Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe
SIFA anazomwagiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk
Harrison George Mwakyembe mitaani, zinatosha kusema kuwa waziri huyo ni
noma katika uchapakazi wake.
Dawati la Ijumaa ambalo kila siku halipoi kusaka habari ziliokwenda
shule limebaini kuwa Dk Mwakyembe amekuwa kiongozi anayetajwa na
wananchi wengi hasa wasanii kuwa anamudu kuingoza wizara iliyo chini
yake.
Ukaribu wake na wasanii wa muziki wa ladha tofauti, ufuatiliaji wa
masuala ya michezo ukiwemo mpira wa miguu, ngumi, riadha na usimamiaji
wa haki za wasanii kwa jumla ni miongoni mwa mambo yanayompandisha chati
waziri huyo.
HABARI ILIYOBAMBA
Hivi karibuni, Dk Mwakyembe, akiwa bungeni jijini Dodoma, aliliamsha
dude kwa kuahidi kufuatilia kwa kina mikataba yote isiyokuwa na tija kwa
wasanii ambayo hatimaye huyaacha maisha yao kwenye ufukara.
Ahadi ya ufuatiliaji huo wa mikataba feki ilichochewa na waziri huyo
kuguswa na hali ya ugonjwa na changamoto za kimatibabu zinazomkabili
mwigizaji mkongwe nchini, Amri Athuman ‘Mzee Mjuto’ ambaye kwa sasa yuko
nchini India kwa matibabu.
“Leo hii Mzee Majuto anaumwa, anaomba pesa, ninachanga pesa kutoka
mfukoni kwangu, lakini leo hii nusu ya mabango ya biashara, matangazo ya
biashara kwenye TV ni Majuto, ninaomba sasa nitumie nafasi hii kusema
nimeunda kamati ya wanasheria, tunaanza na kesi ya Majuto. Mashirika
yote, kampuni zote zilizoingia mkataba na Majuto, tutapitia hiyo
mikataba, kama ameonewa lazima ilipwe familia yake…tumechoka.
“Tukishamaliza na Majuto tunarudi na kwa Kanumba (marehemu Steven
Kanumba) na msanii yeyote ambaye anaona ameingia mkataba wa kipumbavu,
aje tuone. Mheshimiwa mwenyekiti inaudhi, lakini ndiyo hivyo.
“Leo hii Mzee Majuto yuko hospitalini, amekosa shilingi laki tano,
nimtumie mimi wakati waziri pesa yenyewe ndiyo hiyo mnaelewa, eeh…maisha
siyo…”
IJUMAA NA DK MWAKYEMBE KATIKA MAZUNGUMZO
Baada ya tamko hilo la waziri huyo anayetaka kuuvunja mfupa uliowashinda
mawaziri wenzake wengi wa kuwafanya wasanii wa Kibongo nao kula bata
kupitia kazi zao za sanaa, gazeti hili lilizungumza katika mahojiano
maalum na kutaka kujua amefikia wapi katika kushughulikia mikataba au
naye amepoa?
Fasta bila kuchelewa, waziri huyo alipokea simu yake ya mkononi
iliyopigwa na Mwandishi Wetu saa 7: 24 mchana wa Mei 9, mwaka huu na
hapo ndipo alipofungua kabrasha la taarifa kamili juu ya kauli yake
hiyo.
MSIKIE DK MWAKYEMBE
“Zoezi limeshaanza, kwa sababu suala la mikataba linahitaji umakini,
weledi na kusimamia haki, nimeshaunda timu ya wanasheria watano ambao
wanapitia hiyo mikataba.
“Lakini kwa sababu suala lenyewe ninahitaji liende haraka, ninakusudia
kuongeza wanasheria wengine wanne ili wafikie tisa, lakini kwa sasa hao
watano wameshaanza kuchambua baadhi ya mikataba inayolalamikiwa na
wasanii wetu.
“Ninachoweza kukuambia ndugu yangu ni kwamba, katika hiyo mikataba
tuliyopokea, tayari kuna mingine imeshachambuliwa na atumefikia hadi
hatua za kuwakutanisha walalamikaji na wanaolalamikiwa, kwa hiyo zoezi
linakwenda vizuri,” alisema Dk Mwakyembe wakati akijibu baadhi ya
maswali aliyoulizwa na Mwandishi Wetu.
