Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewataka viongozi wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokatishwa tamaa na hali ya kisiasa
nchini hususan marufuku za mikutano yao ya kisiasa pamoja na misukosuko
mingine wanayopitia.
Lowassa
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ameyasema hayo jana jijini
Arusha alipokutana na Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zinazoongozwa
na Chama hicho.
Aliwataka
wasiogope bali washikamane zaidi na kutambua ukweli kuwa hakuna
Serikali yoyote duniani inayovipenda vyama vya upinzani.
Alisema
kuwa Chama hicho kinatakiwa kujikita katika kushikamana na wananchi
zaidi kwani uchaguzi wa mwaka jana ulionesha dhahiri kuwa wana imani na
vyama vya upinzani na hadi sasa bado wananchi wana imani kubwa nao.
“Kuna
uanaharakati na kuna siasa. Chama chetu cha Chadema ni hodari sana,
tume-graduate. Tumevuka ngazi ya uanaharakati. Uanaharakati ni mzuri
lakini unafika mahali unavuka ngazi katika kitu kingine ambacho ni chama
cha siasa,” alisema.
“Chama
cha siasa kazi yake ni kukamata dola. Hakuna kitu kingine duniani.
Kwahiyo mnapokaa hapa mnajipanga kukamata dola na sio kitu kingine.
Maandamano ni process tu, na sisi tumekaa hapa kutafuta namna ya
kukamata dola, wanataka hawataki wanajua hilo.
"Na
wenyewe watakazana kuzuia tusikamate dola. Mliona walivyotufanyia
kwenye uchaguzi, kwa gharama yoyote. Na sisi kwa gharama yoyote tutataka
tuwanyang’anye dola na ndio tunakuwa chama cha siasa,” aliongeza.
Alisema
kuwa CCM wanahofu kwakuwa bado wanakumbuka walichokipata wakati wa
uchaguzi mkuu uliopita na akawataka Chadema kutofanya kazi kwa mazoea
bali kukijenga chama kuanzia ngazi za mashina na matawi.
Katika
hatua nyingine, Lowassa aliwataka Chadema pamoja na vyama vingine vya
upinzani kulinda Ukawa kwani ndio chanzo kikuu cha mafanikio yao.
Alisema wanapotofautiana wakae chini na kutafuta ufumbuzi.
“Ndugu
zangu tulinde umoja wetu na tuhakikishe kuwa Ukawa inaendelea kuwapo
hasa. Umoja wetu ndio nguzo kubwa na tutumie busara kukosoana.
Tunapokosea tuache maneno ya mitaani. Tuwalinde viongozi wetu,” alisema.
Mwanasiasa
huyo mkongwe alitoa wito kwa viongozi hao wa halmashauri kuhakikisha
wanafanya kazi nzuri na kuwaletea maendeleo wananchi ili wasione ‘bora
CCM’.
Aliwataka
kuhakikisha hawaangalii maslahi binafsi bali maslahi ya wananchi na
kujieupusha na migogoro na viongozi wa CCM watakaotaka kuwakwamisha
katika shughuli zao.