JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema inaendelea na
upelelezi kuhusu tuhuma zinazomkabili Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT
Wazalendo, Kabwe Zitto ambaye ni Mbunge Kigoma Mjini na
watakapokamilisha atafikishwa Mahakamani.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema, sababu za kumhoji
Zitto ni kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa katika mkutano wake
wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Zakhem, Mbagala.
Alisema,
tayari Zitto ameshahojiwa katika kituo hicho mara mbili, lakini bado
jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kujiridhisha dhidi ya tuhuma
zinazomkabili.
Sirro
alisema jeshi hilo haliwezi kuruhusu siasa ambazo zinavunja amani,
hivyo ameendelea kuwataka wanasiasa kufuata taratibu na endapo
wamekataza kufanya mikutano basi watii.
“Kama
hakuna amani hakuna siasa hatuwezi na hatutakubali kuruhusu amani
tuliyonayo itoweke sababu ya wanasiasa lazima kutii ili kulinda amani
yetu,” alisema Sirro.
Hivi
karibuni Zitto alijisalimisha Kituo cha Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya
saa tatu baada ya kuandikiwa barua ya kuitwa kituoni na Mkuu wa
Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura.
Hatua
ya Zitto kuhojiwa ilitokana na maudhui ya hotuba yake aliyoitoa Juni 5,
mwaka huu kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika
viwanja vya Zakhem, Mbagala wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kutoka katika mahojiano hayo, Zitto alisema haoni kama
hotuba aliyoitoa ina tatizo lolote, kwani hotuba hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa majukumu ya kisiasa.
0 comments:
Post a Comment