test

Friday, June 17, 2016

Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi Wasomwa ..Waliohukumiwa kwa Rushwa Kunyimwa Zabuni, Mikataba yote Kuwa na Mashuhuda


MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi wa Mwaka 2016, umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana na kuwekwa wazi kwa umma, na moja ya vifungu vinavyopendekezwa ni kuzuia mtu yeyote aliyewahi kuhukumiwa kwa rushwa, kufanya biashara na serikali.

Katika marekebisho hayo yanayopendekezwa na serikali, wizara, taasisi au shirika lolote la serikali wakati wa kufanya biashara na kampuni yoyote, ikibaini kampuni husika au mmoja wa wakurugenzi wake aliwahi kuhukumiwa kwa rushwa, biashara hiyo itasitishwa mara moja na taarifa kutolewa serikalini.

Mbali na watu waliohukumiwa kwa makosa ya rushwa, marekebisho hayo yamependekeza kuwa pamoja na sifa nyingine za viongozi wakuu wa serikali hasa maofisa watendaji wakuu, watapaswa kuwa na sifa ya ziada ya uzoefu katika masuala ya manunuzi.

Katika kukidhi haja ya kuondoa malalamiko ya sheria iliyopo kutumika kuibia nchi, marekebisho hayo yamesisitiza bei za huduma na bidhaa zitakazotolewa ziwe za soko, ununuzi ufanyike moja kwa moja kiwandani badala ya kupitia kwa mtu wa kati na mkataba wa manunuzi, lazima usainiwe mbele ya mashuhuda.

Watuhumiwa wa rushwa
Katika Ibara ya 83 ya Sheria hiyo, imependekezwa ibara ndogo ya pili kwamba shirika au wizara itakaporidhika kwamba kampuni au mtu anayependekezwa kupewa zabuni, amewahi kutangazwa na Mahakama kuwa alishiriki katika vitendo vya rushwa, ufisadi, au ukiukwaji wa taratibu wakati wa kushindania zabuni, ofisi hiyo ya umma itapaswa kukataa pendekezo la kumpa mhusika zabuni hiyo.

Ofisi hiyo ya umma, pia itapaswa kumtangaza mtu huyo au mzabuni ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wake, kuwa hawapaswi kupewa zabuni yoyote inayogharimiwa na fedha za umma.

Pia ofisi hiyo ya umma, itapaswa kumtaka huyo mtu au mzabuni, kurejesha sehemu ya fedha aliyopewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa au huduma au kuzuia sehemu ya fedha iliyopaswa kwenda kwa mzabuni kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa au huduma.

Mapendekezo hayo yameendelea kuitaka ofisi husika ya umma ndani ya siku saba baada ya kutangaza kuwa mzabuni huyo, hafai kupewa zabuni inayogharimiwa na fedha za umma, kuwasilisha jina la mzabuni na wakurugenzi wake kwa mamlaka inayotajwa na sheria husika.

Mamlaka hiyo nayo imetakiwa na mapendekezo hayo ya sheria, kwamba baada ya kupata taarifa hiyo, kumfungia mtu au mzabuni husika asipate zabuni yoyote inayogharimiwa kwa fedha za umma, kwa muda usiopungua miaka 10.

Sifa za CEO
Katika mapendekezo kwenye Kifungu cha 23 cha Sheria hiyo, Kifungu Kidogo cha II, kimezungumzia uteuzi wa maofisa watendaji wakuu wa ofisi hizo za serikali.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa ofisa mtendaji mkuu, atateuliwa kutoka kati ya wataalamu wenye uzoefu wa angalau miaka 10 katika fani za uhandisi, usanifu wa majengo, sheria, menejimenti ya ununuzi na usambazaji na ukadiriaji majengo.

Fani nyingine zilizotajwa ni pamoja na uongozi wa biashara, mipango ya kiuchumi na maendeleo au katika fani nyingine yoyote, lakini awe na uzoefu usio na shaka katika masuala ya ununuzi wa umma.

Bei ya soko
Katika Kifungu cha Tisa cha Sheria hiyo sehemu (o) imeitaka ofisi ya umma, wizara au taasisi ya umma, kila taasisi imetakiwa kuwa na taarifa ya bei ya soko ya bidhaa na huduma inayotumika mara kwa mara na ofisi husika kutoka katika ofisi husika ya umma ili kuhakikisha bei ya bidhaa na huduma zitakazonunuliwa, zinalingana na za soko.

Katika kuhakikisha ofisi za umma zinanunua bidhaa bora kwa bei ya soko, ununuzi wa umma umetakiwa kwa mujibu wa muswada huo, kufanyika kwa kuzingatia uaminifu wa hali ya juu, ushindani, uwajibikaji, kuzingatia kupunguza gharama, ufanisi, uwazi na kupata thamani ya fedha iliyotumika.

Aidha, ili kupata bei iliyo chini ya soko bila kuathiri ubora wa bidhaa au huduma, ofisi husika kwa nia ya kupata thamani ya fedha na ubora wa juu, imetakiwa kufanya ununuzi wa bidhaa na huduma mahususi moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji, au kiwandani, mwakilishi wa mtengenezaji au wa kiwanda, muuzaji wa jumla au mtoa huduma.

Wawekezaji wa ndani
Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka pale kampuni au taasisi ya umma inapolazimika kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya nchi, ofisi hiyo ya serikali inalazimika kuhakikisha kuna wataalamu wa ndani ya nchi.

Ushiriki huo wa wataalamu na kampuni za ndani katika shughuli za ushauri kutoka nje ya nchi, sheria hiyo imependekeza kuwa, kampuni yoyote ya ushauri ya nje ya nchi, inapoomba kazi katika kazi zinazogharimiwa na fedha za umma, lazima ishirikiane na kampuni, mshauri wa Kitanzania kwa asilimia mpaka 15.

Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe zabuni katika shughuli ambazo zinagharimiwa na fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia 60 ni Watanzania.

Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi Watanzania, kampuni husika lazima ieleze kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi, ambazo itazinunua katika utekelezaji wa shughuli zake.

Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa katika Bunge hili, ili kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, ambazo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017, asilimia 40 ya trilioni 29.53, imepelekwa katika miradi ya maendeleo.

0 comments:

Post a Comment

TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU