SERIKALI
imeagiza wote waliotengeneza watumishi hewa wafunguliwe mashitaka
mahakamani huku ikionya kuwa iko tayari kusimamisha kazi maofisa
utumishi wote nchi nzima wanaofikia 1,500 katika sakata hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo jana alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
Amesema
tayari serikali imeshatoa agizo hilo la kuwashitaki maofisa wote
waliotengeneza watumishi hewa na ikibidi iko tayari kuwasimamisha kazi
maofisa utumishi 1,500 waliofundishwa kazi hiyo na serikali.
Kwa
mujibu wa Waziri Kairuki, mpaka mwishoni mwa Mei, serikali ilikuwa
imebaini uwepo wa watumishi hewa 12, 246 waliokuwa wakitafuna Sh bilioni
25.06 kila mwezi.
Katika
kuelezea athari za ufujaji huo wa fedha za serikali, Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema hata katika ulipaji wa madeni
ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais John Magufuli aliagiza uhakiki
ufanyike, kabla ya kulipa kwa kuwa penye wafanyakazi hewa, kuna malipo
hewa ya wastaafu.
Alitoa
mfano wa deni la Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Serikali ilikuwa ikidaiwa
Sh trilioni 2.67 lakini uhakiki wa deni hilo ulipofanyika, deni hilo
likabainika ni Sh trilioni 2.04, hatua iliyosaidia Serikali kuepusha
wizi wa karibu Sh bilioni 600 za wastaafu hewa.
January na uthubutu
Naye
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano),
January Makamba alizungumzia ahadi ya Rais ya kutoa Sh milioni 50 kila
kijiji na kufafanua kuwa Sh bilioni 59 zilizotengwa, zitatumika
kujifunza namna ya kutekeleza ahadi hiyo.
Aliwataka
wabunge wa CCM kukumbuka kuwa chama hicho kilipomtangaza Dk Magufuli
kuwa ndiye mgombea urais, kilitoa taarifa duniani ya aina ya Serikali,
uongozi na mabadiliko wanayotaka Watanzania.
Alisema
mabadiliko ya kweli hayawezi kutokea bila kuwepo kwa hatua kubwa na
uthubutu ndio maana serikali imethubutu kuwa na Bajeti ya Sh trilioni
29.5 na uthubutu wa kutenga asilimia 40 ya bajeti hiyo katika maendeleo.
Kwa
mujibu wa January, mahali popote kwenye uthubutu, lazima kutakuwa na
watu watakaotia shaka na kuwataka wabunge wa CCM wasitilie shaka uwezo
wa serikali katika kukusanya Sh trilioni 29.5 zilizokusudiwa.
Alisema
wabunge wa CCM ndio wengi katika Bunge na Ilani ya Uchaguzi
inayotekelezwa ni ya chama hicho, hivyo ni muhimu wamuunge mkono Rais
Magufuli kwani akifanikiwa Rais na Tanzania imefanikiwa.
Alikumbusha
kuwa maendeleo yanahitaji kujitoa sadaka na viongozi wao wamekubali
kujitoa sadaka, hivyo wabunge, wafanyabiashara mpaka wadogo wakiwemo
bodaboda, wajitoe sadaka kwa kulipa kodi.
Alitumia
kauli ya Rais John Kennedy wa Marekani aliyoitoa miaka ya mwanzo ya
1960, alipowataka wananchi wa nchi hiyo, kutouliza nchi hiyo itawafanyia
nini, bali wajihoji wao wataifanyia nini nchi yao.
Watanzania wanune
Naye
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alieleza
namna Serikali ya China ilivyoridhia kutoa Sh trilioni tano nje ya
Bajeti ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwa sekta binafsi,
huku ikiahidi kutoa fedha nyingine Dola za Marekani milioni 100 kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
Alihitimisha
kwa kusema ujenzi wa uchumi wa viwanda ni sawa na vita na wakati wa
vita, hakuna anayecheka hivyo Watanzania wote lazima wanune, ili
kutimiza malengo ya kuongeza pato la jumla la taifa.
Aidha,
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema pato la
jumla la Taifa kwa sasa ni Dola za Marekani bilioni 55 na ili Tanzania
ifike katika uchumi wa kati, inatakiwa kuongeza uzalishaji utakaoongeza
pato la jumla la Taifa kuwa Dola za Marekani bilioni 200.
Alisema
injini za kupeleka uzalishaji na uchumi katika kipato hicho, ziko
nyingi na mojawapo ni sekta ya nishati ya umeme ambayo katika bajeti
hiyo ya serikali, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh trilioni
1.43 ambapo asilimia 94 ya hizo ni za maendeleo na kati ya fedha hizo za
maendeleo, asilimia 95 inakwenda kwenye umeme.
Katika
kudhihirisha nia ya serikali katika sekta hiyo, Profesa Muhongo alisema
katika bajeti inayomaliza muda wake, wizara hiyo imeshapata asilimia 80
ya fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu unaoisha huku Wakala
wa Umeme Vijijini (Rea) ikiwa imeshapata asilimia 80 ya fedha
iliyotarajia.
Aliwaeleza wabunge kuwa katika bajeti waliyopitisha, usambazaji wa umeme vijijini umepangiwa Sh bilioni 534.