MMOJA
wa madereva waliosababisha ajali ya mabasi ya City Boy Jumatatu
iliyopita katika kijiji cha Maweni wilayani Manyoni, Jeremiah Semfungwe
(34), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na
makosa 30 ya kuua bila kukusudia.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joyce Minde, ilidaiwa
kuwa mshitakiwa Semfungwe alitenda makosa hayo Julai 4 mwaka huu saa
8.15 mchana wakati akiendesha basi T. 247 BCD mali ya Kampuni ya City
Boy kwa kuligonganisha na basi T.331DCE.
Wakili
Mkuu Mfawidhi wa Serikali, Zakaria Ndaskoi alidai kuwa siku ya tukio
mshitakiwa ambaye ni dereva na mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam,
bila kukusudia, alisababisha vifo vya abiria 30 kinyume na Kifungu 195
na 198 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.
Wakili
wa mshitakiwa, Francis Kitope aliiomba mahakama impe mteja wake dhamana
kwa kuwa chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kosa
hilo linadhaminika.
Hata
hivyo, Wakili wa Serikali Ndaskoi alipinga hoja hiyo kwa kudai kuwa kwa
kufanya hivyo usalama wa mshitakiwa utakuwa hatarini kwa kuwa ndugu wa
marehemu na majeruhi bado wana hasira kutokana na ajali hiyo kuwa bado
“mbichi”.
Aidha,
Ndaskoi ambaye alikuwa akisaidiana na Petrida Muta aliendelea kudai
kuwa majeruhi 54 wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na hatma yao
haijulikani hivyo si vyema mshitakiwa kupewa dhamana na kwamba
mshitakiwa mwingine, dereva Boniface Mwakalukwa ametoroka.
Mshitakiwa
hakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka
juu ya kesi za mauji na ameswekwa rumande hadi Julai 21 kesi yake
itakapotajwa tena.