Mshtakiwa
katika kesi ya kujiteka na kusambaza taarifa za uongo katika mitandao
ya kijamii, Abdul Nondo ameandika barua ya kumkataa Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Mkoa wa Iringa, John Mpitanjia, anayesikiliza kesi hiyo
kwa madai ya kuwa karibu na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Iringa.
Wakili
anayemtetea Nondo, Jebra Kambole ametoa sababu tano za mteja wake
kuandika barua hiyo tangu Mei 11, mwaka huu za kumkataa hakimu huyo
ikiwamo hakimu huyo kuonekana akiingia katika gari la Mkuu wa Upelelezi
na kwenda sehemu isiyojulikana, ambapo kutokana na hali hiyo, mteja wake
ameona haki haitatendeka.
Amedai sababu nyingine ni hakimu huyo kukutwa amekaa na Paul Kisapo ambae ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo.
Kwa
upande wake Wakili Upande wa Jamhuri, Abel Mwandalama amedai pamoja na
kupokea barua ya mshtakiwa kumkataa hakimu lakini ameona hayana msingi
katika kesi hiyo.
“Tunasema
hayo kwa kuwa Aprili 19, shahidi wa tatu katika shauri hilo alitoa
ushahidi wake na mshitakiwa hakuandika barua yoyote na hata kesi hiyo
ilipokuja tena Mei 10, mwaka huu hakuna barua iliyoandikwa iweje barua
hiyo kuandikwa Mei 11, baada ya mahakama hiyo kukubali vielelezo
vilivyotolewa na upande wa jamhuri kutumika kama ushahidi,” amedai
Wakili Mwandalama.
Baada
ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mpitanjia alisema uamuzi
wa kujitoa ama kuendelea na kesi hiyo utatolewa Mei 16, mwaka huu.
Nondo
anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kusambaza taarifa za uongo
akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, na kutoa taarifa za uongo akiwa mjini
Mafinga kwa askari Polisi kituo cha Mafinga Wilayani Mufindi.
0 comments:
Post a Comment