Utaratibu
huu mpya na wa kwanza kutumiwa na tume hiyo, nchini ulianza kutekelezwa
jana baada ya gazeti la serikali la Habari Leo kuchapisha tangazo hilo,
likianisha sifa za kitaaluma na uzoefu zinazohitajika na uzoefu wa
waombaji na viambatanisho vya uthibitisho wa sifa hizo na uzoefu wa
kitaaluma vinavyohitaji.
Akizungumza
kuhusu utaratibu huo, Jaji Chande ambaye ndiye mwenyekiti wa tume hiyo
alisema wameamua kutumia utaratibu huo kuongeza uwazi, kupanua wigo na
kuongeza ushindani ili kuwapata majaji wenye sifa.
Hata
hivyo, Jaji Chande alisema utaratibu huo si kwamba ni mpya bali upo,
kwa kuwa ni miongoni mwa taratibu za tume hiyo katika hatua ya kwanza ya
upatikanaji wa majaji, yaani ya kupata orodha ya majina ya watu wenye
sifa za kuteuliwa kuwa majaji.
“Huu
ni utaratibu wa tume, upo kwenye tume na tumekuwa tukiuongea mara kwa
mara kwenye tume, lakini tulikuwa hatujautekeleza tu.
"Sasa safari hii tumeona ngoja tujaribu kupanua wigo kwa kutangaza,” alisema Jaji Chande.
Alifafanua
kwamba katika taratibu za tume hiyo kupata majina ya kuingia kwenye
mchakato wa kuteuliwa kuwa majaji kuna njia tatu ikiwamo ya tume yenyewe
kuwasaka.
Njia
nyingine ni kuziandikia taasisi za kisheria kama vile Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakuu wa vitivo vya sheria wa katika vyuo
vikuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili
kutoa mapendekezo ya majina ya watu wenye sifa hizo.
Pia, alisema njia nyingine ni utaratibu wa kuwapandisha watumishi wa ndani ya mahakama, kama vile mahakimu wakazi na wasajili.
“Lakini
pia, hili la kutangaza ni utaratibu wa nchi za Jumuiya ya Madola. Kuna
kanuni kwamba uteuzi wa majaji uwe wa wazi ili kuongeza ushindani na
ulenge uzoefu, umakini na ujuzi na uzingatie jinsia bila ubaguzi,” alisisitiza Jaji Chande.
Akizungumzia
uzoefu wa nchi nyingine katika utaratibu huu wa kutangaza nafasi hizo,
Jaji Chande alisema kuwa kuna nchi ambazo zimefanikiwa kuwapata majaji
wenye sifa, lakini pia kuna nyingine hazikufanikiwa.
Alitoa
mfano wa Kenya ambayo ilianza utaratibu huo kulingana na Katiba Mpya
pamoja na Uingereza, lakini akasema Botswana licha ya kutumia utaratibu
huo haikufanikiwa kuwapata watu wenye sifa kama ilivyokuwa ikitarajia.
Akizungumzia
uteuzi wa majaji, Jaji Chande alisema kuwa hupitia katika hatua tano
kabla ya hatua ya uteuzi wa mwisho ambao hufanywa na Rais.
Alizitaja
hatua hizo kuwa ni kwanza hatua ya kupendekeza majina, ambayo hufanywa
ama kwa watu kuomba au kupendekezwa na taasisi na mamlaka husika; hatua
ya uchambuzi wa sifa na mafanikio yao na hatua ya usaili.
Hatua
ya nne, Jaji Chande alisema ni kupendekeza au kuandaa orodha ndogo na
ya tano ni hatua ya uchunguzi ambayo hufanywa na vyombo mbalimbali vya
dola, kama vile Usalama wa Taifa na vinginevyo.
“Baada
ya hatua hizo, ndipo Rais hupelekewa orodha ya majina ya watu wenye
sifa na kufanya uteuzi kutoka miongoni mwa majina hayo kulingana na
idadi ya nafasi zilizopo. Kwa kila nafasi moja, yanatakiwa majina
angalau matatu kwa nafasi moja,” alifafanua.
Kutokana
na mchakato huo wa upatikanaji wa majaji, Jaji Chande alikanusha madai
ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa wakati mwingine
Rais huteua majaji wasio na sifa au ambao hawakupendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Mahakama.
“Hakuna
jaji aliyewahi kuteuliwa bila kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama, hiyo haijawahi kutokea. Majina yote yanapendekezwa na Tume na
hakuna jina linaloteuliwa nje ya mapendekezo ya Tume kwani huo si
utaratibu wa kikatiba,” alisema Jaji Chande.