KAMPUNI
ya Usafirishaji ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (UDART)
inatarajia kusitisha matumizi ya tiketi za karatasi ifikapo Julai 30
mwaka huu.
Uamuzi
huo unalenga kudhibiti foleni za kununua tiketi za karatasi kutokana na
idadi kubwa ya abiria; kati ya 150,000 na 200,000 wanaotumia usafiri wa
mabasi hayo kwa siku.
“Kwa
siku abiria wapatao laki moja na nusu hadi laki mbili wanatumia usafiri
wa mabasi yaendayo haraka kila siku, sasa kumekuwa na foleni vituoni na
pia tunakusanya magunia na magunia ya karatasi na kuna maeneo mengine
uchafu unakuwa mwingi,” Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa aliwaambia waandishi wa habari jana.
Hata
hivyo, kusitishwa huko kwa tiketi za karatasi, kunalenga watu wazima
pekee wanaolipa Sh 650. Wanafunzi wanaolipa Sh 200, wataendelea kutumia
tiketi za karatasi ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye vituo vya mabasi.
Mgwasa alisema licha ya hatua hiyo kulenga kupunguza foleni kwenye vituo, pia itaondoa uchafu unaotokana na tiketi za karatasi.
Wakati
huo huo, alisema kutokana na mpango huo wa kusitisha tiketi, kuanzia
leo kampuni imepunguza gharama ya ununuzi kutoka Sh 5,000 kwa tiketi za
hadi Sh 2,000, Sh 500 itakuwa gharama ya kadi na Sh 1,500 ni nauli.
“Kuanzia kesho (leo) kadi zitauzwa kwa gharama ya Sh 2,000 kwenye vituo vyote vya mabasi ya mwendokasi,” alisema.
Mgwasa
alisema tangu kuanza kuuzwa kwa kadi hizo kwa gharama ya Sh 5,000
tayari kadi 55,000 zimeshanunuliwa na kubakia kadi 150,000 ambazo ziko
kwenye promosheni ya kuuza kadi kwa Sh 5000.
Alisema
baada ya kadi hizo kuisha, abiria atalazimika kununua kadi hiyo kwa
thamani ya Sh 5,000 bila kuwekewa fedha za nauli kama ilivyokuwa awali.
Mkuu
wa Kitengo cha Biashara wa Maxcom Afrika (MaxMalipo), Deogratius Lazari
alisema wamejipanga kuhakikisha tiketi za kadi zinapatikana kwenye
vituo vya mabasi. Aliwataka wateja kuhakikisha wanaweka salio katika
vituo hivyo.
“
Kampuni za simu ziko katika hatua ya mwisho za kukamilisha mifumo yao
ili abiria aweze kuongeza salio kupitia mitandao ya simu ila kwa sasa
abiria wanatakiwa kutumia vituo vyetu vya mabasi na wakala wa max
malipo,” alisema.
Mabasi
ya haraka yalianza kutoa huduma Mei mwaka huu kwa kuanza na tiketi za
karatasi na baadaye, kuanzishwa utaratibu wa kadi ambao haujaitikiwa kwa
kiwango kikubwa.