Mkazi wa Miembeni mjini Unguja, Hassan Juma amenusurika kifo baada ya kutolewa ndani ya kontena alikojifungia.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassri Ali alithibitisha
tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo.
Msimamizi
wa makontena katika Bandari ya Malindi, Ibrahim Abdallah jana alisema
chanzo cha Hassan anayekadiriwa kuwa na miaka 30 kuingia kwenye kontena
na kujifungia hakijajulikana.
Abdallah
alisema wakiwa katika kazi zao za kila siku eneo hilo juzi saa moja
asubuhi walisikia sauti ikitoka ndani ya kontena lililopo juu ya jingine
na kuzua taharuki miongoni mwao ikidaiwa ‘nakufaa’.
Alisema mtu huyo aliashiria kuomba msaada na walimuuliza yeye ni nani na alijitaja jina.
“Baada
ya kutaja jina tulifungua kontena hilo ambalo alikuwa amelifunga na
kumtoa akiwa na hali mbaya kiafya, tulimpeleka Hospitali ya Mnazi Mmoja
na kupatiwa huduma ya kwanza,” alisema.
Naye
msemaji wa hospitali hiyo, Hassan Makame alisema katika hatua za awali
wamempatia huduma ya kwanza ili kuhakikisha hali yake inarejea kawaida.
Alisema hajafanyiwa vipimo kutokana na hali yake kuonekana kudhoofu.
“Tumemtia dripu ili apate nguvu ili kuendelea na huduma nyingine za vipimo,” alisema Makame.
Kuli
katika bandari hiyo, Mohamed Khamis Makame alisema ni mara ya kwanza
kutokea tukio la aina hiyo eneo hilo, hivyo wanapaswa kuimarisha ulinzi.
0 comments:
Post a Comment