**
Hatimaye mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa amekuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, amepandishwa kizimbani na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199, wote kwa pamoja.
Mfanyabiashara
huyo, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake Alloyscious Gonzaga Mandago,
Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif
Kabla, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo jana katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa
wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha
nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha na
kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.
Katika
ya mashtaka hayo, Yusufali maarufu kwa majina ya Mohamedali, Choma au
Jamalii anakabiliwa na mashtaka 198 yeye peke yake huku wenzake
wakikabiliwa shtaka moja la utakatishaji fedha.
Kutokana
na wingi wa mashtaka hayo, waendesha mashtaka wawili; Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai walilazimika kubadilishana
ili kuwapa muda wa kupumua.
Kutokana
na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la kutakatisha fedha,
washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo
haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na kulingana
na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana.
Baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hivyo,
Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo aliamuru
washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Julai 25, kesi hiyo itakapotajwa
tena.
Kabla
ya kupandishwa kizimbani, Yusufali alitajwa na Rais Magufuli kuwa ana
mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzisambaza kwa wafanyabiashara wengine,
hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika.
Rais
Magufuli alieleza kuwa mtandao wake unawashirikisha watumishi wa TRA na
Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), hivyo kuisababishia Serikali
hasara ya mabilioni ya shilingi.
Katika
mashtaka hayo, Yusufali anakabiliwa na mashtaka 181 ya kughushi,
mashtaka 15 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, udanganyifu katika kulipa
kodi moja, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya
Sh15,645,944,361, huku shtaka moja tu la utakatishaji fedha ndilo
likimhusisha na wenzake.
Waendesha
mashtaka hao walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akighushi nyaraka
za kampuni mbalimbali, kuonyesha kuwa zimesajiliwa na zinaendesha
shughuli zake nchini kihalali wakati akijua siyo kweli.
Pia, walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasilisha nyaraka za uongo TRA.
Kuhusu
shtaka la kutakatisha fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa
hao kwa pamoja kati ya Machi 2011 na Januari 2016, walitakatisha
Sh1,895,88500 kwa kujifanya kuwa ni malipo ya mikopo waliyoipokea kwa
watu mbalimbali.
Upande
wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016,
mfanyabiashara huyo alifanya udanganyifu katika kuwasilisha kwa Kamishna
Mkuu wa TRA taarifa ya uongo ya marejesho ya mapato, hivyo kuikosesha
Serikali mapato ya kodi ya VAT zaidi ya Sh15.6 bilioni.