SERIKALI
imetangaza kununua rada mbili mpya kwa ajili ya kusaidia kukusanya
mapato, zaidi ya Sh bilioni 18 ambazo zinapotea kila mwaka kutokana na
kukosekana udhibiti katika anga la Tanzania.
Kauli
hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Ujenzi na Teknolojia, Edwin Ngonyani, kwenye mkutano uliowakutanisha
wataalamu wa masuala ya anga pamoja na wamiliki wa kampuni za ndege
barani Afrika.
Alisema
katika awamu ya kwanza, Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kununua
rada mbili ambazo zitafungwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius
Nyerere na Kilimanjaro (KIA), huku awamu ya pili ikifungwa katika
viwanja vya Mwanza na Songwe.
“Serikali
tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inanunua rada
mbili, ili kuokoa kiasi cha takribani bilioni 18/- ambazo zimekuwa
zikipotea kila mwaka, jambo ambalo linafanya nchi kupoteza mapato, kwani
inakuwa haiwezi kulisimamia anga lake lote na hivyo kufanya ndege, hata
zile zisizotua nchini huku zikitumia anga hilo, kushindwa kulipa
ushuru.
“Kwa
sasa Kenya na Rwanda ndiyo nchi zenye rada hizo licha ya kuwa nchi hizo
ni ndogo ukilinganisha na Tanzania, rada hizi kila moja inauzwa dola za
Marekani milioni 24. Unapoagiza unatakiwa kulipia nusu ya gharama na
pindi inapokamilika unamalizia nusu iliyobaki,” alisema Naibu Waziri Ngonyani.
Kwa
upande wake, Mkurungezi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa ununuzi wa rada hizo utasaidia
kuongeza mapato na hivyo kufanya viwanja vya ndege kujiendesha vyenyewe
bila kusubiri msaada kutoka serikalini.
Katika
hatua nyingine, Johari alisema kuwa mamlaka hiyo imesema Tanzania bado
haijafikia kiwango cha utengenezaji ndege na hivyo kuwapiga marufuku
wanaofikiria kuzitengeneza bila kuwa na kibali cha mamlaka hiyo.
“Ili
kuunda ndege unatakiwa kuwa na zana za kisasa… Kwa Tanzania bado
hatujafikia uwezo huo, hivyo kama TCAA tunatoa wito kwa wale wote
wanaotaka kufanya hivyo bila kushirikisha mamlaka, kuacha mara koja
mpango huo kwani ndege hizo wanazotengeneza bila kufuata taratibu, ni
hatari na zinaweza zisimudu kukaa hewani muda mrefu na hivyo kusababisha
hatari kubwa.
“Hivyo
kama mtu anafikiri kuwa ana mawazo ya kutaka kutengeneza ndege, ni
lazima aanzie kwetu ili tumshauri kupitia wataalamu wetu na si
vinginevyo,” alisema Johari.
Mkutano
huo ulikuwa ukikutanisha wamiliki wa ndege zilizokidhi vigezo na wadau
mbalimbali wa masuala ya anga kutoka kote Afrika, ukiwa na lengo la
kujadili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.