MPIGACHAPA
Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo amekiri kuwepo kwa nyaraka bandia
za serikali katika sekta mbalimbali, nyingi zikiwa za ukusanyaji wa
mapato ya serikali, vyeti vya kitaaluma, ndoa na nyinginezo.
Kutokana
na hali hiyo, amewaasa wananchi wanaofanya shughuli hizo za kutengeneza
nyaraka hizo bandia ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi, kuacha kwani
wanaendesha oparesheni ya kudumu itakayowabaini na kuchukuliwa hatua
kali, ikiwemo kifungo cha miaka 20 jela.
Hivyo
amewataka watendaji na wasimamizi katika idara mbalimbali kufanya
uhakiki upya wa nyaraka za serikali, kwani zimezagaa sehemu mbalimbali
nchini hususan katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyuoni na katika
maeneo ya kazi.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Mpigachapa Mkuu Chibogoyo alisema nyaraka hizo
bandia ni pamoja na stakabadhi za malipo, vibali mbalimbali, hati za
makontena, leseni za magari pamoja na bima.
Alisema
katika oparesheni iliyofanyika mwaka jana ya ‘Okoa Pato la Taifa‘
katika kutafuta nyaraka bandia za serikali, walibaini kuwepo kwa nyaraka
za vyeti vya ukaazi au kuzaliwa vinavyomilikiwa na raia wa kigeni,
stakabadhi za mapato, leseni za biashara, vyeti bandia vya kitaaluma na
vinginevyo.
Alisema
nyaraka hizo walizikuta katika vituo vyao vya mauzo na wengine kwenye
nyumba zao za kutengenezea uhalifu huo na kubaini kuwa uhalifu huo ni
zaidi ya ujambazi kutokana na madhara yake kwa nchi.
Alisema
katika oparesheni hiyo walibaini kiwanda cha kutengeneza bidhaa hizo
maeneo ya Buguruni katika Manispaa ya llala, Dar es Salaam pamoja na
vyeti feki vya Chuo Kikuu cha Kampala (KIU), vitambulisho vya ukaazi
ambako kuna raia wa kigeni amepewa cha ukazi akiishi Kariakoo, risiti za
usalama barabarani pamoja na shahada za ndoa za Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Maria Magomeni jijini Dar es Salaam.
Alisema
pia walikamata boksi tatu za stika za bima zinazowekwa kwenye magari
zikiwa tayari kusafirishwa kwenda mkoani Tanga zikiwa zimewekwa kwenye
jokofu bovu lililochakaa karibu na mama ntilie katika maeneo ya
Salamander.
“Wananchi
wasio waaminifu wanaotaka kupoteza maisha ya wananchi wema na usalama
wa nchi ikiwemo kurudisha nyuma maendeleo na uchumi wa nchi, nawapa
salamu zangu kuwa mimi na timu yangu tumejipanga kutokomeza vitendo
hivyo na tutapigania nchi,” alisema Chibogoyo.
Alieleza
kuwa makatazo ya udhibiti wa nyaraka yapo katika Sheria ya Makosa ya
Jinai, Sheria ya Ngao ya Taifa, Sheria ya Ushahidi na Sheria ya Usalama
wa Taifa, hivyo ukikamatwa na katatasi inayokusudia kutumika kwa
udanganyifu, adhabu ni kufungwa miaka saba.
Aidha,
alifafanua kuwa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 inakataza kuwa
na nyaraka, mihuri, karatasi maalumu na kumiliki taarifa za serikali
isivyo halali na sheria inasema kuwa ni mhalifu na adhabu yake ni miaka
20 jela.
Chibogoyo
aliwataka wananchi wema kutoa taarifa pale wanapowabaini watu hao
wanaotengeneza nyaraka bandia za serikali pale wanapohitaji nyaraka hizo
kwa haraka na ofisi yake itampatia nyaraka halali kwa haraka.
Akizungumzia
nyaraka hizo bandia za serikali, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema hali ya nyaraka hizo inatisha kwani
ni kubwa kwani nyaraka hizo zote muhimu zipo na zinatumika katika
maeneo mbalimbali.
Kamanda
Sirro alisema kuna watu wamenufaika kwa nyaraka hizo kama vyeti
kutumika kupata ajira hivyo watafuatilia na watawachukulia hata za
kisheria wanufaika wote wa nyaraka hizo bandia.
Alisema
katika oparesheni waliyoshirikiana na Mpigachapa Mkuu wa Serikali
walikamata watu watatu ambao inaonekaan ndiyo mabosi au wakurugenzi wa
kutengeneza nyaraka hizo huku wakiwa na mawakala wao katika mikoa
mbalimbali kama Mwanza na kwingineko.
Alisema wataendelea kufanya oparesheni ili kuhakikisha suala hilo linakoma kwa kuwakamata wahusika wote.