Naibu
Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amesema hoja ya wabunge wa Ukawa kutaka
aenguliwe kwenye wadhifa huo inafanyiwa kazi na Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge ambayo iwapo itaridhia, itarejeshwa bungeni
kupigiwa kura ambazo hata hivyo, hazitatosha kwa uchache wao.
Dk Tulia alisema hayo jana wakati akihojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam TV.
“Hoja
ikishakuja bungeni hapo sasa huwa ni kampeni na baadaye kupigiwa kura.
Kwa kuwa waliopeleka hoja ni wabunge wa upinzani, hivyo wanatakiwa
kufikisha idadi fulani ambayo kiuhalisia wao kwa sasa hawana,” alisema.
Kwa
karibu mwezi mzima kwenye Bunge la Bajeti, wabunge wa Ukawa walimsusia
Dk Tulia na walikuwa wakitoka bungeni kila alipoingia, tayari
wameanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani kwa madai kuwa hawatendei
haki na anaminya demokrasia ndani ya Bunge.
Dk
Tulia alisema Katiba inatambua kwamba kiongozi aliyechaguliwa anaweza
kuondolewa madarakani na wale waliomchagua, hivyo wabunge wa upinzani
wametumia haki yao ya msingi na kinachosubiriwa ni hoja yao kufanyiwa
kazi.
“Kanuni
imeweka wazi na msingi ule umejengwa kwenye Katiba kwa sababu inatambua
wale waliomchagua kiongozi wasiporidhika naye wanaweza kumuondoa
madarakani. Nafarijika kuona wanachukua hatua, hivyo mimi sina malumbano
nao,” alisema.
Hakuna maridhiano
Dk
Tulia alisema hakuna maridhiano yanayotakiwa baina yake na wabunge wa
Ukawa kwa kuwa hana malumbano nao, bali kanuni na taratibu zinafuatwa
kufanikisha hoja yao ya kumuondoa madarakani.
Naibu Spika huyo alisema maridhiano huwapo baina ya watu wanaolumbana na kwamba, baina yao hakutakuwa na suala hilo.