WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wafugaji wenye mifugo mingi nchini
kujiweka tayari kwa ajili ya kuhamia kwenye maeneo yatakayotengwa na
Serikali katika ranchi mbalimbali nchini ili waweze kufuga kisasa.
Pia
aliwataka wafugaji hao kushirikiana na Serikali katika kuboresha
miundombinu ya maeneo hayo ikiwemo ujenzi wa visima vya maji na majosho
ili ufugaji wao uwe na tija.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Agosti 03, 2016) wakati
alipotembelea kiwanda cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch
kilichoko wilayani Movomero.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alisema kitendo cha wafugaji hao kuhamia katika
ranchi kitawezesha mifugo yao kuwa na ubora kwa sababu aina ya ufugaji
wa sasa ya kutembeza mifugo umbali mrefu inasababisha ufugaji wao kuwa
na tija ndogo.
Akizungumzia
kuhusu uwepo wa kiwanda cha kuchakata nyama wilayani Mvomero Waziri
Mkuu alisema kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na
wafugaji kwa kuwa wafugaji watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani
hapo.
“Uwepo
wa viwanda katika maeneo yetu utatuwezesha kupunguza matatizo
tuliyonayo katika maeneo yetu ikiwemo suala la migogoro kati ya wafugaji
na wakulima. Viwanda ndiyo vitakavyotuondoa kutoka katika uchumi wa
chini hadi wa kati,” alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi na Mshauri wa kiwanda cha Nguru Hills Ranch,
Dunstan Mrutu alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe
300, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku kinatarajiwa kufunguliwa mwezi
Desemba mwaka huu.
Mkurugenzi
huyo alisema takriban asilimia 80 ya nyama itafungashwa na kuuzwa nje
ya nchi hasa Uarabuni kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania imebainika
kuwa na mvuto maalum katika nchi hizo.
“Mbali
na uwekezaji huu wa kiwanda cha nyama pia tunatazamia kuwekeza katika
mnyororo wa thamani kuanzia kusindika ngozi inayotoka kiwandani hadi
kuzalisha viatu, mikanda na bidhaa zote za ngozi na kupunguza uagizaji
wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” alisema.
Mrutu
alisema nia yao ni kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli wa kutaka
viwanda vizalishe viatu nchini kuanzia vya majeshi na wananchi wote
ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza kuuza bidhaa hizo.
Aliongeza
kuwa uwepo wa kiwanda hicho utatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kuuza
majani, mifugo na mazao ya chakula kama mtama, mahindi, ambapo tayari
wameanza kuhamasisha jamii za wafugaji na wakulima wa Mvomero,
Ngerengere na sehemu zinazozunguka eneo la kiwanda kuchangamkia fursa
hiyo.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wilaya ya Mvomero
kufanya mapitio ya mashamba ili kujua wamiliki wake na kama
hawajayaendeleza wachukue uamuzi wa haraka wa kuyatwaa na kuyarudisha
mikononi mwa Serikali.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo wakati akijibu ujumbe uliokuwa katika mabango
yaliyobebwa na wananchi wa kijiji cha Maji ya Chumvi wilayani Mvomero
waliosimamisha msafara wakati ukitokea kwenye kiwanda cha nyama.