Maandalizi ya CCM kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho ili ashike kofia zote mbili, yataanza kesho katika kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Taarifa kuhusu kikao hicho iliyotiwa saini na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ilisema: “Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM itafanya kikao cha kawaida siku ya
Jumamosi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kitafanyika chini ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.”
Japokuwa
taarifa hiyo haikueleza ajenda za kikao, habari kutoka ndani ya chama
zinasema kikao hicho cha siku moja kinatarajiwa kujadili masuala
mbalimbali, ukiwamo mchakato wa makabidhiano ya kiti hicho katika
mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao.
Kipindi
cha uongozi wa chama kwa Kikwete kitamalizika mwakani, lakini imekuwapo
desturi kwa rais mpya kuachiwa kofia hiyo mapema, hivyo Rais Magufuli
anatarajiwa kurithi mikoba ya uenyekiti mwezi ujao.
Vilevile,
kikao hicho kinatarajiwa kuhitimisha hoja zinazodaiwa kuibuka katika
vikao vya ndani vya chama hicho kwamba CCM inataka kuvuruga utaratibu
uliodumu kwa muda mrefu wa mwenyekiti kumwachia kijiti Rais aliyeko
madarakani.
Madai
kuhusu mkakati huo wa ndani yalisambazwa katika mitandao ya kijamii
yakimnukuu Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
lakini Ole Sendeka alisema hana sababu yoyote ya kumjibu kiongozi wa
dini.
Februari
5, mwaka huu Kikwete alipokuwa anazungumza na wazee wa Manispaa ya
Singida alisema sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya miaka 39 tangu
chama hicho kuanzishwa zilikuwa za mwisho kwake akiwa mwenyekiti, kauli
ambayo iliashiria ataachia mapema uenyekiti.
Kwa desturi, wenyeviti wa CCM huwa wanaachia madaraka yao kabla ya muda wa uongozi wao kumalizika.
Rais
wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikabidhiwa chama na Alhaji Ali
Hassan Mwinyi mwaka 1996 badala ya 1997 na Mkapa alimkabidhi Kikwete
kiti hicho mwaka 2006 badala ya 2007.
Kulingana
na kalenda ya chama hicho, Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua mwenyekiti
unapaswa kufanyika mwaka 2017, lakini utafanyika mwaka huu kuendeleza
utamaduni wa kung’atuka mapema.
Habari
kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kinachoendelea sasa mikoani
na wilayani ni maandalizi ya mkutano huo mkuu yanayosimamiwa na Naibu
Katibu Mkuu wa Bara, Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti.
“Kikao
hicho cha Kamati Kuu ndicho kitakachojadili ajenda za mkutano huo
sambamba na kupanga tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu,” zilieleza taarifa hizo.
Dk
Magufuli anatajwa kuwa uongozi wake ndani ya CCM utakuwa wa kasi ya
aina yake kutokana na hatua mbalimbali za ‘utumbuaji majipu’
anazozifanya ndani ya Serikali tangu Novemba 5, alipoapishwa kuwa Rais.
0 comments:
Post a Comment