Mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa
nafasi muhimu za uongozi serikalini unaofanywa na Rais John Magufuli,
hauzingatii hali halisi ya uwakilishi wa kijinsia.
Akizungumza jana
jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao
wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha ya kupiga kelele
tangu uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado
hali inaonekana kuwa tete kwa upande wa wanawake.
Alisema katika baraza
hilo, kati ya mawaziri 19, wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia
21.1 ya mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi wa baraza la Serikali ya
Awamu ya Nne ambalo lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na asilimia
33.3.
Alisema manaibu waziri kati ya 16 waliopo, wanawake ni watano sawa
na asilimia 31.25.
“Ukiangalia upande wa makatibu wakuu, walioteuliwa
ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7 huku wanawake
wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7 ya mwaka 2014 hadi
kufikia watatu sawa na asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi.
Alisema
uteuzi wa wanawake katika nafasi hizo umepungua kwa asilimia 10. Katika
nafasi ya wakuu wa mikoa, Liundi alisema idadi ya wanawake imeshuka
zaidi, kati ya wakuu wa mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni wanaume sawa na
asilimia 80 na wanawake ni watano sawa na asilimia mbili.
Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia 35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi umepungua kwa asilimia saba.”
Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi wanawake kwa nafasi ya ukuu wa wilaya.
Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia 35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi umepungua kwa asilimia saba.”
Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi wanawake kwa nafasi ya ukuu wa wilaya.
“Hii iko hata kwenye
nafasi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa
halmashauri, hatuoni idadi ya wanawake ikiongezeka na badala yake
inashuka,” alisema.
Mwakilishi wa Taasisi ya Women Fund Tanzania
(WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati ya mataifa duniani
yaliyoridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda
inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu ikiwamo ushiriki katika ngazi
zote za uamuzi, lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka
isukumwe na asasi za kiraia jambo linaloleta ukakasi.
Alisema miongoni
mwa mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu
(UDHR: 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi
dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba
wa Ziada wa Maputo na Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC).
Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo alisema Tanzania kupitia Dira ya
Maendeleo ya 2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa
uchumi ni pamoja na kuwa na jamii yenye maono ya kimaendeleo na
utamaduni wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.