VIGOGO
wakiwamo wabunge na wananchi wengine, walionunua nyumba za serikali na
kutomaliza kulipa madeni yao kwa wakati kama mikataba yao inavyoelekeza,
wameanza kuondolewa kwa nguvu kwenye nyumba hizo na nyumba kupigwa
mnada ili kupata fedha za kulipa madeni ya Sh bilioni sita.
Madeni hayo serikali inadai kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart
ambayo imepewa kazi ya kukusanya madeni hayo ya TBA kutoka kwa wadaiwa
sugu hao, Scholastica Kevela alisema kazi ya kuwaondoa vigogo walionunua
nyumba hizo au kupangisha bila kulipa, inaanza leo jijini Dar es
Salaam.
Kevela
alisema katika kazi hiyo, TBA wamewapa orodha ya zaidi ya nyumba 3,000
nchi mzima za walionunua na wengine kupangisha nyumba za TBA ambao
wanadaiwa madeni na muda wa kurejesha ulishapita.
“Tuna
orodha za nyumba zaidi ya 3,000 nchi nzima, juzi tulianza Mwanza
tumeshikilia nyumba zaidi ya 20, kwa kuwatoa watu nje, na juzi Dodoma
tumefanya hivyo, tumeshashikilia nyumba 40 zikiwemo za vigogo, kesho
(leo), tunaanza zoezi hilo hapa Dar, hatutakuwa na huruma kwa mdaiwa,
wote tulishawapa taarifa za kimaandishi, kazi yetu ni utekelezaji tu,” alisema Kevela.
Alisema
wanatekeleza kazi waliyopewa kwa sababu hata Rais John Magufuli
anasisitiza wananchi kulipa kodi ili nchi iendelee na kuacha utegemezi,
hivyo wadaiwa sugu hao muda wa kulipa na hata muda wa ziada waliopewa
kuhakikisha wamemaliza madeni yao nao ulipita na wengi hawakulipa, hivyo
Yono inaingia kazini kupiga mnada nyumba hizo.
Alisema
walionunua nyumba za serikali na hawajamaliza kulipa madeni wakiwemo
wabunge, vigogo na wananchi wengine wanajitambua, hivyo kuanzia leo
wanapaswa kuondoka kwani zitauzwa ili kulipa deni la serikali.
Kadhalika
alisema waliopanga kwenye nyumba hizo na bado wanadaiwa kodi msako huo
unawahusu na kwamba wataondolewa wote na vitu vyao kupigwa mnada ili
kupata fedha za kulipa kodi wanayodaiwa na serikali.
“Sisi
tunatekeleza agizo kulingana na mkataba wetu na pia tunamsaidia Rais
kukusanya kodi, hivyo wote wanaodaiwa wafahamu tutawafuata walipo na
kupiga mnada mali zao ili kulipa kodi ya serikali,” alisema Kevela.
Hata
hivyo, alisema mchanganuo wa nyumba hizo na majina ya vigogo na wabunge
watatoa baadaye baada ya kufanya upembuzi kwa sababu nyumba za wadaiwa
ni nyingi.
Awali
akizungumzia madeni ya wakwepa kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA),
waliokwepa kulipia kontena zaidi ya 320 zilizogunduliwa na Rais
Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Yono Kevela alisema
wanaendelea kukusanya madeni ya wadaiwa hao.
Alisema
Yono imekamata mali za wadaiwa hao na baadhi zimeshapigwa mnada na
nyingine zinaendelea kuuzwa ili kupata fedha za kulipa kodi, na hadi
sasa takribani Sh bilioni saba zimeshalipwa kati ya Sh bilioni 18
zilizokuwa zinadaiwa.