RAIS
mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema yuko tayari kuitumikia
Afrika kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika katika Umoja wa
Afrika (AU), ikiwa atapewa majukumu hayo.
Alisema akiteuliwa kushika nafasi hiyo atakubali, lakini hawezi kuiomba kwa kuandika barua.
Alisema
hayo jana Dar es Salaam alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu
kutajwa kwa jina lake kwamba ana nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo
katika uteuzi utakaofanywa siku chache zijazo ili kumrithi Mwenyekiti wa
sasa, Nkosazana-Dlamini Zuma wa Afrika Kusini.
“Inawezekana
mtu alikaa mahali akasema hawa ndio watatu wanaweza kutufaa, lakini
mimi siwezi kuandika barua kuomba kazi yoyote,” alisema.
Mwanadiplomasia
huyo maarufu alisema amefanya kazi kubwa kuliko zote ambazo binadamu
anaweza kufanya ambayo ni kazi ya kuwa Rais wa nchi yake, hivyo
hakusudii tena kuandika barua ya kuomba kazi. Alisema kama viongozi wa
Afrika wakiamini kuwa anaweza kushika nafasi hiyo na kuongoza, yuko
tayari kujitolea kama kiongozi wa Afrika, lakini si kuiomba.
Alisema, “Ili
kuwa Mwenyekiti lazima uombe, mimi si mgombea na waliogombea wapo. Watu
wananiombea heri, In Shaa Allah, lakini haliwezekani kwa sababu
sijaomba.”
“Naandika
barua na nani anaomba na mwingine anaomba, hapana jamani si vizuri.
Wakiridhika viongozi wa Afrika wakasema hapa tunakuomba utusaidie
ntafanya siwezi kuipa Afrika kisogo,” Kikwete alisema.
Katika
tukio jingine, Kikwete alizitaka nchi za Afrika zinazoingia katika
mapinduzi ya viwanda kuzingatia athari za tabia nchi zenye madhara
makubwa.
Alitoa
rai hiyo alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa watafiti na
wataalamu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi duniani, unaojadili
namna ya kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema
nchi isipopanga maendeleo yake vizuri itafika mahali mazingira
yataharibika na kuwa na madhara makubwa, hivyo ni wajibu wa nchi zote
duniani kulishughulikia.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alimtaja
Kikwete kuwa shujaa aliye mtari wa mbele kupambana na tatizo hilo la
athari za tabia nchi.