WAKALA
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), inakusudia kuzifutia usajili
bodi za udhamini 680 za taasisi mbalimbali; ambazo zimekiuka masharti,
ikiwa ni pamoja na kutokuwa hai.
Aidha,
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuruhusu wakala huo
kuanza kusajili bodi za udhamini; huku akiutaka kuhakikisha bodi
zitakazosajiliwa zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Akizungumza
jana Dar es Salaam katika mkutano wa Bodi ya Wadhamini ya Rita, Dk
Mwakyembe alisema, wakala huo unatakiwa kuzifuta haraka bodi hizo ili
kuwepo na bodi chache ambazo ziko hai.
“Mmefanya
kazi nzuri ya kuhakiki baadhi ya hizi bodi, endeleeni kuhakikisha tuna
vyombo vichache ambavyo viko hai…kuna bodi kama 500 ambazo haziko hai na
mnakusudia kuzifuta, zifuteni haraka,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema
serikali imedhamiria kudhibiti mapato na ndio sababu katika mkutano
wake na Bodi ya Rita alitoa agizo kwa wakala huo kusitisha usajili mpya
wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti, makanisa na taasisi mbalimbali
huku akitoa siku 90 wakala huo ukamilishe uhakiki wa bodi hizo.
Alisema
baadhi ya vikundi hivyo ambavyo vingine vimekuwa vikiibuka wakati wa
kampeni na uchaguzi vimekuwa vikitumika vibaya kupata misamaha ya kodi
na vingine kuomba ruzuku.
Dk
Mwakyembe alifafanua kuwa katika kikao chake na mamlaka zote
zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na
asasi mbalimbali ulikuwa na lengo la kuimarisha taratibu za usajili ili
kudhibiti utitiri wa vikundi hivyo.
Aidha,
alisema mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa
mamlaka hizo ili mifumo yao iweze kuwasiliana ili kulinda maslahi mapana
ya Taifa.
Awali Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema, tayari tangazo la kusudio la kuzifutia usajili bodi za wadhamini limeshaandaliwa na litatolewa muda wowote kuanzia sasa.
Awali Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema, tayari tangazo la kusudio la kuzifutia usajili bodi za wadhamini limeshaandaliwa na litatolewa muda wowote kuanzia sasa.
Alisema
jumla ya bodi za wadhamini zilizosajiliwa ni 5,262 ambazo kati ya hizo
zilizohakikiwa ni 1,544 na kwamba katika uhakiki huo walikumbana na
changamoto ya malalamiko kutoka kwa bodi hizo kuwa nyingine ziko mbali.
Hudson alisema kati ya hao 5,262 ambao wako kwenye kanzi data ya wakala huo walichambua na kubaini walioko hai ni 4,287 pekee.
“Bodi
za Udhamini 500 zimebainika kuwa haziko hai…zoezi la kuingiza taarifa
kwenye databae (kanzidata) linaendelea lakini pia tunaomba tuongezewe
muda au ikiwezekana liwe endelevu,” alisema.
Alisema
kabla ya kuanza kwa uhakiki wa bodi hizo tayari walikuwa na idadi ya
bodi 200 ambazo zilitakia kufutiwa usajili na zilipelekewa notisi za
kufutiwa usajili wao ambapo kati ya hizo 20 tu ndizo zilizojibu na
kuomba kutofutiwa usajili wao.
Hata
hivyo, alisema wakala huo umekuwa ukikabiliana na changamoto mbalimbali
ikiwemo za taasisi kumiliki mali bila kuwa na idhini ya bodi ya
wadhamini kinyume cha sheria, muda wa kutembelea taasisi hizo kuwa
mdogo, baadhi ya taasisi kubadili majina na anuani zao bila kutoa
taarifa.
“Lakini
pia tumebaini kuwepo kwa baadhi ya bodi ambazo hazitambui wajibu wao na
pia mkanganyiko wa tafsiri ya sheria kutoka katika taasisi mbalimbali
zinazoshughulika na usajili,” alisema Hudson.
Kazi kubwa zinazofanywa na bodi za udhamini ni kusimamia rasilimali fedha pamoja na uendeshwaji wa kampuni au taasisi husika.