WABUNGE
watatu kutoka Chama cha Wananchi (CUF) mikoa ya Lindi na Mtwara
wamepongeza kasi ya utendaji kazi ya Rais John Pombe Magufuli katika
kutatua kero za wananchi wa mikoa hiyo.
Wabunge
hao Bw. Selemani Said Bungara (Kilwa Kusini), Bw. Zuberi Mohammed
Kuchauka (Liwale) na Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) walitoa
pongezi hizo jana, (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati walipopewa nafasi ya
kusalimia wananchi kwenye mikutano ya hadhara ambayo Waziri Mkuu
alihutubia.
Akiwa
wilayani Lindi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuzindua
kituo cha kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa katika kijiji cha
Mahumbika, aliwapa fursa wabunge wote alioambatana nao katika ziara hiyo
maalum kwa ajili ya uzinduzi wa miundombinu ya nishati kwa mikoa ya
Kusini.
Akizungumza
na wananchi na viongozi wa taasisi mbalimbali mkoani humo waliohudhuria
uzinduzi huo, Mbunge wa Kilwa Kusini, Bw. Bungara ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Lindi alisema analishukuru Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuisimamia vizuri Serikali ya
CCM.
“Faida
ya demokrasia ya vyama vingi ni kwamba CCM bila CUF, CCM hakuna na CUF
bila CCM, kama ambavyo hakuna Simba bila Yanga wala hakuna Yanga bila
Simba. Tuwe kitu kimoja tu, Kusini kwanza, vyama baadaye!” alisisitiza.
Alitumia
fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa juhudi zake za kuwaunganisha
wabunge wa mikoa ya Kusini bila kuwabagua au kujali itikadi zao.
Naye
Mbunge wa Liwale, Bw. Kuchauka alisema: “Niwapongeze wewe Waziri Mkuu
pamoja na Mheshimiwa Rais Magufuli kwa yale ambayo mnayasimamia na
mnaamini kwamba yataleta ukombozi kwa wananchi wa Tanzania. Lazima
nikiri kwamba wakati mnazindua sera ya uchumi wa viwanda, nilikuwa
siamini katika hiyo sera yenu kwa sababu niliona ni moja ya mbinu zenu
za kututenga sisi watu wa mikoa ya Kusini.”
“Niliona
hivyo kwa sababu nilijiuliza unawezaje kuwa na uchumi wa viwanda wakati
huna nishati ya uhakika ya umeme? Sasa nimeona mwanga kwamba mikoa ya
Kusini nayo inaweza kushiriki kwenye uchumi wa viwanda,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema
hivi sasa hakuna asiyeona mambo yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya
tano kwani dunia yote imekuwa kama kijiji na lolote linalofanywa na
Mhe. Rais au Waziri Mkuu hakuna asiyejua. “Lolote analolifanya
Mheshimiwa Rais au wewe Waziri Mkuu Watanzania wote watalijua, hakuna
asiyeliona. Hivi sasa hakuna haja ya kubishana nani kafanya nini, jambo
kubwa ni kuungana na tuangalie Tanzania yetu. Vyama vyote baadaye,
Kusini kwanza,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Bw. Maftaha alisema mwaka 2006
baada ya kuhitimu kidato cha sita, alipangiwa afanye mafunzo ya ualimu
kwa vitendo katika shule ya sekondari Mingoyo, eneo la Mnazi Mmoja
lakini alitafuta nyumba ya kuishi yenye umeme hakupata.
“Wakati
ule nyumba zenye umeme zilikuwa hazizidi hata 10, na kulikuwa na simba
na wadudu wa kila aina. Leo nafarijika kuona kwa kasi ya ajabu, ninyi
viongozi tuliowapa dhamana, mnatumia rasilmali za nchi hii, mnasambaza
umeme kwa wananchi wa mikoa ya Kusini, na pale Mnazi Mmoja leo hii,
umeme siyo tatizo tena.”
Wabunge
wengine waliofuatana na Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bibi Hawa Ghasia;
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bi. Hamida Mohammed
Abdallah (Viti Maalum). Mbunge wa Nachingwea, Bw. Hassan Elias Masala,
Mbunge wa Nanyamba, Bw. Abdallah Dadi Chikota.
Waziri
Mkuu alizuru pia mkoa wa Mtwara na kukagua ujenzi wa bandari, ukarabati
wa mabomba ya kupokelea mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta, kuzindua
upanuzi wa kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuzungumza
na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa bandari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment