Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.
Aliwataja
wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75)
ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.
Msengi
alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo
bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi
la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati
wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.
Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa
na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza
kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.
Hata
hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia
nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.
Alilaani
kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee
kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi
dhidi yao.
Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.
Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.