MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachia huru wabunge watatu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuomba
rushwa ya Sh milioni 30.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kuwafutia mashitaka.
Wabunge
hao na majimbo yao katika mabano ni Kangi Lugola wa Mwibara mkoani Mara
maarufu kama ‘Nyoka wa Shaba,’ Suleiman Saddiq ‘Murad’ (Mvomero –
Morogoro) na Victor Mwambalaswa (Lupa – Songwe).
Awali
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiwa na Wakili
Emmanuel Jacob kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), waliieleza mahakama kuwa kesi hiyo imetajwa kwa ajili ya
washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Kishenyi
alidai mbali na kutaka kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, DPP
anaomba kuwafutia mashitaka yao kwa kuwa hana nia ya kuendelea na
mashitaka dhidi yao.
Baada
ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Mpale Mpoki aliiomba mahakama itoe
agizo ili apewe maelezo ya mlalamikaji. Hakimu Mwijage alisema, mahakama
imekubali ombi la DPP hivyo kuanzia sasa wabunge hao wapo huru.
Aidha,
alisema wakili Mpoki anatakiwa afanye juhudi kwenda katika ofisi za DPP
ili kupata taarifa hizo, kinyume cha hapo mahakama haiwezi kutoa amri
kwamba apatiwe maelezo hayo.
Baada
ya washitakiwa hao kuachiwa huru, ndugu na marafiki wa wabunge hao
waliokuwa wamefika mahakamani, walianza kuangua kilio cha furaha.
Akizungumza
kwa niaba ya wabunge wenzake, Lugola alisema watakaa na wanasheria hao
ili wajue nini cha kufanya kutokana na udhalilishaji waliofanyiwa na
Takukuru.
"Tumesikitishwa
sana na kitendo cha Takukuru walivyotufikisha mahakamani na kutushitaki
kwa kashfa ya rushwa na dunia nzima imetambua, lakini tangu tufike
mahakamani mioyo yetu ilimtanguliza Mungu na leo (jana) Mungu ametoa
majibu,” alisema Lugola.
Alisema
walikuwa wanajua kuwa kesi hiyo ni ya kutunga na ilijaa siasa kwa kuwa
awali Takukuru ilisema upelelezi umekamilika, lakini hawakuwa na
ushahidi na ndio maana wameamua kuifuta.
Kwa
mara ya kwanza wabunge hao walipandishwa kizimbani, Aprili mosi mwaka
huu wakidaiwa kuwa Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne
usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni jijini Dar es Salaam,
kwa pamoja wakiwa kama wabunge na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), waliomba na kushawishi kupewa
rushwa ya Sh milioni 30.
Inadaiwa
waliomba fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, kama kishawishi cha kutoa mapendekezo
ya hati safi kwa halmashauri hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kupandishwa
kizimbani kwa wabunge hao kulitokana na kashfa ya rushwa
iliyomsababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kupangua wenyeviti na makamu
wenyeviti kwa kuwaondoa kwenye kamati walizokuwa wanaziongoza.
Mabadiliko hayo yaliwagusa pia wabunge 27, ambao baadhi yao wanadaiwa
kujihusisha na vitendo vya rushwa.