HUZUNI
imetanda katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, baada ya ajali ya moto
wa kibatari kuteketeza watoto wanne wa mama mmoja, waliokuwa wamefungiwa
chumbani na dada anayewalea.
Ajali
hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Nyerere, mji mdogo
wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakati mama wa watoto hao aliposafiri
kwenda shambani Kiteto mkoani Manyara, kwa ajili ya kuvuna mazao na
kuwaacha watoto wake mikononi mwa dada, aliyekuwa akimsaidia kuwalea.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro
Mambosasa alisema chanzo cha ajali hiyo ni mlipuko wa kibatari
kilichokuwa ndani ya chumba walicholala watoto hao, ambacho kilichoma
godoro na kuteketeza nyumba yote.
Moto
huo ulioanzia katika chumba hicho, umeelezwa kuteketeza nyumba yote ya
vyumba sita iliyojengwa kwa tofali za udongo mali ya Nelson Mdachi.
Kamanda
Mambosasa aliwataja watoto hao kuwa ni Elizabeth Nelson (11) mwanafunzi
wa darasa la saba, Samweli Mdachi (7) anayesoma darasa la kwanza na
Nase Mgomba (9) anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Miembeni
na Peter Lema (9) mwanafunzi darasa la tatu shule ya msingi St Paulo.
Kutokana
na ajali hiyo, Kamanda Mambosasa amewakumbusha wazazi wasiache watoto
peke yao nyumbani kwa kuwa ni hatari kwani ajali ikitokea ni vigumu
kuokolewa.
Taarifa
kutoka kwa watu wa karibu na majirani wa familia hiyo, zimedai kuwa
mama wa familia hiyo alikwenda shambani kuvuna mazao katika wilaya ya
Kiteto, mkoani Manyara na kuwaacha watoto hao chini ya uangalizi wa
msichana aliyefahamika kwa jina moja la Ester.
Kwa
mujibu wa madai yao, ilipofika usiku Ester anayetajwa kuwa na jukumu la
kulea watoto hao, alitoka na kwenda kusikojulikana huku akiwafungia
watoto hao kwa nje.
Mkazi wa Kibaigwa, Denis Luhunga, alipozungumza na mwandishi kuhusu ajali hiyo alidai kuwa kibatari kilipolipuka, kilisababisha godoro kushika moto na kuteketea kwa watoto hao.
“Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa ndani,” alidai Luhunga.
“Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa ndani,” alidai Luhunga.
Kuhusu
alipo baba wa familia hiyo, mkazi mwingine wa eneo la tukio hilo, Paulo
Sauli alisema baba wa watoto hao, aliyemtaja kwa jina la Nelson Mdachi,
alishakufa miaka mitatu iliyopita na jukumu la kuwalea aliachiwa mama
yao.
Alifafanua
kuwa baba huyo ambaye wakati wa uhai wake alifahamika kwa jina maarufu
la ‘Moja kwa moja’, alikufa baada ya kuanguka kutoka juu ya mti
alipokuwa akirina asali na tangu hapo, jukumu la kulea likabaki kwa mama
mzazi wa watoto hao.
“Tukio hilo limetusikitisha sana ni tukio baya maana wameteketea kabisa hajulikani nani ni nani,” alisema Sauli na kuongeza, “Hata Ester hafahamiki alipo, kuna watu wengi lakini tumemuangalia hapa msibani hatumuoni.”
Taarifa
nyingine kutoka eneo la tukio, zilidai kuwa Mdachi alizaa na mama huyo
watoto wawili na baada ya kufariki, mama huyo alizaa watoto wengine
wawili na wanaume wengine.