana (juzi) mchana
alifika na nikamuapisha kwa kuwa ni DC wa Mbozi pekee aliyekuwa
amebaki.”
Alisema
siku ya Alhamisi alimuapisha mkuu wa Wilaya ya Ileje, na kwamba wengine
wa wilaya za Momba na Songwe hawakutumiwa tiketi mapema, lakini
walifika na juzi asubuhi aliwaapisha wakati wakimsubiri Palingo.
Alisema
kazi ya kwanza kuwapangia ni mbio za Mwenge wa Uhuru ambao uliingia
jana asubuhi mkoani kwake ukitokea Mbeya. Alisema mwenge huo
utawawezesha kufahamu vyema jiografia ya wilaya zao.
Mkoani
Dodoma, Jordan Rugimbana aliwaapisha wakuu wapya sita kati ya saba wa
wilaya za mkoa huo baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko madogo.
Baada
ya kuwaapisha wakuu hao wa wilaya, Rugimbana alielezea mabadiliko hayo
ya Rais yaliyofanya akosekane mteule wa wilaya moja.
“Aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa sasa atakwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi baada ya aliyeteuliwa kujiuzulu,” alisema.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, Wilaya ya Kongwa inasubiri uteuzi mwingine utakaofanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Wakuu
wa wilaya walioapishwa Dodoma ni Elizabeth Kitundu (Bahi), Vumilia
Nyamoga (Chamwino), Simon Odunga (Chemba), Christina Mdeme (Dodoma
Mjini), Veneranda Makota (Kondoa) na Jabir Shekimweri (Mpwapwa).