WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku moja kwa uongozi wa Manispaa ya
Morogoro kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na
kuyatangaza kesho ( leo ).
“Mbali
na kutenga maeneo pia nawaagiza muwasaidie wafanyabiashara hawa kuunda
vikundi kulingana na aina ya biashara wanazozifanya ili kuwawezesha
kupata mikopo kwa urahisi kutoka katika taasisi za fedha” alisema.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumatano, Agosti 03, 2016) wakati
alipotembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi Msamvu unaojengwa kwa
ubia kati ya Manispaa ya Morogoro na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.
Awamu
ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kufunguliwa Agosti 12 mwaka huu
utakuwa ni kituo cha mabasi cha kwanza cha kisasa Tanzania ambapo Waziri
Mkuu amezitaka halmashauri zote zilizoko makao makuu ya mikoa nchini
kuiga mfano huo.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Madiwani la Manispaa ya
Morogoro na LAPF kwa kubuni mradi huo wa kisasa utawezesha abiria kupata
taarifa ya basi lilipo na muda litakapowasili kituoni hapo hivyo
kupunguza udanganyifu kutoka kwa mawakala wasiokuwa waaminifu.
Kwa
upande wake Meneja wa mradi huo Stanley Mhapa alisema mradi huo
umegharimu sh. bilioni 40 ambapo Manispaa inamiliki asilimia 40 ya hisa
na mfuko wa LAPF unamiliki asilimia 60.
“Mafanikio
ya mradi huu ni pamoja na kuiwezesha Manispaa kuongeza ukusanyaji wa
mapato kutoka sh 350,000 kwa siku hadi kufikia sh. milioni 1.7 kwa
siku,” alisema.
Mhapa
alisema mradi huo utakapokamilika utatoa huduma mbalimbali ikiwa ni
pamoja na huduma za kibenki, vibanda vya biashara, sehemu za chakula,
ofisi na sehemu ya mapumziko ya abiria na vibanda vya kukatia tiketi.