Tume
ya kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoundwa na Rais John
Magufuli, imebaini madudu ukiwamo utapeli na usimamizi mbaya wa mali
hizo.
Kamati
hiyo iliyoundwa na Rais Magufuli kukagua mali za chama hicho, imefanya
kazi hiyo kwa miezi mitano ambapo imekusanya taarifa, kuhakiki na
kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya
mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.
Akikabidhi
ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk. Bashiru Ally, amesema tume yake pia
ilibaini usimamizi mbovu wa mali za chama.
Akielezea
namna tume hiyo ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo
mengine, tume iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za
usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya
mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.
Katika
ripoti hiyo, Dk. Bashiru ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa
wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi,
usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji
wa miradi ya chama.
“Uhakiki
huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu
mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa
zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za
mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,”
amesema.
Kwa
upande wake Rais Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa
iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati
Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“Nilipokuwa
nateua tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa
mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa
kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni
kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment