ONYO
limetolewa kwa vyama vya siasa vinavyojaribu kusuguana na Jeshi la
Polisi kukumbuka kuwa hilo ni jeshi, ambalo liko tayari kutumia nguvu na
rasilimali zote, kuhakikisha raia na mali zao ni salama.
Jeshi
hilo pia limesema halihitaji msaada wowote kutoka kwa vyama vya siasa
na wakihitaji msaada, wataomba kutoka katika vyombo vingine vya
kiusalama.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Kaimu Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo,
Nsato Mssanzya, baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Bavicha), kudai kuandaa vijana kwenda Dodoma kusaidia polisi
kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu.
“Nawaasa
vijana, watoto msisuguane na jeshi, si busara kusuguana na jeshi,
fanyeni mambo ambayo nchi itakuwa salama, polisi itatumia nguvu zote
pamoja na rasilimali tulizonazo kuhakikisha raia na mali zao wanabaki
salama.
“Hakuna suala la kusaidia Jeshi la Polisi au nini, sisi tunajitosheleza wenyewe, kama tutahitaji msaada wowote katika ulinzi basi msaada huo tutauomba kwa vyombo vingine vya ulinzi, ambavyo vina mafunzo kama sisi na si kwa vyama vya siasa,” alionya.
“Hakuna suala la kusaidia Jeshi la Polisi au nini, sisi tunajitosheleza wenyewe, kama tutahitaji msaada wowote katika ulinzi basi msaada huo tutauomba kwa vyombo vingine vya ulinzi, ambavyo vina mafunzo kama sisi na si kwa vyama vya siasa,” alionya.
Alisema
anatumia neno ‘ole’ kwa watu watakaojaribu kuvuruga amani kwa madai ya
kusaidia kuzuia mkutano, kwamba polisi haitasita kuchukua hatua.
Alifafanua
kuwa Jeshi la Polisi halijazuia mikutano yote ya kisiasa na kwamba
limelazimika kutoa ufafanuzi, kutokana na kuibuka kwa tafsiri tofauti
kutoka kwa vyama vya siasa na makundi ya watu, baada ya polisi kutoa
tamko Juni 7 mwaka huu la kupigwa marufuku mikutano ya hadhara.
Mssanzya
alisema hakuna sehemu yoyote tamko hilo lilipiga marufuku mikutano ya
kiutendaji na kiutawala ya vyama vya siasa iliyofanywa kwa mujibu wa
kanuni za vyama husika.
“Ndio
maana baada ya tamko lile, baadhi ya vyama vimefanya na kupanga kufanya
mikutano ya kiutendaji na kiutawala bila kuingiliwa au kuzuiwa na Jeshi
la Polisi,” alisema Mssanzya akitolea mfano mkutano wa Bavicha kuzungumza na vyombo vya habari Julai 3, mwaka huu.
Alisema
shughuli ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Chadema (Chaso)
iliyopanga kufanyika Dodoma na ule wa chama cha ACT Wazalendo,
ilizuiliwa kwa sababu ujumbe uliolengwa katika shughuli hizo, ulikuwa wa
uchochezi na haikuwa mikutano ya kiutendaji au kiutawala.
Hata
hivyo alisema pamoja na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano
hiyo ya ndani, bado jeshi hilo lina mamlaka ya kuzuia pale
itakapobainika ina lengo la kuhamasisha uchochezi au kuharibu amani na
utulivu.
Alitoa
mwito kwa wananchi wote na vyama vya siasa, kuheshimu sheria za nchi na
kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuhakikisha usalama wa raia na
mali zake unaendelea kuimarika.