MAJENGO
ya madarasa tisa, ofisi za walimu nne, maabara na vyoo katika shule ya
sekondari Lindi, vimeteketea kwa moto, unaodaiwa kutokana na hitilafu ya
umeme.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga aliwaambia waandishi wa
habari kwamba moto huo ulianza saa 7 usiku wa kuamkia jana.
Alisema kikosi cha Zimamoto kilifika eneo la tukio, lakini kutokana na tatizo la kiufundi, walishindwa kufanya kazi ipasavyo.
Kwa
mujibu wa kamanda, lililetwa gari la polisi lenye maji ambayo hutumika
wakati wa kutuliza ghasia maarufu kama ‘washawasha’ likasaidia kazi ya
kuzima moto, kabla ya kudhibitiwa kikamilifu asubuhi ya jana. Hata hivyo
alisema wakati jamii ikihangaika kuzima moto huo, mmoja wa watu
alikamatwa akidaiwa kuiba kompyuta mpakato.
Ingawa
hakuna mtu aliyekufa, kamanda alisema vifaa mbalimbali vilivyokuwamo
madarasani, ofisi za walimu na maabara, vimeteketea vyote.
Wananchi waliozungumzia ajali hiyo, walilalamikia utendaji wa kikosi cha Zimamoto kwa kusema si mzuri.
Kwa
mujibu wa mashuhuda, gari la Zimamoto lilipofika, madarasa mawili ndiyo
yaliyokuwa yameteketea lakini kutokana na kushindwa kuzima moto,
uliendelea kusambaa na kuteketeza madarasa tisa, ofisi za walimu na
vyoo.