Serikali
imeifunga Shule ya Sekondari ya Lyamungo iliyoko Hai mkoani
Kilimanjaro, baada ya wanafunzi wake kuzusha vurugu kubwa huku wakivamia
na kuivunja ofisi ya Makamu Mkuu wa shule hiyo.
Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu, alithibitisha jana kuifunga
sekondari hiyo ya kitaifa kuanzia Machi Mosi hadi Machi 17, mwaka huu.
Shule hiyo ya kitaifa hupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita kutoka mikoa mbalimbali nchini.
"Ni
kweli nimeifunga hiyo shule kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na sababu
za kiusalama. kulikuwa na uchaguzi wa serikali ya wanafunzi na wakati
unafanyika mwanafunzi mmoja aliandika matusi makubwa akiwatukana walimu.
"Baada
ya kufanyika uchunguzi aligundulika huyo mwanafunzi na hapo ndiko
walipoandaa vurugu hizo na kujielekeza kuharibu mali na kusababisha
hasara ambayo bado haijafahamika," alisema Buswelu.
Kwa
mujibu wa Buswelu, vurugu hizo ziliibuka baada ya mwanafunzi huyo (jina
limehifadhiwa) kupewa barua ya kufukuzwa shule kutokana na vitendo vya
utovu wa nidhamu.
Buswelu
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Siha ameagiza Bodi ya shule hiyo
kukutana kesho (leo) kufanya tathmini ya hali ya uharibifu na madhara
yaliyojitokeza na kuiarifu serikali.
Mpaka sasa, hakuna mwanafunzi anayeshikiliwa kwa kufanya vurugu na kusababisha hasara ya mali na rasilimali za serikali.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi Hamisi Issah, alisema wanafunzi hao walifanya tukio hilo saa
4:30 asiku juzi.
"Hao
wanafunzi wameharibu ofisi ya mwalimu huyo ambaye pia ni mwalimu wa
nidhamu kwa kuvunja paa la juu, milango, madirisha na samani za ndani,"
alisema Kamanda Issah.
0 comments:
Post a Comment