Mwenyekiti
wa Bodi ya Taifa ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema
amemmwagia sifa Rais John Magufuli huku akiwataka Watanzania kumpa siku
100 aonyeshe mabadiliko katika magereza nchini.
Mrema aliyasema hayo jana alipohojiwa katika kipindi cha Amka Tuongee kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star tv.
“Ni
Rais mzuri tuliyempata, ni mchapa kazi, tumpe muda kwa sababu ndiyo
kwanza ana miezi minane, lakini ni mchapa kazi kiasi kwamba marais
wenzake wanatembea yeye anakimbia,” alisema.
Julai
16, Rais Magufuli alimteua Mrema ambaye ni Mwenyekiti TLP baada ya
kumkumbusha ahadi aliyompa wakati wa kampeni eneo la Himo Kilimanjaro
kuwa wasipomchagua kuwa Mbunge wa Vunjo atampatia kazi.
“Nina
uhakika nitafanikiwa kwa sababu nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
nilifanya mambo makubwa hadi nikapewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu,” alisema.