Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemwamuru mkurugenzi wa kampuni ya Tiptop
Connections Company Limited, Hamis Shaban Taletale maarufu kwa jina la
Babu Tale, kukaa mahabusu katika kituo cha Polisi akisubiri amri ya
kupelekwa kifungoni.
Mahakama
hiyo katika uamuzi uliotolewa na Naibu Msajili, Wilbard Mashauri
Februari 16, iliamuru Babu Tale na ndugu yake Idd Shaban Taletale
wakamatwe na kupelekwa kifungoni baada ya kushindwa kutekeleza hukumu
yake.
Hukumu
hiyo iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016, iliwaamuru
ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu,
Sheikh Hashim Mbonde kwa makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara
bila ridhaa yake.
Kutokana
na amri hiyo ya kuwakamata, Babu Tale alitiwa mbaroni juzi na jana
alipelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya amri ya kumpeleka kifungoni,
lakini alilazimika kurudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi kwa kuwa
Naibu Msajili aliyetoa amri ya kuwakamata hakuwepo.
Amri
hiyo ya kumrejesha rumande ilitolewa na naibu msajili wa mahakama hiyo,
Ruth Massam hadi hapo Naibu Msajili Mashauri aliyetoa amri ya kuwafunga
atakaporejea kutoka Dodoma alikokwenda kikazi.
Kwa
kuwa haijulikani ni lini atarejea, Babu Tale ambaye pia ni meneja wa
msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Abdul Nassib maarufu kama
Diamond Platnum, atalazimika kukaa mahabusu kwa muda usiojulikana mpaka
atakaporejea.
Hati
ya kuwakamata Babu Tale na ndugu yake ilitolewa April 4, mwaka huu
kutokana na maombi ya Sheikh Mbonde kupitia wakili wake Mwesigwa
Muhingo.
Sheikh
Mbonde aliwasilisha maombi hayo baada ya Babu Tale na nduguye kushindwa
kutekeleza hukumu hiyo, yaani kumlipa kiasi hicho walichoamriwa na
Mahakama wala kubainisha mali za kampuni yao, au zao binafsi, ili
zipigwe mnada kulipia fidia hiyo.
Katika
kesi ya msingi, Sheikh Mbonde aliieleza Mahakama kuwa Juni 6, 2013
aliingia makubaliano na kampuni hiyo ili irekodi mawaidha yake na
kuziuza kisha wagawane faida, lakini baada ya kurekodi masomo saba,
walimwambia kuwa walikuwa wameachana na mpango huo.
Alieleza
kuwa baadaye alibaini kuwa mikanda ya video ya mfumo wa DVD zenye
mawaidha yake zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali huku zikiwa na
majina na namba za simu za wakurugenzi wa kampuni hiyo, ndipo akafungua
kesi hiyo.
Baada
ya Sheikh Mbonde kuwasilisha maombi ya kuwafunga jela Babu Tale na
nduguye, mahakama ilimwelekeza Sheikh Mbonde kuwalipia wafungwa hao
watarajiwa pesa za chakula mahakamani na kumtaka pesa kwa ajili ya
matumizi mengine kuziwasilisha gerezani.
Kwa mujibu wa Mahakama, gharama za kuwahudumia wafungwa hao wakiwa gerezani ni kama ifuatavyo:
Vifaa
ambavyo ni taulo ya kuogea Sh12,000; godoro Sh40,000; mto wa kulalia
Sh10,000; chandarua Sh13,000; mashuka manne Sh48,000; kandambili
(malapa) Sh3000; mswaki na dawa ya meno Sh2,000 ambazo jumla ni
Sh128,000 kwa mtu mmoja na kwa watu wote wawili ni Sh256,000.
Chakula,
kifungua kinywa Sh7,000; chakula cha mchana Sh8,000; maji lita tatu
3,000, jumla Sh18,000 kwa mtu mmoja kwa siku na kwa wote wawili ni
Sh36,000. Wote kwa mwezi ni Sh1,080,000.
Pia, kuna fedha za tahadhari kiasi cha Sh800,000 kwa kila mfungwa na kwa wote wawili jumla ni Sh1,600,000.
Sheikh
Mbonde alisema kuwa tayari ameshawalipia wafungwa hao fedha za chakula
ya mwezi mmoja kiasi cha Sh1,080,000 na kusema ataendelea kuwalipia
kiasi kama hicho kila mwezi.
Alisema
fedha za matumizi mengine kama yalivyoainishwa na mahakama, ziko tayari
na kwamba hizo ataziwasilisha kwa uongozi wa gereza baada ya wafungwa
hao kufikishwa huko.
0 comments:
Post a Comment