WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka
mikakati endelevu ya kuwawezesha wananchi kuvua katika maji ya kina
kirefu cha bahari kwa kutumia meli kubwa na za kisasa ili Taifa liweze
kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imekuwa ikichukuliwa na wavuvi wenye
vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.
Aidha,
amezitaka halmashauri zote nchini ziweke mikakati na mipango ya
kuifanya mito na maziwa mbalimbali nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa
kufuatilia kwa karibu shughuli za wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua
kinyume na sheria.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua
maadhimisho ya 23 ya sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki
katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa
Morogoro ambapo amesema bado nchi haijaweza kutumia rasilimali hiyo
kikamilifu.
Amesema
halmashauri zinatakiwa zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha
miradi ya kufuga samaki katika maeneo yao na wewezeshwe kupata
teknolojia ya ufugaji huo.
Akizungumzia
vikundi vya wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa
alishauri waelimishwe kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana
bora za kisasa za uvuvi ili shughuli zao ziwe na tija.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amesema wakulima wanatakiwa kuzingatia
matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya zana za
kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa na wataalam ili
kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.
Akizungumzia
kuhusu suala la usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda
mbalimbali alipata fursa ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na
wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.
Amesema
amefurahi kuona wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao,
pembejeo na zana za kilimo wana ari kubwa ya kushiriki katika kuleta
mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali
ya kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza uchumi wa
viwanda.
“Naamini
kuwa pamoja na lengo la kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji
na wavuvi wataongeza ari ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma
na binafsi katika kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani
ya mazao,” alisema.
Kufuatia
hatua hiyo Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote kuhamasisha
uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya
kilimo, mifugo na uvuvi kwa kushirikisha taasisi za umma na binafsi,
mashirika na vikundi vya ujasiriamali katika maeneo yao.
Akizungumzia
namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya
wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi
watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye
mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda na maeneo ya vipando vya
mazao mbali mbali yaliyoko katika viwanja hivyo ambapo alisema
ameridhishwa na juhudi zilizofanyika katika maandalizi ya maonesho ya
mwaka huu ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa uwanja huo.
“Napenda
kutoa pongezi za dhati kwa kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za
kufanyia maonesho. Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu,
Mashirika yetu ya Umma na binafsi; na watu binafsi ambao wamejenga na
wanaendelea kujenga majengo mazuri na ya kudumu,” alisema.
Pia
alizindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na kusema kuwa
uboreshaji wa viwanja hivyo unaonesha jinsi wadau wote katika sekta ya
kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika wanavyotambua umuhimu wa maonesho hayo
kama njia ya kuongeza maarifa na kumuenzi mkulima, mfugaji na mvuvi kwa
kutambua mchango wao katika uchumi wa Taifa.
Kauli
mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni kilimo, mifugo na uvuvi ni
nguzo ya maendeleo: vijana shiriki kikamilifu (“HAPA KAZI TU”)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 01, 2016.