Idadi
ya watu waliokufa katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya Kampuni ya
City Boy imeongezeka na kufikia 32 baada majeruhi aliyekuwa amelazwa
katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kufariki
dunia.
Ajali
hiyo iliyohusisha mabasi hayo wakati moja likitokea Dar es Salaam
kuelekea Kahama mkoani Shinyangana lingine likitokea Kahama kuelekea Dar
es Salaam, ilitokea saa tisa Jumatatu katika eneo la Maweni, Kata ya
Kintiku Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza
jana Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk
Ibehzi Ernest alisema kazi ya kutambua miili ya marehemu hao bado
inaendelea.
Alisema
hadi jana miili ya watu 25 waliokufa kwenye ajali hiyo ilikuwa
imetambuliwa na ndugu zao. Dk Ernest ambaye pia ni Daktari Bingwa wa
Ajali, Upasuaji na Mifupa alisema kati ya maiti 25 zilizotambuliwa 12
zimechukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
“Wengine wametibiwa na kuruhusiwa tumebaki na majeruhi watano ambao hali zao zinaendelea vizuri,” alisema.
Kwa
siku nzima ya juzi na jana watu walikuwa wakipishana kuwatambua ndugu
zao katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Dodoma. Kutokana
na miili kuharibika, ndugu hao walikuwa wakirudi mara mbili kuangalia.