test

Wednesday, July 13, 2016

Mwalimu acharangwa mapanga kwa kumpa mimba mwanafunzi


Mwalimu wa Shule ya Msingi Geitasamo iliyopo Kata ya Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Raphael Charles (22) amenusurika kufa kwa kucharangwa mapanga kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ikorongo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Geitasamo, Marwa Meng’anyi alisema mwalimu huyo amejeruhiwa kwa kucharangwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni kaka wa mwanafunzi huyo baada ya kuchukizwa na kitendo cha dada yao (jina linahifadhiwa) kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito.

Akizungumzia tukio la kucharangwa mapanga, Mwalimu Charles alisema mkasa huo ulimkumba akiwa njiani kwenda nyumbani akiwa ameongozana na mwalimu mwenzake aliyemtaja kwa jina la Frank Batholomeo.

 “Tukiwa njiani ghafla walijitokeza na kuanza kunihoji kwa nini nimempa mimba mdogo wao, kabla sijajibu mmoja wao alichomoa panga na kuanza kunishambulia akilenga kunikata shingo,” alidai Charles. 

Alidai katika jitihada za kujinusuru ilimbidi kutimua mbio, lakini alianguka chini na vijana hao kufanikiwa kumfikia na kuendelea kumshambulia kwa mapanga.

Mwalimu huyo aliyefungua kesi kuhusu shambulio hilo na kupewa namba ya jalada Mug/RB/2886/2016 la kujeruhi, alidai alinusurika kuuawa baada ya mmoja wa mafundi pikipiki waliokuwa eneo jirani kujitokeza kumsaidia. 

Tukio la kushambuliwa kwa mwalimu huyo limekuja huku madai dhidi yake kumpachika mimba mwanafunzi huyo yakiwa yamefikishwa mahakamani kwa shauri namba 82/2016 tangu Mei 13.

Akizungumzia kitendo chake na wanawe kumshambulia kwa mapanga mwalimu huyo, baba wa binti aliyepachikwa mimba, Chacha Masiko alidai familia imechukizwa na kesi dhidi ya mwalimu huyo kuahirishwa mara kwa mara bila wao kuelezwa sababu za msingi, huku mshtakiwa huyo akiwatambia mtaani kuwa hatafungwa.

Mwalimu aliyeshuhudia mwezake akicharangwa mapanga, Batholomeo alilaani kitendo cha wanafamilia hao kujichukulia sheria mkononi na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

Kaimu Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Hawamu Tambwe alisema ameunda timu itakayoshirikiana na uongozi wa kijiji kuelimisha wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria katika kushughulikia changamoto na matatizo yanayojitokeza kwenye jamii badala ya kuchukua sheria mkononi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ngh’azi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kutokana na simu yake kuita bila kupokewa, lakini mmoja wa maofisa wa polisi wilayani hapa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema jeshi hilo linawasaka ndugu hao ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU