Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii iliyoanza
mwezi huu, imezishtua nchi 30 za Ulaya ambazo zimeiandikia barua
Serikali ya Tanzania zikiomba ifikirie upya au isianze kutumika hadi
mwaka ujao.
Kodi hiyo, ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kukusanya
mapato ili kuondokana na utegemezi, ilitangazwa kwenye Bunge la Bajeti
lililopita na tayari Sheria ya Fedha imeshapitishwa kubariki matumizi
yake, licha ya wabunge kuipinga kwa maelezo kuwa itazipa nchi washindani
mwanya wa kukuza utalii.
Dk Philip Mpango alisema walipata wazo la
kuanzisha kodi hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya, lakini wakati
akitangaza hayo waziri mwenzake wa nchi hiyo alitangaza kuiondoa baada
ya utalii kuathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi.
Wakati
sheria hiyo ikianza kutumika nchini, nchi hizo za Ulaya ambazo ni wadau
wakuu katika sekta ya utalii zimemwandikia barua hiyo Dk Mpango, naibu
wake, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe.
Chama cha Kitaifa wa Mawakala wa Usafiri na
Wasimamizi wa Utalii (ECTAA) kutoka nchi 30 za Ulaya ndicho
kinachoziwakilisha kampuni zaidi ya 70,000 za utalii barani humo. Nchi
hizo ndizo zinazotoa asilimia 50 ya watalii wote duniani.
Katika
barua yao iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa ECTAA, Michel de Blust, nchi
hizo zilieleza wasiwasi wao kutokana na utambulishwaji wa ghafla wa kodi
hiyo katika huduma za utalii, zikisema uamuzi huo unaongeza gharama za
safari nchini.
“Najua utakubaliana na mimi kuwa kodi ina umuhimu
wake na ina madhumuni yake, lakini inaweza kubadili mawazo ya watalii
na wakachagua maeneo mengine,” inasema barua ya Blust.
Waziri wa
Fedha na Mipango, “Mfano mzuri ni Kenya, utambulishaji wa kodi katika
huduma za utalii mwaka jana ulishusha idadi ya watalii kwa asilimia nne
na baadaye Kenya waliamua kuachana na kodi hiyo ili kudumisha ushindani
wake.”
Barua hiyo inasema kodi hiyo katika huduma za utalii
itaathiri waandaaji wa safari za watalii wanaotoa huduma nchini kwa
sababu hakukuwa na tangazo la kuwaandaa kabla ya kuanzishwa kwa tozo
hiyo.
“Waandaaji wa safari wa Ulaya wanawajibika na sheria
inayomlinda mteja, hivyo wanatakiwa wawe wanafahamu bei na kodi mpya
kabla. Kwa sasa ni vigumu mno kwa waandaji kubadili bei zao ghafla,”
inasema barua hiyo.
Kadhalika, barua hiyo inaeleza kuwa Wakala
wa Utalii wa Tanzania uliwasiliana na Wakala wa Ulaya kuhusu kodi hiyo
na mawakala wa Ulaya wanatafakari kama wanaweza kuingia gharama hiyo au
kujiondoa katika mpango huo.
“Kama kodi hii ikiahirishwa, basi
waandaaji wa safari za watalii watajipanga kuingia gharama hizi na
kubadili mfumo wote wa huduma hizo Ulaya,” inasema barua hiyo.
Hivi
karibuni, Waziri Maghembe alinukuliwa kwenye mkutano wa Shirika la
Hifadhi za Taifa (Tanapa), akisema kuwa Serikali haitabadili msimamo
huo.
Alisema Sh7 bilioni wanazotarajia kupata kwa kutoza VAT
kwenye huduma za utalii, zitawapa uwezo wa kutangaza utalii nje ya nchi
na kuziba pengo la bajeti linalotokana na kushuka kwa utalii wa
uwindaji. Alisema VAT itakayokatwa ni asilimia 18 ya kitu
kilichonunuliwa na inatozwa wakati wa kununua huduma ya utalii.
Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi
alisema hajaiona barua ya ECTAA, lakini akasema watafanya kikao na Chama
cha Wafanyabiashara za Utalii Tanzania (Tato) ili kujadili nini
kifanyike ili sekta ya utalii isiyumbe.
“Hili ni suala mtambuka
na hii VAT ilipitishwa na kikao cha bajeti, wizara kwa sasa haina la
kufanya zaidi ya kutafuta njia mbadala ili sekta isiyumbe,” alisema.
Tovuti
kwa ajili ya watalii ya Afrika, Safaribookings.com imeeleza kuwa
wamekuwa wakipata barua pepe kutoka kwa wateja ambao wamepewa taarifa
kutoka kwa wasimamizi wa watalii kulipa fedha za ziada.
Marc
Harris, mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania Odyssey inayotoa huduma za
kitalii na yenye makazi yake nchini, aliliambia gazeti la Daily
Telegraph la Uingereza kuwa kodi mpya ni janga kubwa ambalo
halikutarajiwa na wengi.
“Watanzania wanaweza kufanya chochote
kuhusu kodi, lakini suala la muda ndiyo tatizo. Wametupa taarifa hizi
Juni 23, wiki moja tu kabla ya kodi kuanza kutozwa,” alikaririwa na
gazeti hilo.
Alisema gharama kubwa itaonekana kwenye malazi ambayo inaonekana kuongezeka kwa asilimia saba.
“Kinachoshangaza ni kuwa Hifadhi za Taifa hazijasajiliwa VAT, lakini inatoza fedha hizo. Sijui watazitumiaje,” alisema Harris.
Mmiliki wa kampuni ya kitalii ya Safaribooking.com, Wouter Vergeer alisema muda mfupi waliopewa umewashtua.
“Maelfu
ya wateja wameshtushwa na chaji hizo ambazo hazikutarajiwa. Wengi
hawajapata muda wa kujipanga kwa tozo hizo, hata risiti zenyewe za VAT
hatuna,”alisema.