MBUNGE
wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi,
ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa
Bujumbura.
Mossi
aliyewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika serikali ya
nchi hiyo, aliuawa jana katika barabara ya Gihosha eneo la Nyankoni.
Taarifa
zilizothibitishwa na Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurikiye
zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 4:00 asubuhi. Nkurikiye
alisema mbunge huyo alipigwa risasi kifuani kwenye moyo na kukimbizwa
katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako baadaye alipoteza maisha.
EALA
ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambacho wanachama wake
ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, ukiwa ni
umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa kibiashara huku ukikusudia kuwa na
sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.
Mkazi
wa eneo alikouawa Mbunge huyo, Achel Majabuka alisema kuwa alisikia
mlio wa risasi na baadaye kuona watu wawili wakiondoka katika gari baada
ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo hilo.
Kwa
upande wake, Bunge la Afrika Mashariki katika taarifa yake iliyotolewa
Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti
wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa risasi katika eneo la
Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.
Alimkariri
msemaji huyo wa Polisi akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu na nyumbani
kwake, huku Mbunge mwingine wa Burundi katika EALA, Emerence Bucumi
akithibitisha kifo hicho.
Spika
wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega alilaani mauaji hayo na
kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi aliyekuwa amejikita kusimamia na
kutetea utengamano wa ukanda huo.
Spika
huyo ambaye yuko Uganda kwa ziara ya kikazi, ameishauri Serikali ya
Burundi kuwatia nguvuni mara moja wauaji wa Mossi ambaye pia aliwahi
kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
“Ninatoa
salamu za rambirambi kwa serikali, familia, marafiki na wananchi wa
Burundi. Ninawaomba wawe watulivu katika wakati huu mgumu na ninaamini
mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka kuhakikisha waliohusika na
tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,” alisema Spika Kidega.
Kwa
upande wake, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alikielezea kifo cha
mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa kwa serikali yake. Naye Katibu
Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema amesikitishwa na kifo
hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada na kuwa jumuiya
imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.
Mwaka
jana, Mossi alitembelea wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na kulia,
ameuawa wakati mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yakiwa yanaendelea
kufanyika jijini Arusha.
Alikuwa
na Shahada ya Uandishi wa Habari na aliwahi kufanya kazi katika BBC na
alikuwa Waziri wa Burundi wa Masuala ya Afrika Mashariki hadi Juni 2012
alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.
Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano, Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005 hadi 2007.
Burundi, taifa katika Afrika Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.
Mgogoro
huo wenye kuendana na umwagaji damu, umesababisha watu 1,500 kuuawa,
huku ukiwahusisha wafuasi wa Rais Nkurunziza na wale wanaopinga ushindi
wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa mara ya tatu, wakidai kuwa ulikiuka
Katiba ya nchi hiyo.