MAMLAKA
ya mawasiliano nchini (TCRA) imetoa onyo pamoja na kuutaka uongozi wa
Clouds TV kuomba radhi Watanzania kupitia taarifa zake za habari ndani
ya siku tano mfululizo kuanzia jana.
Adhabu
hiyo ilitolewa jana na kamati ya Maudhui ya TCRA, baada ya baadhi ya
wananchi hususani watazamaji wa kipindi cha ‘Take One’ kilichorushwa 28
Juni mwaka huu ambacho kilidaiwa kueleza masuala ya mapenzi ya jinsia
moja (Ushoga), kulalamikiwa kwamba kilikiuka maadili ya taifa.
Wakati
akisoma tamko la adhabu hiyo, Joseph Mapunda, Makamu Mwenyekiti wa
kamati hiyo alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya wajumbe wa
kamati kutafakari maelezo ya utetezi yaliyotolewa na uongozi waClouds
TV.
“Tumetafakari
kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na clouds tv kuhusu kipindi
chake cha Take One kilichorushwa hewani tarehe 28 June 2016 ambacho
kilikiuka baadhi ya kanuni za maadili ya utangazaji,” alisema Mapunda.
Aliongeza kuwa “kutokana
na kipindi hicho kuwakwaza pamoja na kuwasababishia usumbufu wananchi
hususan watazamaji kwa kuwasilisha mada inayozungumzia masuala ya
mapenzi ya jinsia moja (ushoga), Clouds TV inatakiwa kuwaomba radhi
watanzania wote na watazamaji.”
Alisema
taarifa ya kuomba radhi itoke siku tano mfululizo katika taarifa zao za
habari ya saa moja na nusu na ya saa tano usiku kuanzia siku ya kusomwa
hukumu, na kwamba uthibitisho wa taarifa hizo upelekwe TCRA siku ya
Jumatano tarehe 13 Julai 2016 kabla ya saa kumi jioni.
“
Hatua ya pili, Clouds Tv inatakiwa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza
na kuhakikisha inazingatia kanuni zote za utangazaji nchini katika
kutekeleza majukumu yake ya utangazaji,” alisema na kuongeza.
“Kamati
inawaonya vikali Clouds tv kwa kukiuka kanuni za huduma za utangazaji
(maudhui) ya mwaka 2005, namba 5(b), 5(c), 5(d) na 15(c) 16(2) uamuzi
huu umetolewa leo, haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi
ndani ya siku 30 tangu siku uamuzi unapotolewa.
Ruge
Mutahaba, Mkurugenzi wa Clouds Media Group alisema baada ya kutafakari
tamko la adhabu atatoa msimamo wake kama watakata rufaa au la.
“Tunaweza
tukarudi nyuma na kusema tufanye kazi ya kukata rufaa, kwa sababu
tunaamini na mimi nina simamia msimamo wangu kwamba tunapoambiwa
tunalinda maadili ya kitaifa, kupinga jambo lolote baya ni kulinda
maadili ya kitaifa,” alisema na kuongeza.
“Sasa
ukiambiwa kwamba ulipinga kwa namna ya ulivyo pinga ni tofauti kidogo
labda inaweza ikasaida kutengeneza mjadala mkubwa wa kujiuliza maadili
tunayotakiwa kuyalinda ni yapi.”
Mutahaba alisema
“Lakini moja kati ya kitu tunachokiona kina utofauti ni kuna baadhi ya
mambo yamezungumzwa ambayo sikumbuki kabisa kama yako kwenye kipindi,
kwa hiyo sijui wamezitolea wapi.”
Alisema kuwa ushoga ni tatizo na kwamba lazima alikemee na ataendelea kulikemea.
“Kwa
ajili ya kosa la kutaja neno shoga katika kipindi cha njia panda mwaka
2000, miaka minne iliyopita kwenye gazeti tulivyosoma neno ushoga
tukatozwa faini ya mil 5, haiwezekani miaka kumi na sita inapita kutaja
neno shoga kila siku mtu anapewa adhabu,” alisema