Kitendo
cha nyaraka za makontena 20 yenye samani yaliyo katika hatari ya
kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato (TRA) mwezi ujao kuwa na jina la mtu
binafsi Paul Makonda,ni moja ya sababu zilizomkwamisha Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam kusamehewa ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la
thamani (VAT) kama alivyoomba, imefahamika.
Kwa
mujibu wa barua ya Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango kwa 'RC'
Makonda ya Machi 24, mwaka huu kwa mujibu wa sheria, shehena hiyo ya
samani haistahili kupata msamaha wa ushuru wa forodha au bidhaa na kodi
ya ongezeko la thamani (VAT) kwa sababu kadhaa ikiwamo kuonekana kuwa
mali ya mtu binafsi.
Makonda
aliiandikia wizara barua Januari 3, mwaka huu akiomba msamaha wa kodi
kwenye samani za shule za Mkoa wa Dar es Salaam zenye thamani ya
"takribani" Sh. bilioni 1.4 ambazo alidai ni msaada kutoka kwa wananchi
wapenda maendeleo waishio Marekani.
Ombi
hilo hata hivyo limekataliwa na Waziri Mpango kwa kuzingatia Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na Sheria ya Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014.
Barua
ya Dk. Mpango inasema kwa mujibu wa Sheria ya VAT, msamaha kwa taasisi
za Serikali ni kwa shughuli zisizo za kibiashara, "kwa masharti kwamba
usiwepo uwezekano wa shughuli kama hiyo kutolewa na taasisi isiyo ya
kiserikali".
Kwa
mujibu wa barua hiyo ya Wizara ya Fedha, samani kama hizo zinaweza
kutolewa na taasisi isiyo ya kiserikali au mtu binafsi hivyo kuwa nje ya
eneo la msamaha.
Aidha,
Makonda amekataliwa msamaha wa kodi kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa siyo
asasi ya kiraia au taasisi ya kidini, barua hiyo inasema na kufafanua:
"Magazeti
ya Serikali namba 205 na 206 ya mwaka 2016 yanatoa misamaha ya ushuru
wa forodha na wa bidhaa kwa asasi za kiraia na taasisi za dini kwa vifaa
vitakavyotumika kwa ajili ya kuendeleza, kuanzisha au kukarabati miradi
inayolenga elimu, usambazaji maji, huduma za afya na miundombinu."
Viti, meza na mbao za darasani vinavyodaiwa kuwamo katika mzigo wa Makonda vinaonekana kuangukia nje ya jedwali hilo.
Mbali
na majibu kwa Makonda, nakala ya barua ya Waziri Dk. Mpango imepelekwa
pia Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Tamisemi, Wizara ya Fedha na TRA.
Alipoulizwa
jana kwa njia ya simu kama Makonda alipokea barua hiyo, Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano kwa Umma wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwipaja
hakuweza kuthibitisha.
Lakini alionyesha kushangazwa kwake kusikia "barua iliyonakiliwa kwa Waziri Mkuu ipo mitandaoni?"
Mwanzoni
mwa wiki iliyopita TRA ilitangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za
Makonda ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku
30 zitakazomalizika katikati ya mwezi ujao.
Katika
tangazo hilo, Kamishna wa Idara ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa,
alitoa siku 30 kwa wamiliki wa mali mbalimbali zilizopo katika ghala la
TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya muda huo zitapigwa mnada kwa
mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa forodha.
Credit: Nipashe
0 comments:
Post a Comment