Askari
watano wa Jeshi la Polisi jana waliuawa kwa kudunguliwa na mtu
asiyejulikana mitaa ya Dallas nchini Marekani, wakati wa maandamano
makubwa ya kupinga mauaji ya watu wawili weusi yaliyofanywa na askari wa
kizungu wiki hii.
Ripoti
ya jeshi la polisi limeeleza kuwa mbali na askari hao waliouawa, askari
wengine wanne wa jeshi la polisi na afisa mmoja wa usafiri wa mwendo
kasi walijeruhiwa vibaya.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi wa Dallas, David Brown aliwaambia waandishi wa
habari kuwa maafisa wa Polisi walikuwa katika hatua za kumtia nguvuni
mtuhumiwa mmoja kutokana na tukio hilo, na kwamba wakati wanajaribu
kuzungumza naye akiwa mbali akiwa ameshikilia bunduki alieleza kuwa
alikuwa amekasirishwa na vitendo vya mauaji ya polisi wazungu dhidi ya
weusi yaliyofanyika Alhamisi.
“Alisema alitaka kuwaua wazungu,” Brown alieleza.
Baada
ya majibizano ya risasi na mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Micah Xavier
Johnson, polisi walituma robot lenye vilipuzi ambavyo vilimuua.