Mahakama
ya Wilaya ya Ilala, imeyatupilia mbali maombi ya kuzikwa Tanga mwili wa
Andrew Daffa, aliyefariki dunia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya
Amana, Dar es Salaam.
Mwili
wa Daffa ulizuiwa kuzikwa kutokana na maombi ya kesi ya madai namba 240
ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na baba yake, Charles Joseph ambaye
alitaka apewe kibali cha kumzika mwanaye Kijiji cha Vigiri mkoani Tanga
alikozaliwa.
Mvutano
huo ulijitokeza baada ya mke wa marehemu, Glory Charles kutaka kupewa
haki ya kuzika mwili wa mumewe katika makaburi ya Kwa Jimmy yaliyopo
Yombo Vituka.
Glory aliieleza Mahakama kuwa eneo hilo ndilo walilozika watoto wao watano, ambao alizaa na mumewe.
“Kwa
sababu mume wangu alikuwa anaishi na mimi Tabata Kimanga na nilimuuguza
mpaka dakika ya mwisho bila kupata msaada wa ndugu yeyote, naomba
Mahakama inipe kibali cha kumzika kwani na mimi nina haki kama mke,” alidai Glory,
Akitoa
uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Adelf Sachore
alisema Mahakama inatupilia mbali maombi ya baba wa marehemu, hivyo
inaamuru mwili huo apewe mke wake.
“Maombi ya baba wa marehemu yanatupiliwa mbali, Mahakama inaamua mwili huo uzikwe walikozikwa watoto wake waliofariki dunia,” alisema.
Hakimu
Sachore alisema katika kesi hiyo, Wakili wa utetezi, Daniel Buma alidai
marehemu anatakiwa azikwe mkoani Tanga kwa madai kuwa ndiyo mila zao
zinavyoeleza kwa sababu hana makazi ya kudumu Dar es Salaam.
Hata
hivyo, Mahakama ilipokea vielelezo kutoka kwa mlalamikiwa (Glory)
ambavyo ni cheti cha ndoa na picha za watoto wao waliokufa na vyeti vya
watoto waliopo.
Baada
ya kutolewa uamuzi huo, Glory alibubujikwa machozi ya furaha na kuomba
Mahakama impe ulinzi wakati wa mazishi ya mumewe yanayotarajia kufanyika
leo katika makaburi ya Yombo Vituka.