ATOA WITO KWA WASANII
Aidha, Waziri Mwakyembe, mbali na kueleza kuwa atajitokeza hadharani
hivi karibuni kuwaambia wananchi kile atakachovuna katika kazi yake hiyo
aliyoianza amewataka wadau wa sanaa wenye mikataba yenye shaka
wajitokeze ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.
Wito huo ulitolewa na waziri huyo baada ya gazeti hili kutaka kujua
wizara yake iko ‘siriaz’ na mikataba ya Kanumba na Majuto peke yake au
na wasanii wengine wanaweza kujiunga katika msafara huo aliouanzisha wa
kuuangamizi unyonyaji.
MITAANI KWA WASANII KUKOJE?
Baada ya waziri kuliamsha dude, gazeti hili lilipita katika ulimwengu wa
sanaa na kuwaangalia wasanii wenyewe wameipokeaje hatua hiyo ya waziri
ambapo ilibainika kuwepo kwa vicheko na nderemo.
Mama mzazi wa msanii maarufu aliyega dunia miaka sita iliyopita, Steven
Kanumba aitwaye Flora Mtegoa ni miongoni mwa watu waliofurahia hatua
hiyo ya waziri.
“Mwanangu amefariki dunia, ameacha mikataba mingi kwenye makampuni,
lakini hakuna nilichopata, kuna siku nilikwenda kwenye kampuni (anaitaja
lakini tunahifadhi jina) kuulizia, nilipofika waliniambia Kanumba
alishakufa na mikataba yake ilishakufa pia.
“Yaani sijui nikuambie nini, nimefurahi kusikia waziri anatafuta haki za
mwanangu, najua kwa sasa yuko bungeni, akitoka huko nitakwenda
kumuona,” alisema mama Kanumba.
Mbali na mama Kanumba, mwingine ambaye Ijumaa lilinasa habari za
kulalamikia mkataba feki ni Wastara Juma ambaye mara kadhaa amekuwa
akijitokeza na kudai kudhulumiwa kiasi cha shilingi milioni 80 na
Kampuni ya KZG ya China.
Wastara anadai kuwa, KZG ilimpa mkataba wa kuwa balozi wa bidhaa za simu
ya mkononi kwa makubaliano ya kiasi hicho cha fedha, lakini baadaye
kampuni hiyo ilitimka nchini na kurejea China huku ikimwacha Wastara
akilia.
WANASHERIA WAFUKUA UTAJIRI WA KANUMBA, MAJUTO
Habari za chini ya kapeti zilizonaswa na gazeti hili zilidai kuwa, timu
hiyo ya wanasheria walioteuliwa na Waziri Mwakyembe wameshaanza kufukua
mikataba yote ya Kanumba na Majuto na endapo hali ikiwa upande wa
wasanii hao, huenda utajiri ukawatembelea licha ya Kanumba kutokuwepo
duniani na Majuto kuwa hospitalini huko India.
Kwa miaka kadhaa, kumekuwepo na kesi mbalimbali za wasanii wa Bongo
kudhulumiwa haki zao, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuanza kupatiwa
tiba na huenda likawatajirisha wasanii wengi.
TUPEKUE KIDOGO HABARI HII
Pamoja na nia njema ya waziri ya kuwasaidia wasanii kupata haki katika
mikataba feki, Timu ya Ijumaa inaungana na Waziri Mwakyembe na kumshauri
kuwa jambo hilo linahitaji umakini mkubwa kulishughulikia kutokana na
aina, maisha na uelewa wa wasanii wengi hapa nchini.
Kutokana na uzoefu na kuishi karibu na wasanii wa Bongo, gazeti hili
limebaini kuwa maisha ya ‘njaanjaa za kujiendekeza’ yamekuwa
yakisababisha baadhi ya wasanii kuingia mikataba feki ili kujipatia
fedha hata kiduchu za kufanyia matanuzi mjini angalau kwa siku moja.
Kwa msingi huo, gazeti hili linawataka wasanii wa Bongo kutambua hadhi
yao, kujielimisha kuhusu mikataba, kuacha tabia za kuingia mikataba kwa
lengo la kukidhi shida ya siku moja.
Thursday, May 17, 2018
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU
0 comments:
Post a Comment