ALIYEKUWA
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro amesema hana mpango wa
kugombea nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho, licha ya kuwepo kwa msukumo
mkubwa wa kumtaka agombee.
Katika
taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Mtatiro alisema kwa
kipindi kirefu amekuwa akipata msukumo kutoka kwa viongozi wa chama
hicho ngazi ya wilaya, wabunge, wafuasi na makada wa chama hicho kumtaka
ashiriki katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uenyekiti.
“Katika
kipindi chote cha misukumo hiyo nimekuwa nikiwajibu wahusika wote kuwa
“sina nia ya kuchukua uongozi wa juu wa chama” kwa sababu bado nahitaji
muda wa kujiimarisha,” alisema Mtatiro katika taarifa yake.
Alisema
hata aliposhauri kuwa Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba anapaswa kupumzika wapo walioona kuwa anatumia nafasi
hiyo kuutaka uenyekiti wa CUF jambo ambalo alisema si kweli.
Aidha,
Mtatiro alisisitiza kuwa hajawahi kuwa na nia ya kuutaka uenyekiti wa
CUF lakini hadi sasa msimamo wake ni kuwa haungi mkono Profesa Lipumba
kurudi katika nafasi yake kwa sababu siasa za sasa zinahitaji viongozi
wapya na wanaoweza kutazama mambo kisasa kwa mahitaji ya kizazi kipya.
“...
Na kwa sababu Profesa Lipumba anayo heshima kubwa kwa CUF na
watanzania, ni muhimu zaidi alinde heshima yake na abaki kuwa mshauri
mkuu wa chama. CUF ya sasa inahitaji mwenyekiti imara anayeweza
kukisimamia chama na kikajijenga lakini pia mwenye uwezo na ushawishi wa
kufanya siasa za ushirikiano na haki,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata
hivyo, Mtatiro alisema anawatakia kila la heri wanachama wa CUF ili
waweze kuchagua mwenyekiti mzuri kwa ajili ya kukiendeleza chama hicho,
na kusisitiza kuwa jukumu lake litaendelea kukisaidia chama katika
masuala mbalimbali ya kiushauri.